Na mwandishi wetu
WAAJIRI kutoka Sekta Binafsi
sasa watalipa asilimia 0.6 ya michango ya wafanyakazi wao kwenda Mfuko wa Fidia
Kwa Wafanyakazi (WCF) badala ya asilimia 1 ya awali kuanzia Tarehe 1/7/2021, WAZIRI
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mheshimiwa Jenista
Mhagama (MB), amesema leo Juni 13, 2021 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Katiba na Sheria wakati walipotembelea ofisi za WCF jijini Dar es Salaam kwa lengo
la kufuatilia utekelezaji wa maelekezo mbalimbali ya Kamati ikiwemo kuwekeza
katika mifumo ya TEHAMA na uboreshe mfumo wa tathmini ya madai, alisema waajiri
kutoka Sekta ya Umma wataendelea kulipa kiwango cha awali cha asilimia 0.5
“Mama yetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani alitoa maelekezo kwa kila
taasisi ya serikali iweke mazingiza mazuri ya kuvutia wawekezaji na kupunguza
kero zilizokuwa zinaleta changamoto, bila ya kupoteza muda Ofisi ya Waziri Mkuu
imeanza kuchukua hatua, na katika kero kubwa iliyokuwa inawakwaza wawekezaji na
waajiri nchini hasa Sekta Binafsi ni ule uwiano wa michango asilimia 0.5 Sekta
ya Umma na asilimia 1 kwa sekta binafsi, sasa tumetekeleza kwa kuondoa huo
mzigo wa uchangiaji.” Alisema Mheshimiwa Waziri.
Pia Mheshimiwa Waziri alisema
sambamba na hilo, Serikali kupitia WCF inafikiria kufuta malimbikizo ya madeni
ya michango ya huko nyuma ili kuwepo kwa mazingira mazuri kwa wale
Waajiri ambao hawajajisajili ili waweze kujisajili na isiwe kikwazo kwao na waliojisaljili
watekeleze wajibu wa kulipa michango.
Alisema kipaumbele cha Serikali ni kuimarisha Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF)
ili uendelee kulipa fidia kwani huduma za hifadhi ya jamii ni haki ya kikatiba.
“Hifadhi ya jamii ni haki ya
kikatiba kwa mujibu wa Ibara ya 11(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya Mwaka 1977. Ibara hii inaipa Serikali wajibu wa kuweka mazingira ya
kisera na kisheria kwa lengo la kuhakikisha, pamoja na mambo mengine, kwamba
kila mwananchi anapata kinga wakati wa uzee, ugonjwa au ulemavu.” Alifafanua
Mheshimiwa Mhagama.
Waziri huyo aliwahakikishia
wajumbe hao kuwa ripoti ya mtathmini (Acturial report) imeonyesha kazi ya Mfuko
ni nzuri na Mfuko unaendelea vema na kuitaka Menejimenti iendelee kuchapa kazi
kwa kujituma na kuweka uzalendo mbele.
“Katika uhai wake wa miaka sita tangu uanzishwe Mfuko umekutekeleza takwa
hilo la kikatiba kwa mafanikio makubwa ambapo mwaka 2015-2016 ulilipa Fidida ya
Shilingi Bilioni 1.55 na sasa Fidia imefikia hadi shilingi bilioni 9.05.
Kwa upande wake Makamu Mwenyemkiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Najma Giga alisema,
Kamati yake imeridhishwa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Mfuko katika kutekeleza
maelekezo ya Kamati ambapo hivi sasa huduma za Mfuko zimerahisishwa kufuatia matumizi
ya TEHAMA ambapo huduma mbalimbali zinafanyika kidigitali.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma alieleza mafanikio mbalimbali
katika upande wa makusanyo ya michango, mifumo ya kutolea huduma, uwekezaji, malipo
ya fidia na katika kipindi chote cha utekelezaji wa majukumu yake, Mfuko umekuwa
ukipata hati safi ktoka kwa Mkaguzi Mkuu.
“Pamoja na mafanikio haya pia kuna changamoto kama vile uelewa mdogo, lakini
pia waajiri kutowasilisha nyaraka za ukweli na sahihi, lakini pia Mfuko unaelekeza
nguzu zake katika kuhakikisha unaondoa changamoto ya madaktari kwa kuendelea kutoa
mafunzo nchi nzima.” Alisema Dkt. Mduma.
Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Tathmini WCF, Dkt. Abdulsalaam Omary akifafanua baadhi ya hoja za Wajumbe
Baadhi ya Wajumbe wakiwa kwenye kikao hicho
Baadhi ya Wajumbe wakiwa kwenye kikao hicho
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mheshimiwa Jenista Mhagama(katikati) akijadiliana Jambo na Mkurugenzi MKUU wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma ( kulia), MAKAMU Mwenyekiti wa Kati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na SHERIA, Mhe. Giga na NAIBU KATIBU MKUU Ofisi ya WAZIRI MKUU, Profesa Jamal Adam, wakati wa ziara ya Kamati hiyo kutembelea Ofisi za Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) jijini Dar es Salaam juni 13, 2021.