Balozi wa Finland nchini Tanzania, Mhe Riitta Swan akimkabidhi picha Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga
Balozi wa Finland nchini Tanzania, Mhe Riitta Swan akimkabidhi kitabu Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga
Kushoto ni Balozi wa Finland nchini Mhe Riitta Swan, akijaza fomu maalumu ya Makumbusho ya Taifa ya kukabidhi mikusanyo, huku akishuhudiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga (wapili kushoto), Mkurugenzi wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Bw Achiles Bufure (watatu kushoto), Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano
…………………………………………………………………….
Na Sixmund J. Begashe
UBALOZI wa Finland nchini Tanzania umechangia picha 23 na vitabu viwili kwa Makumbusho ya Taifa la Tanzania ili viweze kuhifadhiwa kwenye taasisi yenye dhamana ya Uhifadhi, Utafiti, Ukusanyaji, na Utoaji elimu kupitia matokeo ya tafiti na Mikusanyo mbali mbali.
Balozi wa Finland nchini Tanzania, Mhe Riitta Swan, alikabidhi picha na vitabu hivyo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt Noel Lwoga jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Mhe Balozi Swan ameeleza kuwa nchi yake imekuwa ikijihusisha sana na uhifadhi wa mazingira kwa faida ya viumbe hivyo, wamesukumwa kuchangia picha hizo ili zitumike kuelemishia jamii juu ya umuhimu wa mazingira salama kwa watu, mimea na viumbe vingine.
Picha hizi zilipigwa na Prof. Olli Marttla, ambaye ameishi miaka mingi nchini na kusafiri sehemu mbali mbali za Tanzania akipiga picha na kuandika vitabu vya mazingira, alisema Mhe. Balozi na kuongeza kuwa kupitia picha hizo zitkazohifadhiwa kitaalamu Makumbusho ya Taifa, watu wengi watapata elimu ya Mazingira na umuhimu wake ili dunia yote iwe salama kwa kila mtu na viumbe wengine.
“Ni Imani yetu kwamba picha hizi zitawafikia watu wengi zaidi hapa Makumbusho ya Taifa kuliko kuzihifadhi Ubalozi” amesema Mhe. Swan.
Akipokea picha hizo na vitabu, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa nchini, Dkt. Noel Lwoga aliushukuru Ubalozi wa Finland kwa mchango huo mkubwa na muhimu na kusema kuwa Taasisi yake inatarajia kuwa na Makumbusho nyingine ya Elimu Viumbe, hivyo, picha hizo zitatumika huko na hata kuboresha maonesho ya Baolijia yaliyopo sasa.
“Ukiachana na ile tuliyonayo pale Jijini Arusha, pia tuanatarajia kuwa na Makumbusho nyingine ya Elimu Viumbe, hivyo kwa picha hizi nzuri tulizo zipata leo zitasaidia kwenye Makumbusho hiyo.” Alisema Dkt. Lwoga
Dkt Lwoga aliongeza ametoa wito kwa wadau mbali mbali kuendelea kuchangia mikusanyo ya kimakubusho na kwa jamii kutembelea Makumbusho ya Taifa ili kupata elimu ya mazingira na nyinginezo kwani watapanua wigo wa uwelewa juu ya nchi ya Tanzania na dunia kwa ujumla.
Bw. Pius Gondeka, ambaye ni mdau wa Makumbusho ya Taifa, amepongeza kitendo cha Ubalozi wa Finland kuipatia Makumbusho ya Taifa picha ambazo yeye kama mwananchi na wananchi wengine watapata fusra ya kujionea uzuri wa Tanzania kupitia picha hizo lakini pia zitawawezesha kuwakumbusha umuhimu wa uhifadhi wa Mazingira.
Mkuu wa Idara ya Mikusanyo Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni, Dar es Salaam Bi Flower Manase amesema Idara yake imejipanga vyema kuhakikisha picha hizo zinahifadhiwa kwa umakini mkubwa na utaalam wa hali ya juu ili ziweze kuishi miaka mingi na kuwafaidisha watanzania waliopo sasa na vizazi vijavyo.