Muonekano wa Mahakama inayotembea ‘mobile court’ ikiwa inatoa huduma katika eneo la Mkolani jijini Mwanza. Mahakama hiyo hutoa huduma Buswelu, Igoma na Mkolani (Buhongwa) mkoani humo.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wa mkoani Mwanza wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa Mahakama eneo la Mkolani ambapo Mahakama hiyo ilikuwa ikitoa huduma Juni 17, 2021. Lengo la ziara ya Wanahabari wa mkoa huo ni kuwapa uelewa zaidi juu ya huduma zitolewazo na Mahakama hiyo pamoja na mafanikio yake ili waweze kuwajuza wananchi juu ya Mahakama hiyo.
**************************
Na Mary Gwera, Mahakama-Mwanza
Jumla ya mashauri 1,208 yamesikilizwa na kumalizwa na Mahakama inayotembea ‘mobile court’ huku watu 13,668 wakiwa wamenufaika na huduma zinazotolewa na Mahakama hiyo katika mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza.
Akizungumza na Waandishi wa Habari wa mkoani Mwanza Juni 17, 2021, Hakimu Mkazi ambaye pia ni Mratibu wa Mahakama zinazotembea ‘mobile court’, Mhe. Moses Ndelwa alisema kuwa idadi hiyo ya mashauri na wanufaika wa huduma hizo ni tangu kuanza kutolewa rasmi kwa huduma hiyo Julai, 2019 hadi kufikia mwezi Mei, 2021.
“Mahakama hii imeleta mafanikio katika mikoa hii miwili ambapo imesikiliza na kumaliza jumla ya mashauri 1,208, huku Mwanza pekee mashauri 520 yalifunguliwa na kumalizika katika kipindi hicho,” alisema Mhe. Ndelwa.
Mratibu huyo aliongeza kuwa usikilizwaji wa Mashauri katika Mahakama inayotembea ni wa haraka huku akieleza kuwa mashauri yote husikilizwa na kumalizika ndani ya siku 30.
Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza, Mhe. Monica Ndyekobora ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuendelea kuitumia Mahakama hiyo kwa kuwa muitikio wa kufungua mashauri bado si mkubwa sana.
“Mahakama inayotembea imesaidia kupunguza mlundikano wa mashauri, hivyo ni rai yangu kwa wanawanchi wa mkoa huu kujitokeza kutumia Mahakama hii endapo wana kesi za kufungua kwa kuwa inawapunguzia gharama wananchi, inatoa haki kwa wakati na kadhalika” alisema Mhe. Ndyekobora.
Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo-Mkuyuni ambaye pia anahudumu katika Mahakama inayotembea, Mhe. Jenipher Nkwabi alibainisha kuwa mashauri yanayofunguliwa kwa wingi katika Mahakama hiyo ni mashauri ya ndoa na talaka, huku akiongeza kuwa kwa upande wa Mwanza hususani eneo la Mkolani/Buhongwa kumekuwa na muitikio mkubwa wa wananchi kutumia Mahakama hiyo.
Mahakama ya Tanzania iliandaa ziara maalum ambayo iliwahusisha Waandishi wa Habari wa mkoani Mwanza lengo likiwa ni kuwapa uelewa zaidi juu ya huduma zitolewazo na Mahakama hiyo pamoja na mafanikio yake ili waweze kuwajuza wananchi juu ya Mahakama hiyo.
Kwa upande wa Mwanza huduma hutolewa maeneo ya Buswelu siku ya Jumatatu, Igoma-Jumanne na Jumatano na Buhongwa huduma hutolewa Alhamis na Ijumaa.
Aidha, kwa upande wa Dar es Salaam ambapo pia huduma hii inapatikana, Mahakama inayotembea hutoa huduma zake maeneo ya Bunja ‘A’ Jumatatu ya kila wiki, Kibamba siku ya Jumanne, Buza-Jumatano na Chanika-Alhamis.
Mbali na usikilizaji wa mashauri, Mahakama inayotembea inatoa pia huduma nyingine kama kufanya usuluhishi kwa wadaawa, kutoa elimu kuhusiana na masuala ya kimahakama, kutoa fomu za viapo na kuthibitisha nyaraka mbalimbali pamoja na kupokea malalamiko.
Mahakama inayotembea ilizinduliwa rasmi Februari 06, 2019 katika sherehe za kilele cha maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini na aliyekuwa Rais wa awamu ya tano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Mpango wa Mahakama ni kuendelea kusogeza huduma hii katika maeneo mengine kadri bajeti itakavyoruhusu.