Home Mchanganyiko BALOZI MULAMULA AKUTANA KWA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA MAREKANI HAPA NCHINI

BALOZI MULAMULA AKUTANA KWA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA MAREKANI HAPA NCHINI

0

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb.) amekutana
kwa mazungumzo na Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Dkt. Donald J. Wright, jijini Dodoma leo tarehe 15 Juni 2021.

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamejadili umuhimu wa kuendelea kuimarisha
ushirikiano baina nchi hizi mbili. 

Akizungumza kwenye mkutano huo, Balozi Mulamula
amemhakikishia Balozi Wright ushirikiano hususan kupitia Sekta muhimu ambazo
nchi hizi mbili zinashirikiana kwa muda mrefu ikiwemo sekta ya afya, elimu,
miundombinu, teknolojia, uwekezaji na biashara.

“Leo nimekutana na Balozi wa Marekani hapa
nchini ikiwa ni utaratibu niliojiwekea wa kukutana na Mabalozi wawanaowakilisha
nchi zao hapa Tanzania mara kwa mara kwa  lengo la kubadilishana nao mawazo kuhusu namna
bora ya kuimarisha uhusiano wetu na nchi hizo. Katika mazungumzo yangu na
Balozi Wright tumejadili masuala mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo mpango wanaoufadhili
wa kupambana na UKIMWI wa PEPFAR na jambo kubwa amenijulisha kuwa Marekani ipo
tayari kushirikiana na Tanzania na kwamba kampuni nyingi za nchi hiyo zipo tayari
kuja kuwekeza na kufanya biashara hapa nchini wakati wowote kuanzia sasa”
alisema Balozi Mulamula.

“Pia amenifahamisha kuwa, Tanzania mwaka huu
imekuwa miongoni mwa nchi za Afrika zinazostahili kupeleka bidhaa zake za
kilimo nchini Marekani bila kutozwa ushuru kupitia Mpango wa AGOA. Hii ni fursa
muhimu kwetu na kinachotakiwa sasa ni sisi kujiimarisha katika kuzalisha bidhaa
bora zitakazokidhi vigezo vya kuingia kwenye soko la Marekani” alisisitiza  Mhe. Waziri.

Kwa upande wake, Balozi Wright amemshukuru Mhe.
Balozi Mulamula kwa kumpokea na kueleza kuwa nchi yake inathamini na kuuenzi ushirikiano
wa muda mrefu uliopo kati yake na Tanzania na kwamba itaendelea kuuimarisha
ushirikiano huo kwa kuchangia sekta mbalimbali.

“Nimekuwa na mkutano mzuri na Mhe. Balozi Mulamula
na tumejadili masuala muhimu na yenye manufaa kwa nchi zetu mbili hususan
umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kupitia sekta mbalimbali. Marekani inaihesabu
Tanzania kama rafiki na mshirika muhimu hivyo mkutano huu ni moja ya jitihada
za kuimarisha ushirikiano na urafiki huo” alieleza Balozi Wright.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb.) akizungumza na Balozi wa Marekani nchini, Mhe. Dkt. Donald J. Wright walipokutana kwa mazungumzo Ofisini kwake jijini Dodoma tarehe 15 Juni 2021. 

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Hassan Mwamweta akiwa na Msaidizi wa Waziri, Balozi Grace Martin wakifuatilia mazungumzo kati ya Mhe. Waziri Mulamula na Balozi Wright (hawapo pichani)

Maafisa kutoka Ubalozi wa Marekani walioongozana na Mhe. Balozi Wright nao wakifuatilia mazungumzo

Mazungumzo yakiendelea

Mazungumzo yakiendelea

Picha ya pamoja kati ya  Mhe. Waziri Mulamula na Mhe. Balozi Wright

Picha ya pamoja