Home Makala USIYOYAJUA KUHUSU HIFADHI YA GESIMASOWA,NDEGE ANAYESAFIRI DUNIA NZIMA HUPUMZIKA HAPA 

USIYOYAJUA KUHUSU HIFADHI YA GESIMASOWA,NDEGE ANAYESAFIRI DUNIA NZIMA HUPUMZIKA HAPA 

0

Ndege maarufu duniani  mwenye uwezo wa kusafiri toka bara moja kwenda bara jingine anayefahamika kwa jina la Derhams anapumzika kwa muda ndani ya hifadhi ya Gesimasowa kabla ya kuendelea na safari

 Hifadhi ya Gesimasowa iliyopo Halmashauri ya Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma

Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema akizungumza  ndani ya hifadhi ya Gesimasowa 

Milima ya livingistone mwambao mwa ziwa Nyasa  eneo la Chiwindi ambapo pia ndege hao wanapumzika kwa muda na kuendelea na safari

Samaki aina ya mbelele na mbasa ambao huzaliana katika maingilio ya mto Ruhuhu ndani ya hifadhi ya Gesimasowa,kisha hushuka hadi ziwa Nyasa

………………………………………………………………..

Na Albano Midelo

Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa nchini ambayo imebarikiwa kwa kuwa na neema ya vivutio lukuki na adimu vya utalii wa ikolojia na kiutamaduni.

Hifadhi ya Gesimasowa yenye ukubwa wa kilometa za mraba zaidi ya 760 ambayo ipo katika Halmashauri ya Madaba Wilaya ya Songea,ni miongoni mwa vivutio adimu vya utalii.

Hifadhi hiyo ilianzishwa kama msitu wa hifadhi mwaka 1975 na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma wa zamani Hayati Dk.Lawrence Gama  mwaka 1975.Hatimaye mwaka 2015,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma katika kipindi hicho hayati Said Mwambungu alisimamia mchakato wa kupandisha hadhi msitu huo na kuwa hifadhi ya Taifa.

Moja ya vivutio vilivyopo katika hifadhi hii ni mapumziko ya ndege maarufu duniani wanazaliana katika Hifadhi ya Taifa ya Kitulo iliyopo Makete mkoani Njombe wanaitwa kitaalam Derhams wenye uwezo wa kuruka toka bara moja hadi bara jingine. 

Afisa Maliasili na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe anabainisha kuwa ndege hao wanapumzika hapa kwa miezi kadhaa kisha wanaendelea na safari kupitia Bonde la ufa hadi ziwa Nyasa hatimaye wanasafiri hadi nchini Afrika ya Kusini na mabara mengine. 

Kulingana na Challe,hifadhi ya Gesimasowa ni mapito ya ndege hao ambao wanatoka Kaskazini mwa Afrika kuelekea Afrika ya Kusini ambao wanafuata milima ya Livingstone iliyopo ziwa Nyasa na kwamba ndege hao pia wanapumzika Mwambao mwa ziwa Nyasa hasa katika eneo la Kihagara ambapo kuna mazingira ambayo yanavutia ndege hao kuishi.

Kwa mujibu wa Challe,Hifadhi ya Gesimasowa pia ina mfumo wa ikolojia wa pori la Selous ambalo sasa ni Hifadhi ya Taifa ya Nyerere kwa sababu ni mapitio ya wanyamapori wanaotoka katika Pori la Akiba la Selous wanapita kuelekea Bonde la ziwa Nyasa kupitia pori la Liparamba hadi Hifadhi ya Niasa nchini Msumbiji ambapo wanyama wanakwenda nchini Msumbiji na kurudi Tanzania.

“Kikao cha Ushauri cha Mkoa wa Ruvuma kimeridhia hifadhi hii kupandishwa hadi kuwa Pori la Akiba la Gesimasowa,mchakato wa kutangaza rasmi katika gazeti la Serikali,Gesimasowa kuwa pori la Akiba upo katika hatua za mwisho’’,anasisitiza Challe.

Wanyama ambao unaweza kuwaona katika hifadhi ya Gesimasoa ni tembo, simba,ndege, nyati, pofu na samaki adimu duniani aina ya mbelele na mbasa.

Hifadhi hii pia ni maingiliano ya mito miwili ya Hanga na Lutukira ambayo inatengeneza mto Ruhuhu unaomwaga maji yake ziwa Nyasa. Mto huo ndiyo mazalia ya samaki aina ya mbelele na mbasa ambao katika duniani nzima wanapatikana ziwa Nyasa pekee.

