Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato (katikati) akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), wakati wa Semina iliyoratibiwa na Wizara ya Nishati ili kuwajengea uelewa kuhusu sekta ndogo ya umeme iliyofanyika Juni 10, 2021 jijini Dodoma. Kulia ni Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Kheri Mahimbali (kushoto).
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali (katikati) akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), wakati wa Semina iliyoratibiwa na Wizara ya Nishati ili kuwajengea uelewa kuhusu sekta ndogo ya umeme iliyofanyika Juni 10, 2021 jijini Dodoma.
Baadhi ya Watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi zilizo chini yake wakimsikiliza Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka (hayupo pichani). Kutoka kushoto ni Mhandisi Juma Mkobya kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Amos Maganga, Mhandisi Jacob Mayala, Mhandisi Shukurani Rugaimukamu na Mhandisi Zuwena Mkwanya kutoka Wizara ya Nishati, iliyofanyika Juni 10, 2021, Jijini Dodoma
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), wakisikiliza Mada kutoka kwa Meneja Mkuu wa Kampuni Tanzu ya Kusafirisha na Kusambaza Umeme (EDTCO), Mhandisi Maclean Mbonile wakati wa Semina iliyoratibiwa na Wizara ya Nishati ili kuwajengea uelewa kuhusu sekta ya ndogo ya umeme iliyofanyika Juni 10, 2021 Jijini Dodoma.
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Mhandisi Isaac Kamwelwe akichangia hoja wakati wa Semina iliyoratibiwa na Wizara ya Nishati ili kuwajengea uelewa kuhusu sekta ndogo ya umeme iliyofanyika Juni 10, 2021 Jijini Dodoma.
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Aida Khenan akichangia hoja wakati wa Semina iliyoratibiwa na Wizara ya Nishati ili kuwajengea uelewa kuhusu sekta ya ndogo ya umeme iliyofanyika Juni 10, 2021 Jijini Dodoma.
*****************
Na Zuena Msuya – Dodoma
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), wameshiriki katika semina iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati iliyolenga kuwajengea uelewa kuhusu majukumu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Akizungumza wakati wa semina hiyo iliyofanyika Jijini Dodoma, Juni 10, 2021, Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka aliipongeza Wizara ya Nishati kupitia REA na TANESCO kwa kazi kubwa na nzuri ya kusambaza na kuwaaunganishia wananchi umeme katika maeneo mbalimbali.
Semina hiyo iliwashirikisha pia Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt.Tito Mwinuka, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga pamoja na Viongozi wengine Waandamizi wa Wizara hiyo na Taasisi zilizo chini yake.
Katika Semina hiyo, pamoja na mambo mengine, Wajumbe wa PAC walijengewa uelewa juu ya shughuli zinazofanywa na TANESCO kupitia Kampuni tanzu ya Kusafirisha na Kusambaza Umeme (EDTCO) ambayo ina jukumu kubwa la kujenga miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme.
Vilevile miradi mbalimbali inayotarajiwa na inayoendelea kutekelezwa na REA katika kuhakikisha umeme unawafikia watanzania wote hususan walioko vijijini.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato aliwaeleza wajumbe hao mipango na mikakati ya Wizara ya Nishati kupitia TANESCO na REA juu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa katika sekta ya nishati na ile ambayo inatarajiwa kutekelezwa.
Aidha, Wakili Byabato alisema kuwa, lengo la Wizara hiyo ni kuhakikisha kuwa azma ya serikali ya kuunganisha umeme katika vijiji vyote ambavyo havijafikiwa na nishati hiyo nchini inatimia ifikapo 2022, kupitia miradi mbalimbali ya usambazaji wa umeme.
Aliwaomba Wajumbe hao wa Kamati kuendelea kuwahamasisha wananchi wanaowawakilisha kuchangamkia fursa ya kulipia shilingi 27,000 ili kuunganishiwa umeme katika nyumba zao ili wananchi wengi zaidi waweze kuunganishiwa umeme.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Kheri Mahimbali aliwaeleza Wajumbe hao wa kamati kuwa Wizara kwa kushirikiana na Taasisi zilizo chini yake wataendelea kushirikiana na Wabunge kuhakikisha kuwa wananchi wanaowawakilisha wanapata huduma stahiki hasa katika sekta ya ndogo ya umeme.
Akizungumzia mafanikio yaliyofikiwa na Wizara kupitia sekta ndogo ya umeme, alibainisha kuwa ni pamoja na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za kijamii ikiwemo katika vituo vya afya, maji, elimu, kukuza na kuboresha uchumi wa wananchi hasa wale wanaotumia nishati hiyo kwa kuanzisha viwanda mbalimbali.