Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Balozi Brigadia Jenerali Wilbert Ibuge akiongea jana na watumishi na madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga kwenye kikao maalum cha baraza la madiwani la kujadili taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Mbinga wakiongozwa Kaimu mkuu wa Polisi wilaya hiyo Samwel Mwamba katikati wakimsikiliza Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ambaye ni Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Balozi Brigadia Jenerali Wilebert Ibuge(hayupo pichani)katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani cha Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma cha kujadili mapendekezo na hoja za mkaguzi Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ambapo Halmashauri hiyo imepata Hati safi.
Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga wakimsikiliza Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Balozi Wilbert Ibuge(hayupo pichani)wakati wa kikao maalum cha kupitia na kujadili mapendekezo ya hoja za mkaguzi na dhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) kwa mwaka wa fedha ulioishia mwezi Juni 2020 ambapo Halmashauri hiyo imepata hati safi.
Picha zote na Muhidin Amri
…………………………………………………………………
Na Muhidin Amri,Mbinga
HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,imefanikiwa kukusanya shilingi bilioni 3,336,270,400.1 sawa na asilimia 98.33 kati ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 3,383,162,400.00 kama mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha ulioisha mwezi Juni 2020.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Desdelius Haule amesema hayo jana, katika kikao maalum cha Baraza la madiwani cha kujadili hoja na mapendekezo ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG)kwa mwaka wa fedha 2019/2020 kilichofanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari Kigonsera.
Amesema, Halmashauri ya Mbinga kwa miaka mitatu mfululizo imeendelea kupata hati safi kutoka kwa CAG, na mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mkubwa kati ya madiwani na watendaji ambao wanafanya kazi kwa pamoja katika kutekeleza majukumu yao.
Kwa mujibu wa Haule, hali ya kujituma,kufanya kazi kwa weledi na uadilifu hasa katika suala zima la kukusanya,kusimamia na nidhamu ya fedha ndiyo silaha kubwa inayoifanya Halmashauri ya Mbinga kufanikiwa kutekeleza mipango mbalimbali yenye lengo la kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi.
Aidha amesema,wataendelea kutekeleza maelekezo mbalimbali yanayotolewa na CAG ya kutokuwa na hoja na kuzifanyia kazi hoja zote za ukaguzi na namna ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Haule ameongeza kuwa, sasa wataelekeza nguvu kubwa kwenye kuibua vyanzo vipya na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato ya ndani, kudhibiti matumizi mabaya ya fedha na kuwachukulia hatua za kinidhamu watendaji watakaokwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma kwa kuchezea(kuiba) fedha zinazokusanywa.
Ameishukuru ofisi ya Mkuu wa mkoa, kwa ushirikiano na ushauri wa namna bora ya kuijenga Halmashauri hiyo na kuhaidi kufanyia kazi ushauri na mapendekezo mbalimbali kama hatua ya kuboresha utendaji kazi kwa watumishi ili waendelee kupata hati safi mwaka hadi mwaka.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Balozi Wilbert Ibuge, amewataka watumishi wa Halmashauri hiyo kushirikiana, kupendana na kutiana moyo wakati wote wa kutekeleza majukumu yao jambo litakalosaidia kuchochea uwajibikaji na ufanisi kazini.
Aidha,ameipongeza Halmashauri hiyo kwa mafanikio mbalimbali ikiwemo kupata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo na mchango wake kwenye mfuko wa maendeleo ambapo kwa mwaka wa fedha 2019/2020 imeweza kuchangia shilingi milioni 250,341.41 sawa na asilimia 98.
Amesema, fedha hizo zimekwenda kwenye makundi maalum ya walemavu waliopata shilingi milioni 38,737.685,vijana shilingi milioni 103,127.986 na wanawake waliopata shilingi milioni 108,475.370.
Amesema, kutokana na mafaniko hayo watumishi wa Halmashauri wanayo haki ya kutembea kifua mbele,hata hivyo ameshauri kuweka malengo makubwa zaidi ya makadirio ya mapato kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kutokana na kuwa na vyanzo vingi ambavyo bado havijafanyiwa kazi kama sekta ya afya kupitia Bima ya afya iliyoboreshwa(CHF).
Balozi Ibuge, amewaagiza viongozi wa Halmashauri na wilaya ya Mbinga kwa jumla kuhakikisha wanaboresha huduma za matibabu kwenye zahanati,vituo vya afya na Hospitali za serikali ili wananchi waweze kwenda kupata matibabu na hivyo kuchangia fedha badala ya kukimbilia kwenye vituo vya watu binafsi.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa mkoa ameagiza mazao yote yaliyopo kwenye mwongozo wa mfumo wa stakabadhi ghalani lazima yapelekwe kwenye vyama vya msingi vya ushirika(AMCOS)kwa ajili kuuza na sio vinginevyo.
Amesema, mfumo huo ni mzuri na lengo la serikali kutoa mwongozo wa matumizi ya stakabadhi ghalani ni kutaka kuona mkulima ananufaika kwa kupata soko la uhakika na bei nzuri ya mazao yake inayolingana na gharama za uzalishaji shambani.
Amewataka madiwani na watendaji wa Halmashauri, kushirikiana kwa kuhakikisha wanasimamia sekta ya ushirika na kujiepusha kukwamisha mfumo huo ambao umeanza kuonesha manufaa makubwa kwa serikali na wananchi hususani wakulima.
“tukasimamie mfumo wa stakabadhi ghalani ili kuwalinda wakulima wetu wanaoangaika mchana na usiku katika uzalishaji,mfumo huu umeonesha mafanikio makubwa na serikali tunapata mapato ambayo yamesaidia kuboresha huduma kwa wananchi”amesema.