Mkutano wa 31 wa
Baraza la Mawaziri la Kisekta linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na
Mipango umefanyika jijini Arusha hivi karibuni huku Mawaziri
wakipitisha agenda mbalimbali zilizowasilishwa kwao.
Katika hotuba yake ya
ufunguzi, Mwenyekiti wa Mkutano huo ambaye ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki na Maendeleo ya Kikanda wa Kenya, Mhe. Aden Mohammed amepongeza kazi
kubwa iliyofanywa na vikao vilivyotangulia vya Wataalam na Makatibu Wakuu ya kukamilisha
agenda mbalimbali muhimu na kwamba anayo furaha kwa mikutano mbalimbali kuanza
kufanyika jijini Arusha na kuhudhuriwa na Wajumbe kutoka Nchi Wanachama baada
ya vikao hivyo kufanyika kwa muda mrefu kwa njia ya mtandao kutokana na mlipuko
wa ugonjwa wa corona.
Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Peter Muthuki aliwakaribisha Mawaziri kwenye Makao
Makuu ya[H1]
Jumuiya hiyo na alitumia fursa hiyo kuzipongeza Tanzania na Uganda kwa kuendesha
zoezi la uchaguzi kwenye nchi zao kwa amani na utulivu. Kadhalika, alitoa
shukrani kwa Nchi Wanachama kwa kuendelea kushirikiana kikamilifu na
Sekretarieti ya Jumuiya hiyo na kuiwezesha kutekeleza majukumu yake ya kila
siku kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula
ambaye alishiriki mkutano huo kwa mara ya kwanza kwa njia ya mtandao akiwa
jijini Dar es Salaam, alitumia fursa hiyo kumpongeza Mwenyekiti wa mkutano huo
pamoja na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuteuliwa kuiongoza
Jumuiya hiyo na kuwahakikishia ushirikiano kutoka kwake binafsi na kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mkutano wa Mawaziri ulitanguliwa
na Mkutano kwa Ngazi ya Wataalam uliofanyika tarehe 7 hadi 9 Juni 2021 na
kufuatiwa na Mkutano wa Makatibu tarehe 10 Juni 2021.
Pamoja na mambo mengine
Mkutano huo umepokea na kupitisha agenda mbalimbali zilizowasilishwa ikiwa ni
pamoja Taarifa ya Utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa kwenye vikao
vilivyopita; Taarifa kuhusu hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Itifaki ya
Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki; Taarifa kuhusu ombi la Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Congo la kujiunga na EAC; Taarifa kuhusu hatua iliyofikiwa
ya utatu wa Jumuiya za EAC-COMESA-SADC katika Eneo Huru la Biashara Barani
Afrika na Taarifa ya Uchangiaji wa Bajeti ya EAC kutoka Nchi Wanachama.
Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano
wa Ngazi ya Mawaziri umeongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohammed Mchengerwa aliyemwakilisha
Mhe. Balozi Mulamula ambaye alishiriki kwa njia ya mtandao.
Viongozi wengine walioshiriki Mkutano
huo ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Prof. Adelardus Kilangi, Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uwekezaji, Uchumi na Ajira Zanzibar, Mhe. Mudrick
Ramadhan Soraga, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Mhe. Dkt. Godwin Mollel, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi na Utawala Bora, Dkt. Laurean Ndumbaro, Katibu Mkuu wa
Wizara ya Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Bw. Mussa Haji Ali na Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na
Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi
Stephen Mbundi.
Mhe. Mchengerwa akichangia hoja wakati wa Mkutano wa 31 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango uliofanyika jijini Arusha tarehe 11 Juni 2021 |
Ujumbe wa Burundi ukiongozwa na Mhe. Balozi Ezechiel Nabigira (kushoto), Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Vijana, Michezo na Utamaduni |
Ujumbe wa Rwanda ukiongozwa na Mhe. Prof. Manasseh Nshuti (kushoto), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
|
Ujumbe wa Kenya ukiwa kwenye Mkutano wa 31 Baraza la Mawaziri la Kisekta linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango uliofanyika jijini Arusha tarehe 11 Juni 2021 |
Ujumbe wa Uganda ukishiriki Mkutano wa 31 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango uliofanyika jijini Arusha tarehe 11 Juni 2021 |
Ujumbe wa Sudan Kusini ukishiriki Mkutano wa 31 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango uliofanyika jijini Arusha tarehe 11 Juni 2021 |
Ujumbe wa Tanzania ukishiriki Mkutano wa 31 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango uliofanyika jijini Arusha tarehe 11 Juni 2021 |
Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania |