Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Dkt.Faustine Ndugulile,akizungumza kwenye kikao na wawakilishi wa makampuni ya simu nchini kilichoandaliwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) uliokuwa na lengo la kujadiliana namna bora ya
kupeleka mawasiliano katika maeneo mbalimbali kilichofanyika leo Juni 7,2021 jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew,akizungumza wakati wa kikao na wawakilishi wa makampuni ya simu nchini kilichoandaliwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) uliokuwa na lengo la kujadiliana namna bora ya kupeleka mawasiliano katika maeneo mbalimbali kilichofanyika leo Juni 7,2021 jijini Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote,(UCSAF) Justina Mashiba ,akizungumza wakati wa kikao na wawakilishi wa makampuni ya simu nchini kilichoandaliwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) uliokuwa na lengo la kujadiliana namna bora ya kupeleka mawasiliano katika maeneo mbalimbali kilichofanyika leo Juni 7,2021 jijini Dodoma.
Baadhi ya watendaji wa Makampuni wakifatilia hotuba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Dkt.Faustine Ndugulile,(hayupo pichani) wakati na wawakilishi wa makampuni ya simu nchini kilichoandaliwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) uliokuwa na lengo la kujadiliana namna bora ya kupeleka mawasiliano katika maeneo mbalimbali kilichofanyika leo Juni 7,2021 jijini Dodoma.
……………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Dkt.Faustine Ndugulile ameyataka makampuni ya simu nchini kuboresha huduma wanazotoa kwa wateja pamoja na kushughulikia changamoto ya matumizi sahihi ya vifurushi pamoja na kukomesha tabia ya baadhi ya wafanyakazi wa makampuni hayo kuvujisha siri za wateja wao.
Akizungumza leo Juni 7,2021 Jijini Dodoma,katika kikao chake na wawakilishi wa
makampuni hayo,ambacho kilikuwa na lengo la kujadiliana namna bora ya
kupeleka mawasiliano katika maeneo ambayo hayana mawasiliano,kilichoandaliwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)Waziri Ndugulile amesema makampuni hayo yanatakiwa kuboresha huduma kwa wateja kwani kumekuwa na changamoto katika matunzi ya vifurushi kuisha kabla ya muda.
Dkt.Ndugulile amesema kuwa wanataka kuona makampuni hayo yanafanya maboresho kwa kuhakikisha wanashughulikia changamoto hiyo ikiwa ni pamoja na kulinda
siri za wateja pamoja na kuweka mfumo imara wa kusajili namba.
Vilevile ameyataka makampuni hayo kuweka mfumo mzuri kwa mawakala kwani baadhi wamekuwa sio waaminifu kwani serikali ilitaka kuwafutilia mbali lakini iliona hakuna haja kutokana na kutoa ajira zaidi ya watu 50,000.
Hata hivyo,Dkt.Ndugulile amesema serikali itaendelea kutoa ruzuku kwa makampuni hayo ili maeneo ya mipakani mwa nchi yaweze kufikiwa na mawasiliano.
Pia,Waziri huyo amewapa angalizo watendaji hao kuwa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ni mali ya Serikali hivyo ujenzi, upanuzi na uendelezaji wake upo chini ya Serikali na sio makampuni ya simu kufanya ujenzi wowote wa Mkongo wa Mawasiliano.
Aidha, Dkt. Ndugulile ametumia kikao hicho kuyaalika makampuni ya simu kushiriki katika zabuni hizo zitakazotangazwa hivi karibuni na kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kutengeneza mazingira wezeshi ya kufanya uwekezaji katika maeneo mengi zaidi nchini ili kuwafikishia wananchi huduma za mawasiliano kwasababu ni haki yao ya msingi na Wizara yake ina wajibu wa kuwafikishia wananchi huduma hiyo.
“Huduma ya mawasiliano sio anasa ni huduma ya msingi ambayo kila mwananchi anatakiwa kufikishiwa huduma hii kwa kuangalia uhitaji wake kibiashara, kiusalama, kijamii na kiuchumi”, amesema Dkt. Ndugulile.
Naye,Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasilino na Teknolojia ya Habari,Kundo Andrea amesema kwa sasa mawasiliano ni chakula hivyo kila mtanzania anahitaji kupata mawasiliano hata ambaye yupo kijijini.
Amesema ndio maana wanatoa ruzuku kwa makampuni hayo lengo likiwa kila
mtanzania aweze kupata mawasiliano huku akisisitiza serikali ipo
tayari kushirikiana na watoa huduma hao ili wananchi waweze kunufaika.
Kwa upande wake,Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote,(UCSAF)
Justina Mashiba amesema lengo la kikao hicho ni kuangalia namna bora ya kupeleka mawasiliano maeneo ambayo hayana mawasiliano kwani lengo la mfuko huo ni kupeleka mawasiliano kwa wote.
“Watoa huduma tunahitaji kupeleka mawasiliano nchi nzima na tutatoa zabuni kuhakikisha mawasiliano yanafika mpaka katika maeneo ya vijijini,”amesema.
Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Justina Mashiba amesema kuwa anaamini makampuni ya simu wataichukulia kwa uzito stahiki zabuni hiyo pindi itakapotangazwa na Mfuko huo ili kuhakikisha huduma za mawasiliano zinafikishwa katika maeneo yenye changamoto za mawasiliano na maeneo ya mipakani ambayo yanagusa pia usalama wa nchi.
Naye Mwakilishi wa Kampuni ya simu ya Airtel Dkt. Prosper Mafole amesema kuwa amefurahishwa na ahadi ya Wizara hiyo ya kujenga kilomita 1880 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwenda katika ngazi za makao makuu ya wilaya ambapo ujenzi huo utatatua changamoto kubwa ya ufikishaji wa huduma za mawasiliano vijijini.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Vodacom Andrew Lupembe ameishukuru Wizara kwa ushirikiano inayotoa kwa makampuni ya simu na kutoa kipaumbele cha Mkongo wa Taifa ambao utajengwa katika mfumo ambao upande mmoja ukikatika upande mwingine unafikisha mawasiliano kwa wananchi.