Daktari Bingwa wa maradhi ya kina mama na Uzazi wa Hospitali ya Mnazimmoja Ummulkulthum Omar akiwakilisha mada ya matatizo ya shindikizo la damu kwa mama wajawazito kwa maafisa elimu wa Wilaya huko Kidongo Chekundu Mjini Zanzibar .
Mtafiti mkuu wa utafiti kuhusu matatizo ya shindikizo la damu kwa mama wajawazito Omar Mwalim akiwasilisha matokeo ya Utafiti huo uliofanywa na kitengo cha maradhi yasio ambukiza kwa mikoa 5 ya Zanzibar huko Kidongochekundu Mjini Zanzibar .
Washiriki katika uwasilishaji wa matokeo ya Utafiti kuhusu matatizo ya shindikizo la damu kwa mama wajawazito wakijidaliana baada ya uwasilishwaji wa matokeo hayo, huko Kidongochekundu Mjini Zanzibar .
PICHA NA FAUZIA MUSSA /MAELEZO ZANZIBAR.
……………………………………………………………………………
Na Khadija Khamis – Maelezo.
Wizara ya Afya Ustawi wa Jamii Wazee Jinsia na Watoto imeitaka jamii kuwa na utamaduni wa kuchunguza afya mara kwa mara itasaidia kugundulikana mapema kwa maradhi ikiwemo maradhi yasioambukiza .
Ushauri huo umetolewa na Daktari Bingwa wa Maradhi ya Akinamama na uzazi katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja Dkt, Umulkurthum Omar wakati akisoma matokeo ya utafiti kwa wanafunzi wa vyuo vikuu pamoja na maafisa elimu wa wilaya katika ukumbi wa Hospitali ya Kidongo Chekundu.
Alisema tafiti zinaonyesha kuwa maradhi yasioambukiza ikiwemo presha, sukari na kensa ni tatizo sugu duniani kote, jambo linalopelekea ongezeko la vifo siku hadi siku hasa kwa mama wajawazito.
Aidha alisema maradhi yasioambukiza hasa presha huwaathiri zaidi akinamama wajawazito hivyo aliwataka akinamama wajawazito kuhudhuria klinik mapema ili kuchunguzwa afya zao na kupatiwa huduma za haraka .
“Iwapo wajawazito watahudhuria kliniki kwa wakati itasaidia kujulikana hali zao za kiafya mapema ili kupatiwa msaada wa haraka na kupata ushauri wa kuilea mimba yake ”alifhamisha Daktari Ummi.
Alisema kuwa kati ya akinamama wajawazito 100 wanaopata huduma katika hospitali kuu ya Mnazimmoja 25 hugundulika na Presha ambayo inasababishwa na msongo wa mawazo unaotokana na matatizo mbalimbali ya kimaisha.
Alieleza kuwa presha kubwa kwamama mjamzito hupelekea kifafa cha mimba ambacho husababisha kifo kwa mama au ulemavu wakudumu ikiwemo matatizo ya moyo na kufeli kwa figo
Alisema tafiti zilizofanywa za miaka mitatu kwa akinamama wajawazito waliojifungulia hospitali ya rufaa mnazimmoja zimeonyesha kuwa mnamo mwaka 2018 akinamama waliojifungua ni 11,734 waliopata presha kubwa yenye dalili ya kupata kifafa cha mimba ni 123 na waliopata kifafa ni 44 sawa na asilimia 1.14.
Katika mwaka 2019 akinamama waliojifungua ni 14,832 waliopata presha kubwa ambayo inapelekea kupata kifafa ni 348 na waliopata kifafa ni 54 sawa na asilimia 2.75.
Vile vile utafitiwa mwaka 2020 jumla ya akinamama wajawazito waliojifungua hospitalini hapo ni 13,529 waliopata presha kubwa ambayo inapelekea kupata kifafa cha mimba ni 331 na waliopata kifafa ni 44 sawa na asilimia 3.54.
Daktari Ummu alifahamisha kuwa utafiti uliofanywa ulionyesha uchelewaji wa akinamama wajawazito kliniki, ukosefu wa elimu na ushauri nasaha huchangia kwa kiasi kikubwa kukosekana kupatiwa matibabu kwa haraka .
Aidha alisema katika mwaka 2020 asilimia 28 ya vifo vya mama wajawazito vilichangiwa na sababu ya presha.
Nae Mkufunzi Dkt Omar Mwalimu amesema katika utafiti huo umeonyesha bado zipo imani potofu katika jamii zetu zinazochangia uzoroteshaji wa huduma kwa wajawazito jambo ambalo husababisha kifo.
Akitoa wito kwa wahudumu wa afya alisema kuwa iko haja kukaaa karibu zaidi na jamii ili kuwapa muongozo wa kiafya ambao utasaidia kuimarisha afya ya mama mjamzito na mtoto .
Utafiti huo kuhusu shindikizo la damu kwa mama wajawazito ulifanywa na kitengo cha maradhi yasioambukizwa ukijumuisha mikoa mitano ya Zanzibar .