NA KHALFAN SAID, MOROGORO
KATIKA kuhakikisha huduma za tathmini ya ulemavu uliotokana na ajali au magonjwa
yatokanayo na kazi zinawafikia walengwa huko waliko kwa haraka na kwa wakati, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umezidi kuongeza mtandao wa madaktari na watoa huduma za afya kwa kuwapatia mafunzo ya kufanya kazi hiyo.
Akizungumza mjini Morogoro wiki hii wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kufanya tahmini ya ulemavu uliotokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi madaktari na watoa huduma za afya 93 kutoka mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam
na Morogoro, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma alisema baada ya mafunzo hayo idadi ya madaktari na watoa huduma za afya
wenye ujuzi wa kufanya tathmini itaongezeka kutoka 1,085 iliyokuwepo na kufikia 1, 178 nchi nzima.
“Lengo ni kuongeza mtandao wa wataalamu wenye ujuzi kwenye hospitali za umma na
binafsi nchini kote ili kuondoa changamoto ya kuwafikia walengwa kwa muda na kwa haraka na hivyo kutoa tathmini stahiki na kwa wakati.” Alisema Dkt. Mduma
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Tathmini, WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar
akizunguzma wakati wa kufunga mafunzo hayo Ijumaa Juni 18, 2021 alisema mafunzo
hayo yaliendeshwa na wataalamu kutoka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kwa
kushirikiana na wataalamu wabobezi wa masuala ya tathmini za ulemavu uliotokana
na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.
“Tuna hakika watakuwa wamefaidika sana na utaalamu huu ambao ni mpya kwao na kwetu
sisi kama Mfuko tumedhamiria kwa dhati kuhakikisha huduma zetu zinafika kila
pembe ya nchi yetu na hivyo kurahisisha utoaji wa huduma kwa wafanyakazi
watakaopata matatizo hayo kazini.” Alisema Dkt. Omar.
Baadhi ya madaktari walioshiriki mafunzo hayo walieleza jinsi yalivyowawezesha kuwapa utaalamu na uwelewa kuhusu masuala ya fidia kwa wafanyakazi na jinsi
wanavyotakiwa kufanya tathmini kwa mtu aliyepata ulemavu uliotokana na ajali au
magonjwa yatokanayo na kazi kwa weledi.
“Nitakuwa balozi mzuri kwa wataalamu wenzangu kwenye kituo changu cha kazi kwani
nimeelewa kuwa tathmini za ulemavu uliotokana na ajali au magonjwa yatokanayo
na kazi, itafanyika tu pale mgonjwa atakapokuwa amepona na kwamba hakuna tena tatizo litakaloendelea baada ya matibabu (Maximum Medical Improvement-MMI) na sio kabla.”Alisema Dkt. Mohammed
Khalifa kutoka Hospitali ya Wilaya ya Newala mkoani Mtwara.
Naye Dkt. Noel Saitoti kutoka Hospitali ya Ekenywa jijini Dar es Salaam alisema
kabla ya kufika kwenye mafunzo hayo licha ya kuifahamu WCF kama ni Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi mafunzo yamesaidia kujenga uelewa zaidi wa majukumu ya
Mfuko kuwa ni zaidi ya kulipa fidia.
“Baada ya mafunzo haya nimejifunza kuwa Mfuko pia unatoa mafao mbalimbali kama vile
Fao la matibabu, na ikitokea mfanyakazi amefariki kutokana na kazi basi wale
wategemezi wanapata fidia.” Alisema Dkt. Saitoti.
Akieleza zaidi kuhusu manufaa aliyoyapata baada ya mafunzo, Dkt. Saitoti alisema mafunzo
aliyoyapata hakuwahi kujifunza hapo kabla, kwa hiyo ameongeza utaalamu kwenye
eneo maalum na kuupongeza Mfuko kwa kuandaa mafunzo hayo na kuomba mafunzo
yaendelee ili kuweza kuwapata wataalamu wengi zaidi wenye uwezo wa kufanya
tathmini.
“Nawaasa watoa huduma wenzangu (madaktari) tunatakiwa kuwa katikati yaani tutende haki,
kama mtu anastahili kupata mafao tufanye tathmini kama tulivyojifunza ili
kuusaidia Mfuko kutenda haki, kwa sababu mtu anayeonana na yule mgonjwa ni sisi
madaktari kwa hiyo maelezo ya kina kuhusu tatizo lililompata muathirika ni sisi
madaktari ndio tunaolibeba kwa hiyo tunaowajibu mkubwa wa kimaadili kuona
tatizo lilipo na kuwasilisha kwa Mfuko ili aweze kupata haki inayostahili.”
Alisema Dkt. Noel Saitoti kutoka Hospitali ya Ekenywa ya jijini Dar es Salaam.
Aidha Dkt. Husna Lusasi kutoka Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, yeye
alisema wilaya ya Mkuranga ina viwanda vingi sana na kumekuwepo na idadi kubwa
ya vijana wanaoumia kutokana na kazi hivyo pamoja na Mfuko kuwahudumia kwa
kuwapatia fao la matibabu na wakati mwingine fidia, kuna haja ya kufanya
ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha wenye viwanda wanatoa vifaa vya kujikinga kwa wafanyakazi wao na wawe wanavitumia.
“Tuwasaide vijana hawa kwa kufanya ukaguzi wa mazingira ya kazi wa mara kwa mara ili
tuwanusuru na ajali, taifa linahitaji nguvu kazi hii kwa ajili ya maendeleo.”
Alisema Dkt. Lusasi.
Mafunzo haya yametupa elimu kuu mbili mosi ni kwa waajiri kutambua watumishi wao
wanatakiwa kuwa kwenye mazingira sahihi na salama ya kazi mfano kwa kutoa
vitendea kazi maalum kwa ajili ya kuwalinda wakiwa kazini na pili ikibidi
mfanyakazi kaumia au kuugua kutokana na kazi basi mfuko utatoa matibabu sahihi
ili waweze kurudi kazini mapema iwezekanavyo.
Akifunga mafunzo hayo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Ukio Kusirye aliwataka
madaktari hao kuitumia elimu iliyotolewa katika mafunzo hayo ili kuwawezesha
kufanya tathmini ya ulemavu (Impairment Assessment) kwa ufanisi na uweledi wa
hali ya juu na hatimaye kuwasaidia wagonjwa na kusaidia Mfuko utimize lengo la
kutoa fidia stahiki na kwa wakati.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano, Mfuko wa Fidia
kwa Wafanyakazi (WCF), Laura Kunenge akimkabidhi stika ya WCF, Dkt. Sechelela
Pesse kutoka Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Temeke, jijini Dar es Salaam, wakati wa
hafla ya kufunga mafunzo ya siku tano kuwajengea uwezo madaktari na watoa
huduma ya afya ya jinsi ya kufanya tathmini za ulemavu utokanao na ajali na
magonjwa yatokanayo na kazi mjini Morogoro Juni 18, 2021. Stika hiyo
itabandikwa hospitalini hapo ili kuonyesha kuwa huduma za tathmini kwa
mfanyakazi aliyeumia au kuugua kutokana na kazi zinapatikana.
Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Tathmini, WCF, Dkt. Abdulsalaam Omary akijibu na kufafanua hoja mbalimbali za washiriki kuhusu masuala ya tathmini na utaratibu wakuwasilisha madai