Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
TAASISI
ya Wajibu imesema kwamba imepitia na kuchambua Bajeti ya Serikali ya
mwaka 2021/2022 ambapo kwa sehemu kubwa wameipongeza kwa kuja na vyanzo
vipya vya ukusanyaji mapato ikilinganishwa na bajeti za miaka iliyopita.
Akizungumza
leo Juni 16,2021, kuhusu uchambuzi wa bajeti ya Serikali, Mkurugenzi
Mtendaji wa Wajibu Ludovick Utouh amesema taasisi hiyo aliianzisha mwaka
2015 ikiwa na malengo ya kujenga uwezo wa wananchi kufahamu mambo
yanayowahusu uwajibikaji wa rasilimali za Taifa.
“Sisi
wajibu tunajikita zaidi kwenye uwajibikaji kwenye rasilimali za
taifa,niseme ni mara ya kwanza leo WAJIBU imeingia kwenye kuchambua
bajeti ya Taifa kwa jicho la uwajibikaji.Tunafahamu Juni 10 mwaka huu
Waziri wa Fedha na Mipango Dk.Mwigulu Nchemba aliwasilisha bajeti ya
Serikali bungeni.
“Ni
bajeti ya mwaka 2021/2022 ni bajeti ya kwanza chini ya mpango wa tatu
wa maendeleo ya taifa wa miaka mitano na ni bajeti ya kwanza pia kwa
awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan na bajeti hii na mpango huu
inachukua dhima inayosema kujenga uchumi shindani na viwanda kwa
maendeleo ya watu,”amesema Utouh.
Amefafanua
taasisi ya Wajibu imefanya uchambuzi wa bajeti pendekezwa kwa
kuzingatia uwazi, uwajibikaji na utawala bora, hivyo imekuja na maoni,
changamoto na mapendekezo yanayolenga kuboresha ukamilishaji wa bajeti
ya taifa ya mwaka 2021/2022.
“Kama
tulivyoona na tulivyosoma , makadirio ya bajeti ya Serikali ya mapato
na matumizi yameweka malengo ya jumla kwa kuanza na lengo la kwanza la
kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara kwa
kuweka mazingira rafiki kwa mlipa kodi.
“Kwa
lengo la kuvutia uwekezaji, ukuaji wa biashara ndogondogo na zakati
ili kapunia wigo wa kodi.Pili kuboresha mifumo ya usimamizi na
ukusanyaji wa kodi ili kupanua wigo wa kodi.Kwa kweli bajeti hii imekuja
na vyanzo vipya vya mapato ya Serikali ambavyo huko nyuma havijakuwepo.
“Zamani
mabajeti mengi ya Serikali yakuliwa ni marudio ya yaliyofanyika huko
nyuma, lakini safari hii tunaona Serikali imekuja na taratibu za
kukusanya mapato kwa kutumia ufumo wa ununuzi wa umeme LUKU, mfumo ambao
hakuwepo nyuma.
“Wamekuja
kwenye kodi ya laini za simu ambayo ni kitu kipya na vile vile Waziri
ametuambia Serikali inaingia kwenye hati fungani za manispaa kama njia
ya mapato ya Serikali, tunapaswa kuipongeza Serikali kwa ubunifu
huo,”amesema.
Ameongeza
pia bajeti inalenga kuimarisha uendeshaji wa mashirika ya umma ili
kuendelea kufanya kazi kibiashara, kuongeza uzalishaji wa mazao
yatokanayo na sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.Pia kuboresha kilimo cha
umwagiliaji, kuogeza mnyororo wa thamani na masoko ya mazao ya kilimo,
kuchochea uvumbuzi na uhuhishaji wa teknolojia kutoka nje.
“Kuchochea
uwekezaji kwenye viwanda hasa zinazotumia malighafi zinazotoka hapa
nchini, kudhibiti utoroshaji madini na kujenga mitambo ya uchenjuaji
madini nchini pamoja na viwanda vya kuongeza thamani kwenye madini
yanayozalishwa nchini.
“Ikiwemo
jitihada za maksudi za kuwajengea uwezo zaidi wachimbaji wadogo katika
ushiriki wao sekta hii, uboreshaji wa miundombinu ya sekta ya
usafirishaji wa nishati , kuboresha utoaji huduma za kijamii hasa katika
sekta ya afya,elimu na maji.
“Na
kuimarisha ushirikiano wa nchi yetu na nchi jirani,kanda na kimataifa.
Haya ndio malengo makuu ya bajeti inayozungumziwa sasa hivi
bungeni.Hivyo uchambuzi wa bajeti hii tuliofanya tumeona kuna masuala
matano ambayo bajeti imeyataja, ukweli ukienda kwenye ripoti za CAG za
miaka ya nyuma zilikuwa ni mapendekezo.
“Kwa
ajili ya utekelezaji wa Serikali, nitaeleza mabadiliko ya sheria ya
ukaguzi wa umma sura ya 418, kama mtakumbuka mwaka 2013 Serikali ilileta
mabadiliko ya sheria ya ukaguzi ya mwaka 2008 ambapo sheria ilitaka CAG
anawapasilisha ripoti zake bungeni kama alivyowasilisha Aprili mwaka
huu, serikali nayo inatakiwa kwenda sambamba siku hiyo hiyo iwasilishe
majibu,”amesema.
Ameongeza
hiyo kitu ilipingwa sana lakini ilipita, hivyo kwa wao watalaamu wa
ukaguzi walijua haitekelezeki.Bahati nzuri Serikali imetambua hilo na
imekuja na mapendekezo ya kubadilisha yale marekebisho yaliyofanyika
mwaka 2013 .
