Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza katika kikao chake na Watendaji Wakuu wa kampuni za simu kilichofanyika jijini Dodoma. Kulia ni Naibu wake Mhandisi Kundo Mathew.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile na Naibu wake Mhandisi Kundo Mathew wakiteta jambo katika kikao chake na Watendaji Wakuu wa kampuni za simu kilichofanyika jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew akizungumza katika kikao cha kikao cha Waziri wake Dkt. Faustine Ndugulile (katikati) na Watendaji Wakuu wa kampuni za simu kilichofanyika jijini Dodoma. Wa kwanza kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Justina Mashiba.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile(wa pili kulia) akizungumza katika kikao chake na Watendaji Wakuu wa kampuni za simu kilichofanyika jijini Dodoma. Wa pili kulia ni Naibu wake Mhandisi Kundo Mathew, kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Justina Mashiba na kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano wa Wizara hiyo Edith Turuka
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile(wa pili kushoto) akizungumza katika kikao chake na Watendaji Wakuu wa kampuni za simu kilichofanyika jijini Dodoma.
Baadhi ya wajumbe wa kikao cha Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile (hayupo pichani) na Watendaji Wakuu wa kampuni za simu kilichofanyika jijini Dodoma wakifuatilia kikao hicho.
Baadhi ya wajumbe wa kikao cha Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile (hayupo pichani) na Watendaji Wakuu wa kampuni za simu kilichofanyika jijini Dodoma wakifuatilia kikao hicho.
……………………………………………………………………..
Na Faraja Mpina, Dodoma
Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) inatarajia kutangaza zabuni ya awamu ya sita yenye lengo la kupeleka mawasiliano katika kata 179 zenye vijiji 358 mradi unaolenga kupunguza changamoto ya mawasiliano kwa wananchi waishio mipakani.
Akizungumza katika kikao chake na watendaji wakuu wa makampuni ya simu kilichofanyika jijini Dodoma tarehe 07/6/2021 Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amesema Mfuko huo utatangaza zabuni hizo mwezi huu kwa lengo la kuendelea kuboresha huduma za mawasiliano nchini
“Kama Serikali tumejielekeza katika kuboresha mawasiliano ya mipakani ambayo yanakuwa na mwingiliano na nchi za jirani, makampuni ya simu mkiwa kama wadau wa Sekta hii tunaomba mtoe ushirikiano kwa Serikali ili wananchi waishio mipakani wapate mawasiliano ya uhakika ya ndani ya nchi”, alisema Dkt. Ndugulile
Katika hatua nyingine Dkt. Ndugulile ametoa rai kwa watendaji hao kufanya maboresho ya utoaji wa huduma za mawasiliano kwa kufanyia kazi maeneo ambayo wananchi wanayalalamikia ikiwa ni pamoja na kuhakiki namba zilizosajiliwa kwa alama za vidole na kuimarisha mifumo ya usajili wa laini za simu pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa umma ili kupunguza utapeli kwa njia ya simu za mkononi.
Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amesema Serikali ipo tayari kushirikiana na watoa huduma pamoja na watumiaji wa huduma za mawasiliano ili kuweza kutambua mahitaji halisi na changamoto zilizopo katika sekta hiyo na kuzitatua kwa lengo la kuendelea kuboresha Sekta hiyo muhimu nchini kwa kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma za mawasiliano popote alipo.
Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba amesema kuwa lengo la Mfuko huo ni kupeleka mawasiliano kwa wote na zabuni zitakazotangazwa mwezi huu ni kwa ajili ya kupeleka mawasiliano katika maeneo ya mipakani na kuyaomba makampuni ya simu kuchukulia zabuni hizo kwa uzito stahiki pindi zitakapotangazwa.