kijana Viviana Komba ambaye amefanikiwa kuanzisha kampuni ya kutengeneza nepi za watoto kwa kutumia pamba laini
vijana waliopata mafunzo na mitaji kutoka Taasisi ya STOF wakipata maelekezo ya kuboresha biashara zao kutoka kwa Mkrugenzi wa STOF Teresa Nyirenda Msamala mjini Songea
NA STEPHANO MANGO,SONGEA
TAASISI ya Saint Teresa Orphans Foundation(STOF) inayofanyakazi
mkoani Ruvuma nchini Tanzania na nchini Marekani kupitia mfumo wa
TEDNA imeweza kuwapatia vijana mafunzo ya ujasiriamali na kufanikiwa
kufungua kampuni zao.
Mkurugenzi wa STOF Teresa Nyirenda anasema Taasisi yake imeamua
kuanzisha mfumo wa TEDNA baada ya kubaini kuna kundi kubwa la vijana
wamemaliza vyuo vya kati na vyuo vikuu wamekosa ajira.
Nyirenda anasema kupitia TEDNA vijana waliomaliza vyuo vikuu
wameunganishwa na kupewa mafunzo na mitaji ili waweze kujiajiri na
kuajiri vijana wengine waliokosa ajira.
Vijana kadhaa mkoani Ruvuma kupitia Taasisi ya STOF wamepata
mafunzo na mitaji hivyo kufanikiwa kufungua kampuni zao chini ya
usimamizi wa TEDNA.
Galus Mpepo ni kijana wa Songea ambaye amelelewa na STOF tangu
akiwa na umri wa miaka nane ambapo hivi sasa ni mhitimu wa chuo kikuu
ambaye alipata changamoto ya ajira.
Mpepo anasema kutokana na changamoto hiyo STOF iliamua kuwapatia
mafunzo na kuwawesha kuanza biashara na kumiliki kampuni yenye
uwezo wa kuzalisha nyama za kusindika na kusindika bidhaa mbalimbali
kama unga na maharage.
Hata hivyo anasema amejikita zaidi katika kilimo ambacho kitamwezesha
kupata malighafi za mashambani kama mahindi,soya,alizeti ambazo
anazitumia katika ufungaji wa kuku na nguruwe.
“Hivi sasa natumia muda wangu zaidi katika kuimarisha kampuni yangu
ambapo nimeanzia kufanya shughuli za uzalishaji katika eneo la Mlilayoyo
wilayani Namtumbo,katika eneo langu kuna sehemu nimelima mashamba
na eneo linguine nimefuga mifugo kuku na nguruwe’’,anasema Mpepo.
Kwa upande wake Romana Haule mnufaika wa TEDNA anasema
amefanikiwa kuanzisha kampuni ya chakula ambapo hivi sasa
anawafanyakazi watatu.
Anaishukuru Taasisi ya STOF kwa kumwezesha mafunzo na mtaji hivyo
kufanikiwa kuanzisha biashara hiyo kupitia mfumo wa ujasiriamali wa
TEDNA ambapo hivi sasa ameweza kuwatunza watoto wake na kuwalipa
mshahara wafanyakazi wake.
Naye Zesco Ngonyani ni mmoja wa vijana waliofanikiwa kuanzisha
kampuni ya ujenzi kupitia mfumo wa TEDNA ambapo anasema STOF
imemsaidia kumpeleka shule hadi kumaliza kupata mafunzo ya ufundi
ujenzi ambapo awali alikuwa anafanyakazi mitaani bila usimamizi
madhubuti.
“STOF waliniangalia na kuona mafanikio yangu yanachelewa
ndipo,wakanisaidia kuanzisha kampuni ya ujenzi nikiwa na vijana
wenzangu,kwa hiyo hivi sasa Napata tenda za kujenga majengo kuanzia
msingi hadi kuezeka na umaliziaji wote ikiwemo kupaka rangi’’,anasema
Ngonyani
Anasema Kampuni yake ina mafundi bora,wenye uwezo wa hali ya juu na
kwamba wanafanya kazi kwa uaminifu mkubwa hali ambayo imesababisha
kampuni yao kuaminika na kupata kazi nyingi.
Anasema kampuni yake ina uwezo wa kufanya kazi zote zinazohusika na
ujenzi kuanzia kujenga,kuezeka,kupaka rangi,kuchomelea,kuweka
umeme,kutengeneza samani na kwamba mteja akikabidhi ramani ya
nyumba wao wanamaliza kila kitu na kumkabidhi nyumba iliyokamilika kwa
asilimia 100.
Anatoa shukurani kwa STOF kwa kumpeleka shule,kupata mafunzo na
kupewa mtaji hali ambayo inamwezesha kuanzisha kampuni ya ujenzi hali
ambayo imwezesha kuajiri vijana wengine.
Viviana Komba ni miongoni mwa vijana ambao wamesaidiwa na STOF
tangu akiwa na umri wa miaka nane ambapo amesomeshwa hadi elimu ya
chuo kikuu katika fani ya ualimu.
Viviana anasema baada ya kumaliza chuo kikuu alikosa ajira hivyo
Mkurugenzi wa STOF Teresa Nyirenda alivyoona vijana wengi wanamaliza
vyuo na kukosa ajira alianzisha TEDNA ili kuwakuza kifikra na kimtazamo
vijana na kuwapatia mitaji ili waweze kufanya biashara na kufungua
kampuni zao.
Anasema walipewa mafunzo mbalimbali kabla ya kupewa mitaji ambapo
yeye alipata wazo la kuanzisha kampuni ya kutengeneza nepi za watoto
kwa kutumia pamba laini ambazo hazina madhara kwa watoto
ukilinganisha na nepi za dukani.
Kupitia kampuni yake,Viviana anasema anatengeneza sabuni za maji,dawa
za kusafishia masinki,anatengeneza mablankenti ya watoto,mapambo ya
shingoni na mkononi,pochi za shanga na vikoi vya kimasai.
“Nina mashine za kisasa zinazoniwezesha kutengeneza bidhaa hizo,lengo
langu ni kumiliki kampuni kubwa itakayoajiri watu na kuwasaidia vijana
wengine ambao wapo mitaani hawana ajira’’,anasisitiza.
Hata hivyo anasema bidhaa ambazo amezitengeneza baadhi ameshaanza
kuuza na kwamba bado bidhaa nyingine zipo kwenye mchakato wa
kutengeneza jina la kibiashara ili hatimaye kuziingiza sokoni.