Baadhi ya paketi za damu kama zilizotolewa na ndugu wa wagonjwa katika kituo hicho cha afya.
******************
Ugonjwa wa malaria umeelezwa kuwasumbua zaidi watoto wadogo wa umri wa kati ya mwaka mmoja hadi mitano katika hamashauri ya Mpimbwe mkoani Katavi.
Dkt. Omari Sukari ni mganga mkuuwa mkoa wa Katavi amesema kwa Halmshauri ya Mpimbwe maambikizi ya ugonjwa malaria yapo kwa asilimia 7.4 kwa mwaka kiwango ambacho kipo juu kuliko maeneo mengine ya mkoa wa Katavi.
Amesema hali hiyo inatokana na halmashauri hiyo kuzungukwa na misitu pia kuwepo kwa madimbwi ya nayosimamisha maji.
Dkt. Sukari amesema malaria inasababisha damu kupungua mwilini na watoto wanaougua mara kwa mara wamekuwa wakipata tatizo la upungufu wa damu.
“Inapotokea mtoto anatakiwa kuongezewa damu huwa tunawaomba ndugu waje kujitolea damu,kiukweli hatuna damu ya kutosha katika benki ya damu na ndio sababu tumekuwa tukiwaomba wananchi kujitolea damu kila wakati” alisema Dkt. Sukari.
Kwa upande wake Mtaalamu wa Lishe mkoa Bi.Asnath Athuman amesema chanzo kingine cha watoto kupungukiwa damu ni lishe ambapo ameeleza kuwa kutokumlisha mtoto vyakula sahihi kunapelekea kuwa na lishe duni tatizo ambalo kwa mkoa wa Katavi asilimia 33 ya watoto wanalishe duni.
Tatizo la upungufu wa damu pia limekuwa likiwapata kina mama wajawazito hali inayopelekea vifo kwa watoto wachanga.
Bi.Elida Machungwa ni Mratibu wa Mama na mtoto mkoa wa Katavi amesema katika maeneo ya pembezoni kumekuwa kukitokea vifo vya watoto wachanga kutokana na kinamama kutopata huduma za kliniki wakati wa ujauzito.
‘Moja wapo ya sababu za vifo vya watoto ni upungufu wa damu na lishe duni ambapo mtoto anapozaliwa anashindwa kulia na kufariki’ alisema
Aidha amesema ili kuepukana na changamoto hiyo mkoa umeweka mkakati wa kuwafikia kinamama hao kwa kliniki za mikoba ili kubaini changamoto walizonazo.