Mratibu wa mradi wa USAID Boresha Afya Manyara, Dk Ibrahim Simiyu (kushoto) na Afisa takwimu na ufuatiliaji Mkoani Manyara, Phillip Mwanga wakiwa kwenye kikao kazi hicho.
Baadhi ya wauguzi waliohudhuria kikao kazi hicho cha kujengewa uwezo kupitia mradi wa USAID Boresha Afya Manyara, kilichofanyika Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro.
…………………………………………………………………
Na.Gift Thadey, Simanjiro
MADAKTARI na wauguzi 48 wa Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wamejengewa uwezo zaidi katika kutoa huduma kwa wagonjwa wenye maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Mratibu wa mradi wa USAID Boresha Afya Manyara, Dk Ibrahim Simiyu amesema wataalamu hao wa afya, wamejengewa uwezo huo kwa muda wa siku tatu kwenye ukumbi wa Mazubu Grand Hotel Mji mdogo wa Mirerani.
Dk Simiyu amesema wataalamu hao wa afya wamejengewa uwezo kwa ufadhili wa shirika la Elizabeth Glaser Pediatric Aids Foundation (EGPAF).
Amesema mradi huo kwenye mkoa wa Manyara unasaidia Serikali kupeleka huduma kwa watu waliobainika kupata maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi.
Amesema ili kuweza kuboresha utoaji huduma wamewajengea uwezo wataalamu hao kwa muda wa siku tatu kwenye mji mdogo wa Mirerani.
“Ili kuweza kutoa huduma zaidi kwa wahitaji wetu tumefanikisha kuwaongezea uwezo zaidi wataalamu wetu na kuwapa uzoefu zaidi katika sekta hii,” amesema Dk Simiyu.
Amesema pia wamepokea taarifa ya maendeleo ya utoaji huduma za VVU kutoka katika vituo mbalimbali vya Wilaya ya Simanjiro na kuangalia sehemu ambazo zinahitaji kupatiwa maboresha kwa wahusika.
Afisa takwimu na ufuatiliaji wa mradi wa USAID Boresha Afya Mkoa wa Manyara, Phillip Mwanga amesema kwenye wilaya ya Simanjiro mradi huo unahudumia jumla ya watu 2,712 kwenye vituo 25.
Mwanga amesema katika kikao kazi hicho cha kujengeana uwezo, wataalamu hao wa afya waliwasilisha taarifa zao za mwezi Januari hadi Machi.