“Samaki hawa ni adimu sana kwa sababu utafiti umebaini samaki hawa wanapatikana ziwa Nyasa pekee na  wanazaliana katika mto Ruhuhu ambao unachangia asilimia 20 ya maji katika ziwa Nyasa’’,anasema Challe.

Utafiti wa samaki aina mbasa na mbelele katika mto Ruhuhu na ziwa Nyasa ulifanywa na Fransis Challe mwaka 2010 ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kitivo cha Sayansi,Teknolojia na Mazingira na chapisho la utafiti huo lilitolewa mwaka 2011. 

Hata Challe anasema wavuvi katika ziwa Nyasa wanafanya uharibifu wa mazingira kwenye maingiliano ya mto Ruhuhu na ziwa Nyasa eneo la Folkland Lituhi ambapo wanaharibu vifaranga wa  samaki hao ambao wanaingia katika ziwa Nyasa.

Uchunguzi umebaini kuwa katika hifadhi ya Gesimasowa ambako samaki wanazaliana wananchi wamefanya uharibifu mkubwa wa mazingira kwa kukata miti ambayo ni muhimu katika chanzo hicho cha mto Ruhuhu.

Challe anasisitiza eneo la maingiliano ya mto Hanga na Mto Lutukira lililopo katika Hifadhi ya Gesimasowa linatakiwa kulindwa na kuhifadhiwa. 

“Samaki wanazaliana hapa kwenye Maingilio ya mito,kisha wanasafiri hadi ziwa Nyasa na kuendelea na maisha ambapo wakati wa kuzaliana samaki hao wanarudi tena hapa.Hivyo hili ni eneo muhimu sana kitaifa na kimataifa katika Uhifadhi na utalii kwa kuwa samaki hao hawapatikani sehemu nyingine yoyote Duniani’’,anasisitiza Challe.

Hata hivyo anasema hifadhi ya Gesimasowa,bado ni mapya na kwamba lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa maliasili zilizopo katika hiyo zinalindwa ili ziwe endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Kulingana na sheria ya wanyamapori namba tatu ya mwaka 2009 na wananchi hawaruhusu kufanya shughuli zozote ndani ya hifadhi hizo,Wananchi wanajua kabisa hizi ni hifadhi kisheria,hivi sasa tunatekeleza maagizo ya Waziri Mkuu kuhakikisha kuwa wavamizi wote wa maeneo ya hifadhi tunawaondoa’’,anasema Challe.

Kwa mujibu Challe hivi sasa wanyamapori wanahama toka Hifadhi ya Taifa ya Nyerere,wakipitia hifadhi ya Gesimasowa,hifadhi ya Litumbandyosi,Liparamba na kuvuka mpaka hadi hifadhi ya Niassa nchini Msumbiji.

Akizungumzia hatua ambazo Idara ya Maliasili na Utalii inazichukua ili kuhakikisha hifadhi hizo zinalindwa,Challe anasema serikali imeanza kuchukua hatua ikiwemo kuweka alama kubwa za kudumu ili kutenganisha maeneo ya hifadhi na wananchi.

“Tumeanza kutoa elimu kwa wananchi wavue samaki kitaalam bila kuathiri mazalio ya samaki kwa kufuata nyavu zenye matundu yanayokubalika kisheria na kwamba endapo mazalia ya samaki yataharibiwa samaki hao wanaweza kutoweka duniani’’,anasisitiza Challe,

Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema ambaye hifadhi ya Gesimasowa ipo katika wilaya yake anatoa rai kwa wananchi kuacha kukata miti kwenye kingo za mito na kuacha kuvua samaki kwa kutumia nyavu haramu kwenye maingiliano ya mto Ruhuhu ili samaki aina ya mbasa na mbelele wasitoweke duniani.

Mgema anasema tayari wametekeleza agizo la serikali la kuweka mipaka kwenye hifadhi za misitu,mapori na kwenye mapito ya wanyamapori ili kuwadhibiti wananchi wanaovamia maeneo ya hifadhi na kufanya uharibifu mkubwa.

“Vijiji vingi vinavyopakana na hifadhi vinakuwa havijui mipaka yao,ndiyo maana serikali imeamua kufanya zoezi la kuweka alama za kudumu zinazooneka kwenye maeneo yote ili kuondoa hisia za wananchi kuchukuliwa maeneo yao’’,anasema Mgema.

Mwandishi ni Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma

Mawasiliano [email protected],simu 0784765917