Na
Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mbeya
Katika kuchagiza mapinduzi ya Kilimo nchini
Benki ya Kilimo-TADB imekabidhi zana za kisasa za kilimo kwa wakulima 15 kutoka
ushirika wa nguvu kazi Mwanavala ikiwa ni sehemu ya kutekeleza lengo kuu la
uanzishwaji wake.
Katika kufikia mapinduzi ya kilimo nchini
serikali imeweka sera na mikakati mbalimbali itakayowezesha nchi kufikia
mapinduzi hayo makubwa ikiwa ni pamoja na mkakati wa zana za kilimo wa mwaka
2006 ambao ulikuwa chini ya mpango wa maendeleo ya kilimo awamu ya kwanza (ASDP
I) lakini pia mpango wa maendeleo ya kilimo awamu ya pili (ASDP II).
Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda ameyasema
hayo tarehe 20 Juni 2021 wakati akizungumza na wakulima wa Mpunga katika kijiji
cha Imalilosongwe kilichopo kata ya Ubaruku wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.
Waziri Mkenda ameipongeza Benki ya Kilimo-TADB
kwa kuidhinisha mkopo wenye thamani ya Tsh Milioni 949 ambao umewezesha
upatikanaji wa zana za kisasa za kuvunia kwa wakulima 15 katika kata ya
Imalilosongwe wilaya ya Mbarali.
Pamoja na kukabidhi zana hizo kwa wakulima hao
Waziri Mkenda amesema kuwa zana hizo zitakuwa sehemu ya kuimarisha ufanisi wa
kazi na sehemu ya kupunguza upotevu wa mazao kwa kiwango kikubwa zaidi nchini
ambao unatajwa kuwa kati ya asilimia 15 hadi 40.
Matrekta hayo yaliyokabidhiwa na Waziri Mkenda
ni sehemu ya matrekta 15 ya kuvunia kwa wakulima wilayani Mbarali ambapo
miongoni mwao waliokabidhiwa zana hizo za kilimo ni vijana watatu wa kike.
Waziri Mkenda ameipongeza Benki ya TADB kwa
kuona umuhimu wa kuwakopesha wakulima zana hizo bora huku akionyesha kupendezwa
na utoaji huo wa mikopo kwa wakulima wanawake.
Waziri Mkenda amewataka wakulima hao
kuhakikisha kuwa wanatumia ipasavyo mashine hizo pamoja na kuzitunza vizuri ili
kuimarisha uyendaji kazi wao katika kilimo.
“Nitoe wito kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbarali
na vyombo husika vya ulinzi na usalama, naomba mshirikiane kwa pamoja na
wananchi hawa ili kulinda mashine hizi na kuepusha hujuma za aina yeyote kwa
mashine hizi kwa wakulima hawa” Amekaririwa Mhe Mkenda na kuongeza kuwa
“Mashine hizi zimenunuliwa gharama kubwa
hivyo ni muhimu pia kuvitunza na kuvilinda kwa ukaribu ili viweze kudumu na
kutuletea matokeo ambayo tunayoyatarajia”
Akitoa taarifa ya mikopo iliyotolewa na Benki
ya Kilimo Tanzania-TADB Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Ndg Japhet Justine
amesema kuwa hadi sasa TADB imetoa jumla ya Bilioni 300 katika minyororo ya
thamani ya mazao mbalimbali kama vile mahindi, kahawa, pamba, mbogamboga,
alizeti na matunda pia katika sekta ya mifugo na uvuvi ambayo imewanufaisha wakulima
milioni 1.8 nchi nzima.
Amesema kuwa pamoja na mikopo ya moja kwa
moja, TADB kupitia mfuko wa dhamana kwa wakulima wadogo wadogo (SCGS) imekwisha
idhinisha mikopo yenye thamani ya shilingi Bilioni 9.4 kwa wakulima 4,439
katika kanda ya nyanda za juu kusini.