***************************
JUMUIYA ya Waislamu ya HIZB UT TAHRIR, imeeleza hatua ya serikali kupitia muhimili wake wa Mahakama kufuta kesi dhidi ya Masheikh wa UAMSHO inatia moyo katika utendaji haki kwa wananchi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Msemaji wa Jumuiya hiyo, Masoud Msellem, alisema hatua hiyo iwe mwanzo wa safari ya wakati wote katika kutenda haki.
Alisema hatua hiyo inatia moyo na kuonyesha dhamira njema ya serikali, kwamba kuna haja ya kufanywa maboresho ya sheria kadhaa za nchi ili kuepuka ukiukwaji wa haki za baadhi ya wananchi.
Msemaji huyo, Alieleza kuwa ni vyema kwa mamlaka husika kuwa kuangalia upya suala la upelelezi katika kesi za ugaidi ili kuepusha wananchi kukaa muda mrefu rumande bila makosa.
Alisisitiza kuwa matumizi mabaya ya sheria ya ugaidi inaharibu mahusiano mema baina ya Watanzania, hivyo kuna haja ya kufanywa mabadiliko.
Kuhusu Masheikh walioachiwa, alisema jumuiya hiyo kwa kushirikiana na nyingine zinafanya kila namna kuwachangia ili wawe na uwezo wa kujikimu.
Tamko hilo la HIZB UT TAHRIR, linakuja ikiwa ni siku nne tangu Masheikh wa UAMSHO kuachiwa huru baada ya kufutiwa kesi za ugaidi zilizowaweka rumande kwa takribani miaka saba