………………………………………………………………………………
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
SERIKALI Mkoani Pwani ,imeziagiza halmashauri zote mkoani Pwani ,kuwachukulia hatua ikiwemo kutumia vyombo vya dola ili vifanye kazi yake kwa watumishi wanaobainika kuwa na tuhuma mbalimbali .
Aidha imeiagiza ,halmashauri ya Mji wa Kibaha na halmashauri ya wilaya ya Kibaha ,kuhakikisha zinafunga hoja zote ambazo hazijafungwa katika ukaguzi wa hesabu za Serikali ,kwa mwaka 2019/2020 ,ifikapo September 30 mwaka huu.
Akitoa maagizo hayo mkuu wa mkoa wa Pwani ,Aboubakar Kunenge ,wakati wa baraza la madiwani kupitia na kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa hesabu za Serikali (CAG )mwaka 2019/2020, alisema ,ni wakati wa kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi ambao watabainika kujinufaisha kwa mapato ama kusababisha hasara kwa halmashauri.
Aliongeza ,adhabu itakayotolewa ilingane na ukubwa wa tuhuma husika aliyosababisha mtumishi lengwa ili kusaidia kulinda maadili na uwajibikaji.
Pamoja na hilo ,Kunenge alitaka hoja ambazo hazijafungwa zifungwe na kama watakwama watoe taarifa.
Alibainisha pia hoja zinazohusisha taasisi nyingine zishughulikiwe na kuhakikisha hazijirudii katika mwaka mwingine .
Pamoja na hayo,aliwaasa kuacha kuridhika na vyanzo walivyovizoea ,badala yake wabuni vyanzo vipya vya mapato ,pamoja na miradi ya kimkakati itakayowawezesha kuinua mapato yao ya ndani .
“Epukeni kuzalisha hoja ,ongezeni wigo wa ukusanyaji mapato na halmashauri ibueni vyanzo vipya vya mapato ili kuinua mapato .” alisema Kunenge.
Nae mkaguzi mkuu wa hesabu ,Mkoani Pwani Mary Dibogo ,alisema wao wapo kwa ajili ya kufanya ukaguzi kwa maslahi ya jamii na serikali hivyo CAG haiwezi kuonea halmashauri yoyote .
Alitaka fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi zifanyiwe kazi husika na ijengwe kwa thamani inayolingana na fedha iliyotolewa bila miradi hiyo kukaa kwa muda mrefu pasipo kukamilishwa.
Alizitaka halmashauri hizo,kusimamia ukusanyaji wa mapato ,na kuhakikisha yanafika sehemu sahihi .
Kwa upande wake ,Katibu tawala Mkoani Pwani ,Mwanasha Tumbo alitoa rai kwa watumishi na watendaji kuacha kufanya kazi kwa mazoea .
Mwanasha aliwaasa kufuata sheria ,kanuni na muongozo katika masuala ya ukaguzi ili kuondokana na dosari ndogondogo.
Akiwa kibaha mji ,mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Kibaha ,Jeniffer Omolo yeye alisema ,kati ya hoja 38 kufikia juni 2 mwaka huu 22 zilifungwa ambapo hoja 16 hazijafungwa.