Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati akivishwa Skafu na mwanafunzi wa Shule ya Wasabato ya Manispaa ya Shinyanga Esta Amosi alipowasili viwanja vya shule ya Msingi Chibe kushiriki Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Afrika jana Mkoani Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati akipokea risala iliyosomwa na mtoto kutoka Baraza la Watoto la Mkoa wa Shinyanga ambaye jina lake halikujulikana mara moja wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Afrika jana Mkoani Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati akikabidhi msaada wa sabuni na chakula kwa Mkurugenzi wa Shirika la AGAPE Bw. John Myola wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Afrika jana Mkoani Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati akikagua moja ya banda la baadhi ya Mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyoshiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Afrika jana Mkoani Shinyanga.
…………………………………………………………………………
Na Anthony Ishengoma- Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati amewataka wazazi na walezi pamoja na vyombo vya usalama Mkoani Shinyanga kuchukia vitendo vya ukatili dhidi ya watoto kwa kuwa hakuna mbadala watoto katika ustawi jamii kokote duniani.
Dkt. Sengati amesema hayo jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika kimkoa katika Kata ya Chibe nje kidogo ya Manispaa ya Shinyanga na kuwataka wadau wa masuala ya watoto pamoja na wazazi mkoani Shinyanga kuchukia ukiukwaji wa haki za watoto kwa ustawi wa jamii ya Tanzania.
‘’Nitakuwa mkali sana kwa wale wananchi wasio kuwa na maadili mamema, wasio kuwa na nidhamu, wasiokuwa wazalendo na wanaocheza cheza na haki za watoto ni lazima kuhakikisha watoto wanasoma, wanalindwa na wanakula vizuri ili kulinda haki zao’’. Aliongeza Dkt. Sengati Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Aidha Dkt. Sengati alisema kuwa ni lazima jamii ikubali watoto wanapewa haki ya kujieleza na kushirikishwa katika masuala yote yanayohusu ustawi wao katika Taifa la Tanzania ndio maana Umoja wa Afrika ukatenga siku hii muhimu kuadhimisha Siku ya mtoto wa Afrika na lazima na Tanzania sio kisiwa hivyo kuna ulazima kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Bi. Yasinta Mboneko amesema amekuwa mstari wa mbele kutembelea shule mbalimbali katika Wilaya yake ili kuhakikisha watoto wanalipiwa ada lakini pia kujionea kama watoto kweli wanaenda Shule ili kuweza kutimiza ndoto zao.
Aidha Bi. Mboneko alionesha kutambua mchango wa Taasisi za dini kwa mchango wao wa malezi na elimu kwa watoto na kuonya wale wote watakao shiriki katika kuminya haki za watoto kupata elimu atahakikisha wanashughulikiwa uku akiwaomba walezi hususani akina mama kuendelea kuwasimamia watoto ili wasije wakaangukia katika mikono isiyo salama.
Wakati huo Mkurugenzi wa Shirika la African Youth Festival Shinyanga Bi.Justa Denis amesema Sheria ya Ndoa na Sheria ya Mtoto ni vitu viwili vinavyokinzana kwani zinatoa fursa kwa wazazi wasioelimika kukatili watoto lakini pia kukatiza ndoto za mtoto wa kike kufikia ndoto zake na kwa maoni yake haoni kama kuondolewa kwa sheria hizo kutaongeza tatizo la mimba na ndoa za utotoni.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Young Women Leadership Shinyanga Bi. Beatrice John ameiomba serikali kufikirai upya suala la watoto wanaopata ujauzito wakiwa shule kurudi tena darasani kwa kuwa baadhi yao wanapata ujauzito kwa kubakwa na kushawishiwa na hivyo kurudi kwao shule kutawasaidia wao kutoa msaada mkubwa katika kuendeleza familia yao.
Aidha Bi. Beatrice John ameongeza kuwa wapo watoto wakiume ambao wanakosa fursa ya kusoma kutokana na kuajiliwa wakiwa wadogo na hivyo kukosa fursa pia ya kufikia ndoto zao na hivyo kuitaka serikali kuzidisha nguvu katika kupambana na ukatili dhidi ya watoto.
Mkoa wa Shinyanga imeungana na mikoa mingine Nchini kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo hudhimishwa kila ifikapo Juni 16 baada ya mauaji ya Kimbali yaliyotokea Soweto Afrika ya kusini na kupelekea watoto wengi kupoteza maisha na kupelekea Umoja wa Afrika kutenga Siku hii muhimu kuwa Siku ya Maadhimisho ya Mtoto wa Afrika.