Katibu Tawala wa Wilaya ya Mkalama akitoa utambulisho wa watumishi kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Mahenge.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, James Mkwega, akizungumza kwenye kikao hicho.
Baadhi ya watumishi na watendaji wa Wilaya ya Mkalama wakiwa wamejipanga kumpokea Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Mahenge wakati wa ziara hiyo.
Wimbo wa Taifa ukiimbwa.
Madiwani wa halmashauri hiyo wakijitambulisha kwa mkuu wa mkoa.
Wajumbe wa Kamati ya Siasa wa wilaya hiyo wakiwa kwenye kikao hicho.
Kikao kikiendelea.
Dkt.Mahenge akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhandis Masaka funguo ya gari la wagonjwa (Ambulance) lililotolewa na Serikali kupitia wadau wa maendeleo.
Na Dotto Mwaibale, Mkalama
MKUU wa Mkoa wa Singida, Dkt. Binilith Mahenge amewataka watendaji na watumishi wote mkoani hapa kuhakikisha kila mmoja kwa nafasi yake anawajibika ipasavyo hasa kwenye ajenda ya ukusanyaji mapato ya ndani, ongezeko la uzalishaji wa zao la alizeti na maboresho kwenye viwango vya ufaulu.
Akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kuhamasisha na kukagua miradi ya maendeleo ndani ya Wilaya ya Mkalama mkoani hapa jana, pamoja na kuomba ushirikiano-Dkt Mahenge alisisitiza kuwa anataka kila chanzo cha mapato ndani ya halmashauri kichangie asilimia 100 kwa usimamizi wake.
Aidha, alihamasisha sekta ya kilimo kujipanga vilivyo kwenye eneo la kilimo hususani kilimo cha alizeti, ili kuufanya mkoa wa Singida kuwa suluhisho la mahitaji ya upatikanaji wa kutosha wa mafuta ya kula ambayo yanatumia fedha nyingi kuagizwa kutoka nje.
“Nguvu kubwa tutaelekeza kuhakikisha kila chanzo kinachangia kwa asilimia mia moja kwa usimamizi wake, na katika hili sihitaji sababu yoyote kutoka kwa yeyote…na suala hili linamuhitaji kila mtumishi. Ni lazima tukubali mabadiliko,” alisema Mkuu wa Mkoa na kuongeza;
“Pia Singida tuna fursa ya kipekee na hali ya hewa nzuri kutuwezesha kuwa namba moja kwenye uzalishaji wa mazao mengi ikiwemo alizeti, ninahitaji mabadiliko na ushirikiano mkubwa toka kwenu kwenye kuinua uzalishaji wa zao hili.”
Kuhusu Bima ya Afya, aliagiza uhamasishaji mkubwa ufanyike ili kila mwananchi wa Singida aweze kuona umuhimu na kupata ‘Kadi ya Bima’ ambayo gharama yake ni shilingi elfu 30 ili kuwezesha unafuu wa kupata huduma za matibabu.
Aidha, aliwaagiza wakurugenzi na watendaji wa Halmashauri zote ndani ya mkoa kuhakikisha wanatenga asilimia 10 ya mapato yake kama takwa la kisheria na sio hiari kwa ajili ya kutumika kwenye kuwakopesha vijana, wanawake na wenye ulemavu.
Katika hatua nyingine akiwa wilayani hapo Dkt. Mahenge alifanya ziara ya kukagua na kuangalia maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mkalama na kupata fursa ya kuzungumza na wauguzi, wagonjwa na wananchi kuhusu hali ya upatikanaji wa huduma, sambamba na kumtaka mkandarasi wa majengo hayo kuharakisha umaliziaji wa miundombinu ya majengo hayo ili huduma ziendelee.
Aidha, alipata fursa ya kukabidhi gari ya wagonjwa (Ambulance) iliyotolewa na Serikali kwa kushirikiana na Global Fund kwa ajili ya huduma za dharula kwenye hospitali hiyo, huku akiagiza chombo hicho kutumika kwa huduma stahiki na si vinginevyo.
Pamoja na mambo mengine, alipata fursa ya kutembelea ujenzi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya hata hivyo alionyesha kutokuridhishwa na kasi ya ujenzi wake na kumtaka mkandarasi kuharakisha jengo hilo kutokana na umuhimu wake kwa ustawi wa maendeleo.
Pia katika kukagua mwenendo wa ukusanyaji mapato na baadhi ya vyanzo vyake, Dkt. Mahenge alifanya ziara ya kushtukiza kwenye moja ya Mnada maarufu kwenye kijiji cha Hilamoto wilayani hapo na kubaini idadi kubwa hawana vitambulisho vya ujasiriamali wala nyaraka za malipo stahiki ya ushuru, na kuwaagiza watendaji wanaohusika kuhakikisha wanaanza kushughulikia suala hilo ili kunusuru upotevu huo. wa mapato.