***************************
Na Mwamvua Mwinyi,Mafia
MKUU wa mkoa wa Pwani, Aboubakar Kunenge ,amemuagiza Mkurugenzi na Vyombo vya Dola Wilayani Mafia kuanza uchunguzi na kuchukua hatua kwa watumiaji (Watumishi) wote ambao wametumika kuzalisha hoja za ukaguzi wa mahesabu.
Amewataka watumishi kufuata utaratibu, kuheshimu sheria na kuwasilisha nyaraka katika Matumizi yote ya Fedha ili kuepuka kuzalisha Hoja hizo.
“Sitopenda kuona hoja zinaongezeka na kujirudia kwa mwaka ujao” alisema Kunenge
Aliyasema hayo , wakati aliposhiriki kikao Maalumu cha Baraza la Madiwani kupitia na Kujadili Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) Mwaka 2019/2020 Wilayani Mafia.
Kunenge amewataka kufunga hoja za ukaguzi kabla hazijafika kwenye hatua ya kutakiwa kujieleza ili kuepuka kuzalisha hoja zaidi.
Aidha aliitaka Halmashauri hiyo kubuni vyanzo vipya vya mapato kusimamia ukusanyaji wa mapato na kudhibiti matumizi.
Kunenge aliwaeleza amekuja Pwani kufanya kazi na kuwataka Wataalamu wote Mkoani hapo kuandaa Taarifa yenye Fursa zote Muhimu katika sekta zilizopo ikiwemo vyanzo vya Mapato, Huduma za Kijamii, Viwanda Kilimo, Biashara, Utalii, Uvivu ili kupata hali ilivyo kwa sasa na kuainisha maeneo yote yanayohitaji maboresho.
Pia Kunenge alieleza kuwa ili kuleta maendeleo ya haraka ya Mafia ni lazima Viongozi na Wafanyakazi Wilayani hapo kuondokana na dhana ya Mafia ni eneo la pembezoni lenye shida, amewataka kuanza kunadi upya Wilaya ya Mafia.
Kuhusu Changamoto ya uhaba wa watumishi, Taa kwenye Kiwanja cha Ndege, Tozo za magari mara mbili kwenye Bandari ya Nyamisati na Kilindoni mafia amesema ameyachukua na atayafanyia kazi.