………………………………………………….
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka ameahidi kukutana na uongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kujadili namna ya kuwawezesha Wafugaji wa Mkoa wa Dodoma kunufaika na shamba la Mifugo la Serikali lililopo Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma (Kongwa Ranch).
Kauli hiyo ameisema jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa Wafugaji wa Mkoa wa Dodoma.
Mhe. Mtaka amesema atazungumza na Wizara ya Mifugo ili wawapatie Wakulima wa Dodoma, vitalu vya ardhi kwenye shamba hilo la Mifugo la Serikali lenye ukubwa wa Hekta 38,000 (sawa na Ekari 95,000) kwa utaratibu wa kukodisha ili Wakulima hao waweze kupata maeneo ya kutosha ya kuendeshea shughuli za ufugaji wa kisasa na uoteshaji malisho ya Mifugo.
Mhe Mtaka amesema kuwa, kipaumbele chake katika sekta ya ufugaji kwenye Mkoa wa Dodoma ni kuendesha ufugaji bora, wakisasa, wenye tija na uwekezaji wa Viwanda vya kuongeza thamani ya Mazao ya Mifugo Kama vile Nyama, Maziwa, Ngozi, Pembe na Kwato.
Awali akisoma risala ya Wafugaji, katibu wa Chama cha Wafugaji Mkoa wa Dodoma Bw. Reginaldo Lubeleje amesema kuwa baadhi ya maeneo ya ufugaji na malisho yamekuwa yakivamiwa kwa shughuli za kilimo.
Aidha, Wakulima bado wana ukosefu wa Elimu ya Kutosha ya ufugaji bora na kuongeza kuwa kwa hapa Dodoma lipo shamba kubwa la Mifugo la Serikali Wilayani Kongwa (Kongwa Ranch) lakini halina mchango katika kuwasaidia tija Wakulima wa Dodoma na kubadili aina ya ufugaji wao kuwa ufugaji bora na wakisasa.