************************************
Nteghenjwa Hosseah, Mtwara
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa(Mb) ameelekeza ufundishaji wa somo la Michezo uimarishwe kuanzia shule ya awali, msingi, sekondari na vyuo ili kujenga hali ya kujiamini na kuwa mahiri kimwili na kiakili.
Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa ameyasema hayo leo wakati akifungua mashindano ya michezo na taaluma yajulikanayo kama UMISSETA na UMITASHUMTA yaliyofanyika kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona Mkoani Mtwara.
Ameeleza michezo ni muhimu zaidi kwa makuzi na maendeleo ya taaluma ya watoto na vijana na ina mchango mkubwa katika kuimarisha afya ya mwili na akili.
“Watafiti wamethibitisha kuwa michezo kwa madarasa ya awali kwa maana ya miaka 3 – 6 ni muhimu zaidi katika kuongeza uwezo wa mzunguko wa damu katika ubongo (kuongezeka kwa mishipa ya damu) na maendeleo ya afya na makuzi ya watoto kwa ujumla wake hivyo ni vyema tukajikita kumjenga mtoto huyu kuanzia kwenye Ngazi ya awali,”amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Ameongeza “Bila shaka sote tunaelewa kuwa binadamu hawezi kuwa na akili bora kwenye mwili dhaifu na Afya Bora inaweza kujengwa vizuri zaidi kwa kushiriki katika michezo hivyo tujikite katika kutengeneza vizazi vitavyokua na mahiri kwenye michezo wakati wote maisha yao.”
Majaliwa alibainisha kuwa katika siku za hivi za karibuni kumekuwepo na mafanikio makubwa ya vijana waliyoyapata kupitia Michezo na wengi ni wa hapa hapa Tanzania, kama vile Mbwana Samata.
“Kwa hawa wachache wanatuonyesha picha kubwa ya namna ambavyo vijana wetu wengi wanaweza kufanikiwa kupitia michezo na sanaa tuongeze nguvu katika eneo hili,”amesema
Aidha amesema Michezo na Sanaa vikiwekewa mipango sahihi vina nafasi kubwa ya kuchangia na kujenga uchumi endelevu wa Taifa na watu wake.
“Sekta hizi ni fursa kubwa kwa vijana wetu kujiajiri, kuajirika na kuutambulisha utamaduni wetu ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu,”amesema.
Amewataka wanafunzi wote wanaoshiriki katika mashindano hayo kutokuridhika na hatua waliyofikia kwenye mashindano hayo na yawe mwanzo wa kujiimarisha katika michezo na sanaa ili kulitangaza Taifa kupitia michezo na sanaa.
“Matarajio ya wengi ni kuona mkionyesha uwezo wenu kwa nidhamu ya hali ya juu na kuiletea mafanikio mikoa yenu na taifa kwa jumla,”amesema.
Amezitaka Wizara zinazohusika kurudisha mafunzo ya michezo katika vyuo vya Butimba na Mtwara ili kufundisha walimu watakaoweza kuwapa wanafunzi mafunzo sahihi ya michezo.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa, amesema wanakusudia kuanzisha Vituo vya kulea vipaji katika shule mbalimbali ili kuhakikisha kuwa vipaji vya watoto vinaendelezwa kuanzia umri mdogo.
Naye, Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI,Mhe. Davidi Silinde ameelezea malengo ya mashindano hayo kuwa ni kujenga umoja wa kitaifa, mshikamano na upendo baina ya wanafunzi wangali katika umri mdogo , Kuimarisha Taaluma ya Michezo kwa wanafunzi ili kuwajengea ujuzi na maarifa na kuwa mahiri wanapoendelea kukua pamoja na Kujenga umoja, uzalendo na mshikamano miongoni mwa wanafunzi, walimu na wadau wa michezo nchini.
Pia ameongeza kuwa mashindano hayo yatawajengea watoto Ukakamavu na umahiri katika michezo pamoja na kuibua na kuendeleza vipaji vya wanafunzi wangali bado wachanga na kujenga dhana ya uvumilivu na ustahimilivu.
Mashindano hayo yamebeba kauli mbiu ya Michezo, Sanaa na Taaluma kwa maendeleo ya viwanda na jumla ya wanamichezo 3600 kutoka mikoa 26 watashiriki kwenye michezo ya UMITASHUMTA na wanamichezo 3800 kutoka katika mikoa 28 ya Tanzania bara na visiwani watashiriki katika michezo ya UMISSETA, mashindano hayo yatafungwa Julai 4, 2021.