Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima,akisoma Tamko kwa waandishi wa habari leo Juni 9,2021 jijini Dodoma kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo Kitaifa yatafanyika mkoani Dodoma. Kushoto ni Naibu Waziri, Mwanaidi Ali Khamisi.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima,akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari leo Juni 9,2021 jijini Dodoma kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo Kitaifa yatafanyika mkoani Dodoma.
Baadhi ya Waandishi wa habari wakimsikiliza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima,(hayupo pichani) leo Juni 9,2021 jijini Dodoma wakati akizungumzia Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo Kitaifa yatafanyika mkoani Dodoma.
Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Naftali Ng’ondi akifafanua jambo kwa waandishi wa habari mara baada ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima,kutoa tamko leo Juni 9,2021 jijini Dodoma kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo Kitaifa yatafanyika mkoani Dodoma.
………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
KUELEKEA siku ya mtoto wa Afrika June 16 mwaka huu,Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima,amesema kuwa jukumu la kuwalea na kuwalinda watoto ni la familia na jamii kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa na Dkt.Gwajima leo June 9,2021 jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari,kuhusu maadhimisho hayo,ambayo yataenda sambamba na uzinduzi wa Makao ya Taifa watoto katika eneo la Kikombo
Dk. Gwajima amesema wanapoadhimisha siku hiyo,Serikali kupitia Wizara ya Afya –Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii itafanya Uzinduzi wa Makao ya Taifa ya Watoto yaliyopo Kikombo mkoani Dodoma kama shughuli kubwa ya kitaifa ya maadhimisho hayo.
Aidha amesema kuwa uzinduzi huo unatarajiwa kufanywa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Philip Mpango.
Waziri Gwajima amesema kuwa mradi wa ujenzi wa Makao ya Taifa ya Watoto umetekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali kupitia Wizara ya Afya, Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na Shirika la ABBOTT Fund Tanzania.
“Ifahamike kuwa makao ni mahali ambapo mtoto hupelekwa kupata huduma kwa muda maalum na Uamuzi wa kumpeleka mtoto kwenye makao iwe ni hatua ya mwisho baada ya njia nyingine zote za kumsaidia kushindikana,”amesema Gwajima.
Pia Waziri Gwajima amesisitiza kuwa jukumu la kuwalea na kuwalinda watoto ni la familia na jamii kwa ujumla.
“Napenda kutoa rai kwa jamii na familia kuwa jukumu la kuwalea na kuwalinda watoto ni la familia na jamii kwa ujumla,”amesisitiza
Amesema katika kuimarisha ulinzi kwa watoto Serikali na wadau imeendelea kuratibu mifumo ya msaada ya kutolea taarifa ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto kupitia simu ya bure Na 116 ambapo idadi ya taarifa zilizopokelewa kupitia simu imeongezeka kutoka simu 1,010,186 mwaka 2013 hadi simu 14,624 zilizopigwa mwaka 2020.
Pia,amesema jumla wa watoto 6,877 walipatiwa huduma mbalimbali baada ya taarifa zao kupitia simu ya 116 kufikishwa kwa mamlaka husika ukilinganisha na watoto 493 waliosaidiwa mwaka 2013.
Dk.Gwajima amesisitiza kuwa Serikali imeendelea kuimarisha mifumo mingine ikiwemo uanzishaji wa kamati za ulinzi kwa wanawake na watoto ambapo hadi Disemba, 2020 jumla ya Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto 16,343 zimeanzishwa katika Halmashauri 184 kwenye Mikoa yote 26.
Aidha, Dawati la Jinsia na Watoto katika vituo 420 vya Polisi nchini na vituo vya huduma ya mkono kwa mkono 13 katika mikoa 10 na nyumba salama 9 zimeanzishwa katika mikoa 7 ya Tanzania bara.
Pia, amesema katika kuimarisha malezi ya familia, Serikali imeendelea kushughulikia mashauri na matunzo ya watoto ambapo jumla ya mashauri 27,806 katika kipindi cha mwaka 2019/2020.
Aidha, idadi ya watoto wanaopata malezi ya kambo imeongezeka kutoka watoto 85 mwaka 2015 hadi watoto 342 mwaka 2020.
Amesema kuwa Serikali pia imeendelea kuratibu vituo vya kulelea watoto wadogo mchana ambapo vituo hivyo vimeongezeka kutoka vituo 744 mwaka 2015 hadi kufikia vituo 1,543 mwaka 2020.
Dk.Gwajima ameeleza kuwa V Serikali imeendelea kuratibu makao ya watoto walio katika mazingira hatarishi na hadi Disemba, 2020 jumla ya makao ya watoto 178 yamesajiliwa na watoto 351 wanalelewa katika makao hayo.
Amesema pamoja na juhudi hizo Serikali imeendelea kutoa elimu kuhusu malezi chanya kwa Jamii kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii ambapo hadi kufikia Disemba, 2020 jumla ya Maafisa Maendeleo ya Jamii 7,445 walipata mafunzo na wazazi 110,805.
Aidha, maafisa hao wamefanikiwa kuanzisha jumla ya vikundi 3,963 vya kuhamasisha na uelimisha malezi chanya katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuendeleza elimu ya malezi na kukuza uwajibikaji kwa wazazi na walezi katika familia.
Amesema,Serikali imeendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zinazohusu Haki jinai ya mtoto katika vyombo vya sheria. Mwaka 2020 Serikali iliandaa Mkakati wa Taifa wa Haki Jinai ya Mtoto (2020/21 – 2024/25) wenye lengo la kuwezesha Afua zitakazosaidia kulinda haki za mtoto katika mifumo ya kisheria.
Pia Serikali imeongezeka idadi ya mahakama zinashughulikia mashauri ya watoto kutoka 3 mwaka 2015 hadi mahakama 141 mwaka 2020 kwa ajili ya kufikisha huduma za mahakama ya mtoto jirani na walengwa.
Aidha,amesema shughuli nyingine ambazo Wizara itashiriki kuzifanya kuelekea kilele cha maadhimisho haya ni uzinduzi wa ujenzi wa vituo vya kijamii vya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya watoto na uzinduzi wa baraza la watoto la Taifa.
“Pia kutakuwa na jumbe maalum zilizoandailiwa kwa ajili ya kampeni ya kuelimisha jamii kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya watoto kupitia njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari, viongozi, wa dini na makundi mengine maarufu yanaweza kufikisha taarifa kwa jamii,”amesema.