Mratibu wa Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA Leonard Thadeo akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuhitimishwa kwa michezo ya UMITASHUMTA katika uwanja wa Nangwanda mjini Mtwara leo
Baadhi ya wanariadha walioshiriki mashindano mbalimbali ya UMITASHUMTA katika uwanja wa Chuo cha Ualimu Mtwara, mashindano ambayo yamemalizika leo mkoani Mtwara.
*******************
Na Mathew Kwembe, Mtwara
Wanafunzi 10 wa kitanzania wenye umri wa chini ya miaka 15 ambao walishiriki mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa shule za Msingi (UMITASHUMTA) wamechaguliwa kujiandaa kushiriki mashindano ya kimataifa ya riadha ambayo yamepangwa kufanyika mjini Belgrade nchini Serbia.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha mashindano ya UMITASHUMTA leo mjini Mtwara, Mratibu wa mashindano hayo, Leonard Thadeo amesema wanafunzi waliochaguliwa kesho wataanza rasmi kambi ya mazoezi hapa Mtwara kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya kimataifa ya riadha ya shule ambayo yamepangwa kufanyika mwezi septemba mwaka huu.
Amesema kwa kipindi chote cha mashindano ya UMISSETA wanafunzi hao 10 watakuwa kambini wakifanya mazoezi na baada ya hapo watarudi katika shule zao kuendelea na masomo.
Mratibu huyo ameongeza kuwa wanatarajia kuweka kambi nyingine ya maandalizi jijini Dar es salaam kabla ya safari ya Belgrade kwa ajili ya kukimbia kwenye tatan, wazoee tatan na kukimbilia viatu ili baadaye waweze kwenda kushiriki katika mashindano ambayo yataanza tarehe 11 hadi 19 septemba, 2021 huko Serbia.
Mashindano haya ya kimataifa ya riadha mwanzoni yalipangwa kufanyika nchini Slovenia kabla ya kuhamishiwa mjini Belgrade nchini Serbia.
Akizungumzia tathmini yake kwa mashindano ya UMITASHUMTA ya mwaka huu yaliyohitimishwa leo mjini Mtwara, Mratibu Thadeo amesema mashindano hayo yamefanyika kwa mafanikio makubwa kwani mbali na kutoa wanafunzi 10 bora wa riadha watakaokwenda Serbia, ushindani wa michezo mbalimbali ya mashindano hayo umeongezeka.
Mathalani mchezo wa mpira wa goli mwaka 2015 wakati ulipoanza kushindanishwa katika UMITASHUMTA timu zilizokuwa zinashiriki ni tano tu lakini sasa mikoa 23 kati ya 26 imepeleka timu kwenye mcheo huo.
Kadhalika bingwa wa jumla wa UMITASHUMTA mwaka 2019 Tabora safari hii ameshika nafasi ya saba, na hata timu kama Geita ambayo ndiyo walikuwa mabingwa wa soka mwaka 2019 safari hii haikufanikiwa na badala yake Dar es salaam wakafanikiwa kulichukua kombe hilo.
Thadeo amesema msisimko wa michezo hii hasa kwa wanafunzi imeongezeka sana mwaka huu kulinganisha na miaka ya nyuma kutokana na michezo hiyo kutofanyika mwaka jana baada ya COVID 19 kutokea.
Hata hivyo Mratibu Thadeo amesema kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Corona hasa katika nchi za jirani, mashindano ya shule za sekondari kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki FEASSA ambayo ilipangwa kufanyika katika mji wa Nakuru nchini Kenya haitafanyika mwaka huu.