“Pili
kuna mabadiliko ya sheria ya mikopo , dhamana na misaada sura ya 134,
nayo hii mabadiliko haya yatairusu Serikali kuidhamini kampuni au
taasisi yoyote ya umma kukopa kiasi kisichozidi hisa za serikali au
taasis husika.
“Ambapo
hii inaenda kujibu pendekezo la CAG ambapo amekuwa anahoji mara nyingi
kuhusu upungufu wa mitaji kwa mashirika yanayosimamiwa na Serikali .Tatu
kuna kumekuwa na kelele kuhusu mikopo ya Serikali kwenye mifuko ya
hifadhi ya jamii.
“Ukweli
Serikali inakopa hailipi na wakati mwingine hailipi riba , kwa hiyo
mara nyingi inapochukua miaka mingi kwa kulipa madeni yale inaathiri
utendaji kazi wa mifuko hiyo.Kwa hiyo bajeti hii inatuambia Serikali
italipa madeni inayodaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kutenga
fedha kwenye bajeti na kutumia hatifungani zitakazoiva kwa nyakati
tofauti kuanzia miaka miwili hadi miaka 25.
“Hii
itasaidia kuyajumuisha madeni ya mifuko ya hifadhi ya jamii kwenye deni
la taifa, mara nyingi madeni hayo yalikuwa hayaingizwi kwenye deni la
taita.Utaratibu huo sasa madeni hayo yatakuwa yanaingizwa kwenye deni la
taifa, itasaidia mifuko hii kuwa na fedha za kuwekeza na kujiendesha
kwa ufanisi zaidi,”amesema.
Aidha
amesema jambo la nne katika baheri hiyo ni Serikali kuongeza mapambano
zaidi dhidi ya rushwa, udanganyifu na ubadhirifu wa mali za umma.”Kama
mnavyojua ile lugha ya ufisadi huko nyuma , pesa kupigwa huko na huko
kitu ambacho CAG amekuwa akikizungumza kila wakati.
“Serikali
kusema kweli imedhamiria kukaza uzi , na kuweka mazingira magumu zaidi
ya upotevu au matumizi mabaya ya fedha na serikali za taifa. Kuna mfano
wa mwenendo wa fedha na makusanyo ya serikali yenye viashiria vya rushwa
kwa miaka mitatu iliyopita.
“Na
tano ni mapato ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania(TCRA) na Wakala wa Meli Tanzania(TASAC) kuanzia
mwaka 2021/2022 yatakusanywa na mfumo huo kupitia GPE na kuingizwa
kwenye akaunti ya makusanyo zilizopo Benki Kuu.
“Nafikiri
hizi zimetokana na maoni ya CAG kwenye ripoti yake ya mwaka 2019 ambapo
kuliokana kuna upotevu Sh.bilioni 3.9 kutokana na udanganyifu katika
Bandari ya Kigoma na Mwanza ambao ulitokana na udhaifu wa mifumo ya
ndani katika usimamizi wa malipo, hivi kwa upande wa CAG ni furaha,
tunaona utekelezaji wa mapendekezo yake.
Kwa
upande wake Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe tawi la Dar es Salaam Profesa
Honest Ngowi amesema bajeti ya mwaka huu kuna aina mpya za ukusanyaji
kodi ambazo zinaweza kuwa na mjadala kwa mfano kutoza kupitia umeme ina
mjadala wake lakini ni aina tofauti ya kutoza hiyo kodi ukilinganisha na
ilivyozoeleka.
“Njia
ya kwanza ni kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara , hapo ndipo
tunapozungumzia wigo wa kupanua kodi, na hii muhimu kwasababu kodi zote
hizi zinatokana na uzalishaji wa bidhaa na huduma usipopanua wigo na
uwekezaji zaidi utazikosa.
“Lakini
kuboresha mazingira yatakayochochea ulipaji kodi wa hiyari, hiyo muhimu
sana.Ulipaji kodi wa kushurutishana ni gharama sana na unaweza
kuangukia fedha nyingi kupotea lakini utumiaji wa TEHAMA unarahisisha
ukusanyaji wa kodi.
“Siku
hizi kuna mfumo wa kulipia kodi zako kiganjani, msingi wake kuna watu
wanataka kulipa kodi lakini kwenda kupanga foleni kwenye mabenki
inapoteza muda lakini kufanya kiganjani ndio kinazungumziwa
hapa,”amesema Prof.Ngowi.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya WAJIBU , Ludovick Utouh akizungumza mbele ya
Waandishi wa Habari leo mkoani Dar es Salaam kuhusu uchambuzi wa bajeti ya Serikali,ambapo Taasisi ya
WAJIBU imesema kuwa imepitia na kuchambua Bajeti ya Serikali ya mwaka
2021/2022 na kwamba sehemu kubwa wameipongeza kwa kuja na vyanzo vipya
vya ukusanyaji mapato ikilinganishwa na bajeti za miaka
iliyopita,Pichani kulia ni Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe tawi la Dar es Salaam Profesa Honest Ngowi .
Mkuu
wa Chuo Kikuu Mzumbe tawi la Dar es Salaam Profesa Honest Ngowi
akifafanua jambo mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo
mkoani Dar es Salaam,wakati akifafanua kuhusu Bajeti ya Mwaka huu na
uwepo wa aina mpya za ukusanyaji kodi tofauti na ilivyozoeleka hapo awali