Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akizungumza katika semina ya Jukwaa la Wahariri wa vyombo vya habari nchini (TEF) iliyoandaliwa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, jijini Dodoma.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (Mb), akizungumza wakati akimkaribisha Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayumo pichani), kuzungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini, jijini Dodoma.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (Mb), na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula, wakimsikiliza Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayupo pichani) wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini, jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), na Mwenyekiti wa Jukwaa la wahariri Deodatus Balile, wakimsikiliza Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (Mb) akizungumza katika semina ya wahariri wa vyombo vya habari nchini iliyoandaliwa na Wizara hiyo jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki wa semina ya wahariri wa vyombo vya habari nchini wakimsikiliza Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alipokuwa akitoa ufafanuzi kuhusu baadhi ya tozo alizowasilisha bungeni ambazo zimeleta mkanganyiko kwa wananchi ikiwemo kodi za miamala ya simu na kodi ya majengo, jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Bw. Deodatus Balile, akitoa neno la shukrani baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), kuzungumza na washiriki wa semina ya wahariri wa vyombo vya habari nchini, jijini Dodoma.
Mmoja wa washiriki wa semina ya wahariri wa vyombo vya habari nchini iliyoandaliwa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Allen Lawa, akiuliza swali baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), kutoa ufafanuzi wa tozo zilizoibua mkanganyiko katika hotuba aliyoiwasilisha bungeni, jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiagana na baadhi ya washiriki wa semina ya wahariri wa vyombo vya habari nchini iliyoandaliwa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari , jijini Dodoma
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM, Dodoma)
………………………………………………………..
Na. Farida Ramadhani na Peter Haule, WFM, Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ametoa ufafanuzi wa baadhi ya tozo alizowasilisha bungeni wakati wa Mapendekezo ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/22 na kuleta mkanganyiko kwa wananchi ikiwemo makato ya miamala ya simu, kodi ya majengo kwa njia ya Luku na Makato yanayopendekezwa ya mafuta kwa ajili ya ujenzi wa barabara.
Dkt. Nchemba ametoa kauli hiyo Jijini Dodoma alipokutana na kuzungumza na Wahariri wa vyombo vya habari nchini kupitia Jukwaa la Wahariri (TEF), katika kikao kilichoandaliwa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Dkt. Nchemba alisema kuwa kodi hizo zimetafsiriwa kinyume na lengo la Serikali, ambapo kwenye kodi ya kuongeza salio mtu akiweka kuanzia Sh. 1000 hadi Sh. 2500, atatozwa shilingi 10, shilingi 2500 hadi 5000 atatozwa Sh. 21, shilingi 50,000 hadi 100,000 atatozwa shilingi 186 na shilingi 100,000 kwenda juu anatozwa shilingi 200 na sio kila siku ni pale anapoweka mud awa maongezi.
“Hatujaweka kodi kwenye laini za simu kama ambavyo baadhi ya wananchi wamekuwa wakichanganya, hata kule Bungeni wanachanganya wanasema sasa kila siku itakuwa inakatwa shilingi 10 mpaka 200 kwa hiyo kama ni 200 kwa siku 30 ni shilingi 6000, halafu hata kama hukuweka fedha, siku ukiweka inakatwa kama nipige tafu, hatukuweka hivyo”, alieleza Dkt. Nchemba.
Alibainisha kuwa haimaanishi kwamba shilingi 10 sio mzigo lakini Serikali iliangalia matatizo yaliyopo na kugundua kuwa yanagharimu zaidi, kuliko thamani ya shilingi 10 itakayotozwa kama kodi.
Alifafanua kuwa miradi mikubwa inayotekelezwa nchi ukiwemo wa mradi wa Bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere ambao unahitaji zaidi ya shilingi trililioni nne na ujenzi wa Reli ya Kisasa unaohitaji zaidi ya shilingi trilioni 20 ili kukamilika, iwapo fedha zote zitategemea mikopo nchi itapitiliza uwezo wa kukopa na kutokukopesheka hivyo ushiriki wa wananchi ni muhimu.
Akielezea kuhusu kodi ya miamala ya simu Dkt. Nchemba alisema kuwa kila mwananchi atakaopofanya miamala kwenye simu chini ya shilingi 1000 kodi hiyo haiwahusu, kuanzia shilingi 1000 hadi 2000 atatozwa shilingi 10, shilingi 10,000 hadi 15, 000 atatozwa shilingi 300, shilingi 30,000 na kuendelea atatozwa shilingi 1000 na shilingi milioni tatu na kuendelea watatozwa shilingi 10,000.
Kuhusu Kodi ya Majengo kwa kutumia LUKU alisema kuwa mfumo huo mpya unatumika katika nchi nyingi Duniani na unarahisisha ukusanyaji wa mapato kuliko mfumo ulikuwepo ambao unawafanya watu kutumia muda mwingi kwenye foleni.
Kwa upande wa kodi katika mafuta, alisema ongezeko la kodi hiyo itasaidia kukarabati, kujenga na kufufua barabara ambazo ni muhimu katika usafiri na usafirishaji.
Alisema kutumia barabara mbovu ni gharama kubwa kuliko ongezeko la kodi hiyo kwenye mafuta, akitolea mfano wa vifo vya wakinamama wajawazito wanopokwenda kujifungua kutokana na ubovu wa barabara hizo.
Kwa kuwafuata walipa kodi kwa njia ya kawaida hatuzidi watu laki mbili, kwa kutumia Mita za umeme watu wamezidi milioni tatu kwa hiyo tukaona kwa nini tusitumie utaratibu huu wa digitali ili kuwaondolea watu usumbufu.
Waziri Dkt. Nchemba alisema kuwa fedha zitakazopatikana katika kodi hizo zitawekwa moja kwa moja kwenye mifuko husika kama mfuko wa Barabara na elimu hivyo kutumika kwa kusudi lililowekwa.
Kwa upande wao wahariri walioshiriki semina hiyo wamempongeza Waziri Dkt. Nchemba pamoja na uongozi wa Wizara kwa kutoa ufafanuzi huo na kuomba kuendelea na utaratibu huo ili kuondoa mikanganyiko kwa wananchi.