Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Florens Luoga, wakifungua jiwe la msingi la jengo jipya la BoT Tawi la Mwanza.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa jengo jipya la Benki Kuu ya Tanzania Tawi la Mwanza. Kulia kwake ni Gavana wa BoT Prof. Florens Luoga, Waziri wa Madini Mhe. Dotto Biteko na Mkurugenzi wa Tawi la BoT Mwanza Dkt. James Machemba. Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Zanzibar, Mhe. Dkt. Juma Malik Akil, na Manaibu Gavana Dkt. Yamungu Kayandabila, Dkt. Bernard Kibesse na Julian Banzi Raphael.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akipewa maelezo na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Florens Luoga kuhusu muundo wa jengo jipya la BoT Tawi la Mwanza baada ya kulifungua rasmi leo jijini Mwanza.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Florens Luoga, akisoma risala wakati wa ufunguzi rasmi wa jengo jipya la Benki Kuu ya Tanzania Tawi la Mwanza.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akitoa hotuba wakati wa ufunguzi rasmi wa jengo jipya la Benki Kuu ya Tanzania Tawi la Mwanza.
Baadhi ya viongozi wa serikali, wakurugenzi wa taasisi mbalimbali na wananchi wakifuatilia tukio la ufunguzi rasmi wa jengo jipya la Benki Kuu ya Tanzania Tawi la Mwanza, ambapo mgeni rasmi alikua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Wakurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania waliohudhuria ufunguzi rasmi wa jengo jipya la BoT Tawi la Mwanza wakiwa katika viwanja vya Tawi hilo kabla ya ufunguzi huo.
Baadhi ya Wafanyakazi wa Benki Kuu ya Tanzania wakifuatilia tukio la ufunguzi rasmi wa jengo jipya la Benki Kuu ya Tanzania Tawi la Mwanza, ambapo mgeni rasmi alikua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
…………………………………………………………………………………..
Rais Samia Suluhu Hassan amesema baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa kumbukumbu za mikopo na wakopaji, masharti magumu na riba kubwa za mikopo katika benki na taasisi za fedha zinatakiwa kushuka.
Ametoa kauli hiyo wakati akihutubia katika viwanja vya Tawi la Benki Kuu ya Tanzania jijini Mwanza baada ya kufungua rasmi jengo jipya la tawi hilo tarehe 13 Juni 2021.
Amesema riba za mikopo inayotolewa na benki an taasisi za fedha inatakiwa kuwa angalau asilimia 10 kwenda chini, badala ya asilimia 12 hadi 19 ilivyo sasa, hata baada ya kuanza kutumika mfumo wa taarifa za mikopo na wakopaji.
“Ndio sababu serikali ilitunga sera ya taasisi ndogo za fedha ili kuimarisha uratibu. Pamoja na kupitishwa kwa sera, sheria na kanuni hizo, bado baadhi ya taasisi ndogo za fedha zinaendelea kutoza riba kubwa,” alieleza Rais Samia na kuitaka Benki Kuu kushughulikia suala hilo.
Alisema matarajio ni kwamba wananchi waweze kukopa na kukua katika maisha yao. “Tunayemwita machinga leo, tunataka aendelee kukua afikie kuwa mfanyabiashara mdogo; asibaki katika ngazi yake ile ile,” alisema.
Rais ameitaka Benki Kuu kuhamasisha na kujenga mazingira mazuri ili benki zitoe mikopo ya muda mrefu, akisema mikopo ya muda mfupi inakuwa vigumu kukuza sekta za viwanda, kilimo na kuboresha makazi ya wananchi wetu.
Aidha, ametoa wito kwa Benki Kuu kushirikiana na wadau, ikiwemo Wizara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kusaidia uanzishaji wa kanzidata ya pili kwa taasisi zilizoanzisha mifumo ili ziweze kutumika endapo kanzidata mama itapata matatizo. Hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama kubwa zinazohitajika kuwa na kanzidata mbili.
Rais alisema, kufuatia Tanzania kuingia katika nchi zilizo katika uchumi wa kati, upatikanaji wa misaada na mikopo nafuu utapungua na hivyo akaeleza kwamba ni muhimu kuanza kuumiza vichwa namna ya kupata fedha. Aliipongeza Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuanza mchakato wa tathmini ya nchi kukopesheka (sovereign credit rating assessment) ili kujenga imani kwa taasisi za fedha za kimataifa kuendelea kutukopesha.
Aidha, Rais ameiagiza Benki Kuu kuanza kufuatilia teknolojia ya fedha za kidigitali (blockchain) ili kuhakikisha katika mapinduzi ya nne ya viwanda ambayo yanaongozwa na teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) Tanzania haiachwi nyuma
“Tumeshuhudia kuibuka kwa sarafu mpya zinazotumika kwa njia ya mtandao, yaani blockchain, au cryptocurrency. Najua bado nchi ikiwemi Tanzania hazijakubali kuanza kutumia sarafu hizi. Hata hivyo, wito wangu kwa Benki Kuu ni vyema mkaanza kufanyia kazi maendeleo haya. Kujitayarisha tu. yakija yakitukamata, yasitukamate hatuko tayari,” alisema.
Aidha, Rais ameipongeza Benki Kuu kwa kazi nzuri inayofanya katika kujenga uchumi wa taifa na kuwataka wafanyakazi kuendelea kuchapa kazi wakitanguliza mbele maslahi ya taifa.
“Kwa ujumla, Benki Kuu ya Tanzania imejitahidi sana kutimiza majukumu yake kwa ukamilifu,” alisema Rais na kutaja kuimarika kwa uchumi kama uthibitisho wa kazi ya Benki Kuu hadi kuwezesha Tanzania mwaka jana kutambuliwa na Benki ya Dunia kuingia katika nchi zilizo katika uchumi wa kati.
Alisema licha ya mlipuko wa ugonjwa wa corona, Tanzania imeendelea kushuhudia ukuaji chanya wa uchumi kufikia asilimia 4.8 mwaka huu, wakati mataifa mengi yalipata ukuaji wa uchumi hasi.
Viongozi wengine waliozungumza katika hafla hiyo ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel, Mwakilishi wa Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango wa Zanzibar, Dr. Juma Malik Akil, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Florens Luoga, na Waziri wa Madini na Kaimu Waziri wa Fedha na Mipango, Bw. Dotto Biteko.