Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wanawake wa Tanzania katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Convention Center Jijini Dodoma leo tarehe 8 June, 2021.
……………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka Wanawake wote nchini kutojiona wanyonge kwani wao ni Jeshi kubwa na lenye nguvu.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Juni 8,2021 jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na Wanawake wa Mkoa wa Dodoma kwa niaba ya Wanawake wote nchini katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete.
“Wanawake sio viumbe dhaifu ni Watu imara na wenye nguvu kama binadamu wengine na pengine Wanawake wana nguvu zaidi, tuna nguvu za kisaikolojia tunabeba mengi, na tuna nguvu kwenye mioyo yetu tunastahimili mengi kwenye vifua vyetu”amesema Rais Samia
Rais Samia amesema kuwa serikali itaendelea kuongeza fursa za wanawake kupata ajira ikiwa ni pamoja na kubuni mikakati ya kuwaongezea ujuzi.
‘’Naihamasisha sekta binafsi kuingia katika kuongezea ujuzi wanachangia sana kwenye ile tozo ya uendelezaji ujuzi na ndiyo inasaidia kujega vyuo vya veta ili wanawake zaidi waingie wapate ujuzi na wakatumike kwenye mashirika yao’’
Wakati huo huo Rais Samia amesema hatua kubwa imepigwa katika kuelekea uwiano wa kijinsia kwenye eneo la elimu ambapo kwa sasa uwiano kati ya wavulana na wasichana kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu unakaribiana.
Hata hivyo Rais Samia amesema wanawake wamekuwa na mchango mkubwa katika shughuli za kimaendeleo na hakuna taifa linaloweza kupiga hatua bila ya kumtegemea mwanamke.
Pia amewaahidi Wanawake hao kuwa Serikali yake itahakikisha kuwa hadi kufikia mwaka 2025 itakua imetekeleza ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020 na upelekaji wa Maji utakua umekamilika kwa asilimia 95 kwa maeneo ya mjini na asilimia 85 vijijini.
” Niwahakikishie hapa kuwa utekelezaji wa Ilani tutaufikia kwa kiwango kikubwa, Kwenye eneo la umeme tunaendelea nalo kwa kasi kubwa na vijiji vilivyobakia mpaka 2024 vitakua tayari na kazi itakayokua imebakia ni kusambaza.
Niwaombe Wanawake wa Tanzania tunapokwenda kukamilisha upelekaji wa umeme vijijini ifikapo mwaka 2024 basi tutumie umeme huo katika kujinufaisha kiuchumia,” Amesema Rais Samia.
Kuhusu mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwenye Halmashauri nchini kwa makundi maalum wakiwemo Wanawake, Rais Samia amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Ummy Mwalimu kuhakikisha anafuatilia malalamiko yanayotolewa kuhusu upendeleo wa upatikanaji wa mikopo hiyo ili vikundi vyenye sifa viweze kupata mikopo hiyo na kunufaika nayo.
Ameiagiza Mikoa, Wilaya na Halmashauri zote nchini kuendelea kuyatunza majukwaa ya wanawake kiuchumi ambapo ametolea msisitizo kwenye utunzaji wake kwani ana mpango mkamilifu wa kuyalea majukwaa hayo yeye mwenyewe.
Rais Samia pia ameahidi kuendeleza usawa wa kijinsia na ndio maana amekua akiteua wanawake katika nafasi mbalimbali za uteuzi ambazo amekua akizifanya tokea ateuliwe kuwa Rais.
” Nimeongeza Wanawake kwenye teuzi, upande wa Makatibu Tawala hapa nimefanya vizuri zaidi na sijui kama kuna eneo nitafanya vizuri zaidi ya hapo, kati ya Makatibu Tawala 26 Wanawake ni 12 hii ni sawa na 46%, labda uteuzi wa pili utakuwa 50 kwa 50.
Mahakamani tuliteua Majaji 28 na kati yao Majaji 12 au 13 ni Wanawake sawa na asilimia 43%, hii inamaanisha 50 kwa 50 haiko mbali, kwa sasa Mahakama Kuu Majaji Wanawake ni 40 kati ya 86.
Bungeni tuna Naibu Spika Mwanamke Dr. Tulia, Wabunge Wanawake idadi imeongezeka, nimemteua Katibu wa Bunge Mwanamke kwa mara ya kwanza katika historia ya Nchi yetu, kwenye miaka michache ijayo tunaweza kufika au kukaribia sana usawa wa kijinsia,” Amesema Rais Samia.
Kwa upande wa Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt Dorothy Gwajima amesema Jitahada za wanawake zimekuwa zikiathiriwa na changamoto mbalimbali hivyo ameahidi na wasaidizi wake kuwa wako tayari kushughulikia changamoto zinazowakabili wananawake.
Mkutano wa Rais Samia na Wanawake wa Dodoma ni mkutano wa pili kwa Rais kukutana na makundi mbalimbali nchini ambapo awali alikutana na Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam umeenda saambamba na kauli mbiu isemayo ‘’ Mwanamke ni Nguzo ya Mandeleo ,Tujitambua ,tujidhatiti ,tutekeleze wajibu wetu