*************************
Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) inaendesha mafunzo ya ujaribishaji wa miongozo ya elimu ya stadi za Maisha kwa walimu wa shule za Msingi na Sekondari nchini.
Akifungua mafunzo hayo katika wilaya ya Temeke ,Mkurugenzi wa Mafunzo ya Mitaala (TET) Bi.Fika Mwakabungu amesema kuwa ,walimu 1696 katika halmashauri 13 nchini watapatiwa mafunzo hayo na kisha wataweza kuwafundisha wenzao ili wakatoe uelewa wa stadi za maisha.
“Karne hii ya 21 wanafunzi wanapaswa kuandaliwa mapema kwani wanakutana na mambo mengi hivyo tunapowaandaa mapema kujua masuala mbali mbali wataweza kuepukana na changamoto” alisema Bi Fika.
Mafunzo hayo ya stadi za maisha yanahusisha masuala ya afya,afya ya uzazi,Vvu na ukimwi na jinsia na namna ya kuondokana na ukatili wa kijinsia.
Kwa upande wake,mwezeshaji wa mafunzo hayo ,Bi.Amina Tou ameeleza kuwa,wana imani walimu wanaohudhuria mafunzo hayo wataweza kuwaelimisha wengine katika shule zao ambapo pia watahakikisha kwamba wanafunzi watakaopewa elimu hiyo iwasaidie.
Mafunzo hayo yameanza kufanyika leo katika halmashauri 13 ambazo ni; Ilala, Temeke, Ngorongoro, Ifakara, Kasulu, Kisarawe, Kibondo, Ulanga ,Morogoro mjini,Malinyi,Sengerema,Bagamoyo na Mlimba.