*****************************
TAREHE 12 Juni ya kila mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ajira kwa Watoto Duniani – World Day against Child Labour. Siku hii ilianzishwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) mwaka 2002 kwa madhumuni ya kutoa elimu ili kuzuia ajira kwa watoto.
Shirika la Kazi kupitia Mkataba wa Kimataifa Na. 138, liliweka umri wa ajira kuwa miaka 15 na kuendelea, na katika Mkataba Na. 182 liliorodhesha ajira zisizokubalika kwa watoto na ambazo zinatakiwa kuzuiwa.
Jumuiya ya Kimataifa imeutangaza mwaka 2021 kuwa ni mwaka wa kimataifa wa kutokomeza ajira kwa watoto. Hatua hii ni muhimu sasa kutokana na hatua mbalimbali zilizokwishachukuliwa awali za kuondokana na tatizo la ajira kwa watoto kutishiwa kuvurugika kutokana na janga la CORONA (Covid 19) lililoikumba dunia.
Tunapoadhimisha siku hii, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inaungana na wadau mbalimbali wa haki za mtoto duniani katika kupinga ajira kwa watoto, sambamba na kuelimisha jamii juu ya madhara ya ajira hizo. Aidha, Tume itaendelea kuhamasisha jamii kuheshimu Mikataba mbalimbali ya Kimataifa ambayo Tanzania imeridhia, pamoja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Sheria, Sera na Mipango mbalimbali inayolinda haki za mtoto nchini.
Tume inatambua na kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kutokomeza ajira kwa watoto ikiwa ni pamoja na kutunga Sheria ya Mtoto Sura ya 13 ambapo kupitia kifungu cha 12 kinaelekeza kuwa mtoto hatahusishwa katika kazi yoyote ambayo inaweza kumsababishia madhara kiafya, kielimu, kiakili, kimwili na katika ukuaji wake.
Pamoja na hayo, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Sura ya 366 inaelekeza wazi kuwa mtoto ataajiriwa katika kazi zinazofaa ambazo siyo ngumu na zisizoathiri mahudhurio yake shuleni na haki zake nyingine.
Vile vile, Serikali iliandaa Kanuni za Usimamizi wa Utumikishwaji wa Watoto katika Bodi za Mazao na kuwajengea uwezo walimu na watumishi wa sekta ya kilimo kuhusu mbinu za kuzuia utumikishwaji katika sekta ya kilimo na sekta nyingine za uchumi. Hatua hizi zimeenda sambamba na utoaji wa elimu kupitia kampeni mbalimbali kwa lengo la kuzuia utumikishwaji wa watoto katika mashamba.
Pamoja na jitihada mbalimbali zilizochukuliwa bado zipo changamoto kadhaa, ikiwemo watoto kuendelea kufanyishwa kazi ngumu katika maeneo ya kazi za ndani, mashambani, mitaani, na migodini. Ajira hizi zimekuwa kichocheo cha ukatili dhidi ya watoto ambapo baadhi yao hukosa masomo kunyonywa kiuchumi na matatizo ya kiafya jambo linaloathiri ukuaji wao.
Sababu kubwa ya ajira kwa watoto ni umasikini na kukosa uelewa juu ya madhara ya ajira hizo, hali inayowaathiri zaidi watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani; kwani wanahitaji kufanya kazi ili kujikimu.
Kauli mbiu katika maadhimisho ya mwaka huu ni “Chukua hatua: Tokomeza Utumikishwaji Watoto.” Tume inaungana na wadau mbalimbali kuendelea kuihamasisha jamii kuchukuwa hatua mbalimbali kama vile kutoa elimu kuhusu madhara ya utumikishaji wa watoto kwa lengo la kutokomeza ajira hatarishi kwa watoto nchini.
Kupitia maadhimisho haya, Tume inatoa wito kwa umma, Serikali na wadau wa haki za watoto kuunganisha nguvu kupinga ajira kwa watoto mahali popote nchini. Aidha, Tume inapendekeza yafuatayo:
- Serikali iendelee kuwasaidia watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani kurejea shuleni kwa kujenga mifumo bora itakayowawezesha kupata mahitaji yao ya kila siku.
- Serikali iandae mkakati kabambe wa kuwabaini wanaowaajiri watoto na iwawajibishe kisheria.
- Pia jamii iendelee kutoa ushirikiano kwa kuwafichua watu wote wanaowaajiri watoto.
- Wazazi wahakikishe wanawatunza, kuwalinda na kuwapatia watoto mahitaji yao ya msingi. Aidha, wahakikishe watoto wote wanahudhuria shule na hawawatumii kama vitega uchumi vya familia kwa kuwafanyisha kazi ngumu, zisizofaa na zinazowaathiri.
- Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali iendelee kutoa elimu ya haki za mtoto na madhara ya ajira mbaya kwa watoto.
“Chukua hatua sasa: tokomeza ajira kwa watoto”