……………………………………………………………….
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MKUU wa mkoa wa Pwani,Aboubakar Kunenge amewapa salamu ,vishoka wa kuchochea migogoro ya ardhi ,kuwa wakae mkao wa kuchukuliwa hatua kwani Pwani kwasasa si salama kwao.
Pamoja na hilo ,serikali ya mkoa imeamua kuunda timu maalum itakayosimamia migogoro hiyo ili kupunguza malalamiko na kesi za ardhi .
Kunenge aliyasema hayo wakati wa mkutano wa baraza la biashara na uzinduzi wa baraza la biashara mkoa wa Pwani.
Alieleza ,kuna malalamiko ambayo yapo ndani ya uwezo wa mkoa kuyatatua ,lazima kuzingatia sheria na kufanya maamuzi .
“Serikali inajipanga kumaliza maumivu kwa wale wenye kilio cha migogoro isiyokwisha upande wa ardhi wakiwemo wawekezaji na wafanyabiashara na wananchi “
“Ni lazima kuboresha mazingira ya biashara ili kuongeza pato hasa la mkoa na Taifa kijumla” aliongeza Kunenge.
Kunenge alielezea ,viwanda vinajengwa ,lakini haileti mantiki kama vinajengwa vingi kisha vinakufa ni bora kuviwekea mazingira bora ya uwekezaji ,kumaliza migogoro inayowazunguka kwa ustawi na maendeleo ya uwekezaji na Taifa kijumla .
Alibainisha ,anahitaji kujua changamoto zao kila wilaya ,fursa zilizopo ikiwemo EPZA na kuwepo Bandari wilaya ya Bagamoyo ili serikali iangalie namna ya kuondoa vikwazo vilivyopo.
Mkuu huyo wa mkoa aliitaka mamlaka ya mapato kuangalia na ya kuongeza walipa kodi badala ya kuongeza kodi hali inayosababisha kukusanya mapato hafifu.
Kunenge alitaka taasisi kama TANROADS ,TANESCO na DAWASCO kujiwekea mipango kazi ya kujua maeneo yenye mahitaji na ukubwa wa hitaji kila kiwanda ili kuyamaliza.
Nae katibu mtendaji baraza la biashara la Taifa ,dr. Godwil Wanga alifafanua kuwa , lengo la mabaraza ya biashara ni kuleta majadiliano ya karibu kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.
Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyabiashara ,wenye viwanda na kilimo ,Mkoa wa Pwani Saidi Mfinanga alisema changamoto zinazowakabili wawekezaji na wafanyabiashara na miundombinu mibovu ya barabara kutofikika maeneo yao husika ,ukosefu wa umeme na maji ya uhakika.
Pia kodi isiyo rafiki kwa wafanyabiashara na mahusiano yasiyo mazuri kwa baadhi ya wakusanya kodi na walipa kodi.