…………………………………………………………………………………
Na Gift Thadey, Simanjiro
SHULE ya sekondari ya Mgutwa iliyopo Kata ya Shambarai nje kidogo ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, inatarajia kugawa na kupanda miche 12,500 ya miti kwenye shule 25 zilizopo Tarafa ya Moipo ifikapo Mwaka 2025.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa shule ya Sekondari Mgutwa Shedrack Mlemeka amesema katika kipindi cha mwaka 2016/2017 hadi sasa wamegawa miche ya miti 6,390 kwenye shule 20, ambapo shule 19 zipo Tarafa ya Moipo na shule moja Kata ya Orkesumet Tarafa ya Naberera.
Mlemeka ameyasema baada ya mwenge maalum wa uhuru kutembelea na kuzindua mradi wa hifadhi ya mazingira ya shule ya Sekondari Mgutwa.
Amesema shule hiyo ni binafsi iliyopo Kata ya Shambarai, Tarafa ya Moipo na ina walimu 10 na wanafunzi 121, wakiwemo wavulana 61 na wasichana 60
“Tunatarajia eneo hili kuwa la mfano kwa utunzaji wa mazingira kwa jamii zinazotuzunguka na Wilaya kwa ujumla,” amesema Mlemeka.
Amesema kwenye shule hiyo ya Mgutwa wamepanda miti 2,000 ambayo imependezesha na kutunza mazingira ya shule hiyo.
Mwalimu wa mazingira wa shule ya Sekondari Mgutwa, Exaud Mafie amesema mradi wa mazingira
uliozinduliwa na mwenge umegharimu sh16.7 milioni.
Mafie amesema katika mradi huo, shule ya Mgutwa imechangia sh8.8 milioni, Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro sh1.6 milioni, Malihai club sh125,000 na Maivaro Ever Green sh6 milioni.
“Jumuiya ya shule ya sekondari Mgutwa imefurahi kutembelewa na mwenge wa uhuru mwaka 2021 na inawatakia safari njema mnapoendelea na shughuli za kukimbiza mwenge,” amesema Mafie.
Amesema mradi huo unategemea kurejesha uoto wa eneo la shule, upatikanaji wa kivuli na kuboresha mandhari ya shule kwa ujumla na kupunguza kiwango cha hewa ya ukaa kilichopo angani na kukabiliana na athari mabadiliko ya tabia nchi.
Kiongozi wa mbio za mwenge maalum wa uhuru mwaka huu, Luteni Josephine Paul Mwambashi akizungumza baada ya kupanda mti kwenye shule ya Sekondari Mgutwa ameupongeza uongozi wa shule kwa kutunza mazingira.
Luteni Mwabashi amesema utunzaji huo wa mazingira unapaswa kuigwa na shule nyingine kwani miti husaidia kuweka mazingira mazuri ya shule.
“Nawapongeza uongozi wa shule na wanafunzi kwa kutunza mazingira na sisi tumepanda miti ya kumbukumbu tunatarajia mtaendelea kuitunza kama mlivyofanya,” amesema Luteni Mwambashi.