Dodoma, 08 Juni 2021
Tanzania imechaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Mkutano wa 76 wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA 76) katika uchaguzi uliofanyika tarehe 7 Juni 2021, New York – Marekani.
Katika uchaguzi huo, Tanzania imepita bila kupingwa ambapo mara ya mwisho Tanzania kuwa Makamu wa Rais ni mwaka 1991.
Katika uchaguzi huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Maldives, Mhe. Abdulla Shahid, amechaguliwa kuwa Rais wa Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA 76) kwa kura 143 dhidi ya mpinzani wake Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Afghanistan Dkt. Zalmai Rassoul aliyepata kura 48.
Majukumu ya Makamu wa Rais ni kusaidiana na Rais katika kuratibu na kusimamia shughuli za mijadala ya UNGA na kamati zake katika kutunga maazimio. Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ndio chombo kikuu cha kutunga Sera na Sheria chenye uwakilishi wa nchi zote wanachama ambapo mkutano wa mwaka huu unatarajiwa kufanyika mwezi Septemba 2021.
Tanzania iliwahi kuwa Rais wa UNGA mwaka 1979 katika mkutano wa 34 wakati wa uwakilishi wa Balozi Dkt. Salim Ahmed Salim.
Katika uchaguzi huo pia, Tanzania imeshinda nafasi ya Mjumbe wa Baraza la Uchumi na Jamii la Umoja wa Mataifa (Economic and Social Council (ECOSOC) kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 1 Januari 2022 hadi 31 Desemba 2024. Katika uchaguzi huo, Tanzania imepata kura 182 kati ya 186 zilizopigwa na nchi wanachama 54 wanaounda Umoja huo.
Hii ni mara ya tano kwa Tanzania kushika nafasi hiyo ambapo mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2004 – 2006. Mara nyingine ilikuwa ni 1966 – 1969; 1978 – 1980; na 1994 – 1996.
ECOSOC ndio chombo kinachohusika na miradi ya maendeleo ya kiuchumi ya Umoja wa Mataifa hasa katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu ya 2030, na pia husimamia mashirika yaliyo chini ya Umoja wa Mataifa (Specialized Agencies and Commissions) kama UNDP, UNFPA na UNICEF.
Ushiriki wa Tanzana katika uongozi wa vyombo vya Umoja wa Mataifa unaipa nchi nafasi nzuri kutekeleza sera yake ya Mambo ya Nje na pia kuchangia utekelezaji wa majukumu yake kama mwanachama wa Umoja wa Mataifa.
Kuchaguliwa kwa Tanzania chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ni ishara ya kuaminika katika medani za kimataifa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.