Mkurugenzi wa Afya na Lishe ya Jamii, Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) Dkt. Ray Masumo akifungua semina kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu ulaji unaofaa na mitindo bora ya maisha.
Kaimu Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Lishe , Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) Dkt. Esther Nkuba akizungumza jambo jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi semina kwa waandishi wa habari kuhusu ulaji unaofaa na mitindo bora ya maisha.
Afisa Lishe Mtafiti Mwandamizi, Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) Bi. Julieth Shine akiwafundisha waandishi wa habari kuhusu Lishe na magonjwa sugu katika semina iliyoandaliwa na Taasisi ya hiyo jijini Dar es Salaam.
Afisa Mawasiliano Mtafiti, Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) Bw. Fredy Lwoga akieleza katika semina jijini Dar es Salaam kuhusu wajibu wa waandishi wa habari katika kuelimisha jamii kuhusu ulaji unaofaa na mitindo bora ya maisha.
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika semina iliyoandaliwa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) kwa ajili ya kuwajengea uwezo kuhusu ulaji unaofaa na mitindo bora ya maisha.
Afisa Lishe Mtafiti Mwandamizi, Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) Bi. Maria Ngilisho akiwafundisha waandishi wa habari kuhusu vyakula vinavyochangia kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
…………………………………………………………………………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) imetoa mafunzo kwa waandishi wa habari kwa ajili ya kuwapa elimu ya ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha jambo ambalo litawasaidia kuelimisha jamii namna bora ya kuishi ili kuepuka kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo kwa wanahabari, Mkurugenzi wa Afya na Lishe ya Jamii kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) Dkt. Ray Masumo, amesema kuwa wanahabari ni wadau muhimu katika kuelimisha jamii ikiwemo kukabiliana na magonjwa mbalimbali.
Dkt. Masumo amesema kuwa lengo la semina ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha ili kuepuka jamii kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
“Magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanasababishwa na ulaji usiofaa na mtindo isiyo bora wa maisha kwa kutumia vyakula venye chumvi nyingi, mafuta mengi au vinywaji vyenye sukari nyingi ambapo ni miongoni mwa viashiria hatarishi kupata magonjwa yasiyo kuambukiza” amesema Dkt. Masumo.
Amefafanua kuwa mtindo isiyo bora wa maisha ni kutofanya mazoezi, matumizi ya sigara na tumbaku pamoja na unywaji wa pombe ambavyo usababisha mtu kupata magonjwa yasiyo kuambukiza.
Ameeleza kuwa kulingana na tafiti mbalimbali zilizofanywa hivi karibuni zinaonesha ongezeko kubwa la watu wenye uzito uliozidi pamoja na unene uliopitiliza.
Dkt. Masumo ambaye alikuwa anamwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya TFNC, amesema kuwa kutokana na mfumo wa maisha ya ulaji wa chakula usiofaa kuna ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama kisukari, saratani pamoja na magonjwa ya moyo na shinikizo la damu.
“Magonjwa yana athari kubwa katika maendeleo ya taifa letu, lakini yanawezekana kuthibitiwa endapo tutasaidiana kuelimisha jamii kwa kuandika taarifa sahihi ili watu waweze kufata taratibu za ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha” amesema Dkt. Masumo.
Kaimu Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Lishe kutoka Taasisi ya TFNC, Dkt. Esther Nkuba, amesema kumekuwa na taarifa mbalimbali katika mitandao ambazo sio sahihi na kusababisha kujenga hofu kwa wagonjwa.
Dkt. Nkuba amesema kuwa ushiriki wa waandishi wa habari katika semina ni fursa kwa kuandika taarifa za lishe kwa uweledi kwa ajili kuelimisha jamii kuhusu ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha.