…………………………………………………………..
Kocha msaidizi wa Timu ya KMC FC , Habibu Kondo amesema kuwa kikosi chake kinaendelea kujifua zaidi kutokana na mazoezi wanayoendelea kuyafanya ikiwa ni kujiandaa katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Dodoma Jiji utakaopigwa Juni 17 mwaka huu katika uwanja wa Jamuhuri Jijini Dodoma.
Kondo amesema kuwa bado wanaendelea na mikakati ya kujiweka vizuri sio tu katika mchezo dhidi ya Dodoma Jiji lakini pia ni kwenye maandalizi ya kuelekea kumalizika kwa michezo mitano iliyosalia hadi sasa.
Ameongeza kuwa pamoja na ushindani uliopo kwa Timu pinzani ambazo Kino Boys inakwenda kukutana nazo bado anakiamini kikosi hicho kitakwenda kufanya vizuri na hivyo kuvuna alama zote kwani malengo ya Timu ya KMC FC kwa sasa nikumaliza katika nafasi Nne za juu katika msimamo wa Ligi Kuu soka Tanzania bara.
“Tumekuwa na kipindi kirefu ambacho hatuna mechi, lakini mikakati ambayo tulijiwekea kama Timu ni kujiweka vizuri kabla ya mchezo wa Juni 17, hivyo tumecheza mechi zakirafiki, lakini pia kufanya mazoezi yenye viwango, na wiki hii tutakuwa na mechi mbili za kirafiki nyingine kabla ya mchezo wetu dhidi ya Dodoma Jiji.
KMC FC hivi sasa inaendelea na mandalizi ya michezo yake mitano ya kumalizika kwa msimu wa Ligi Kuu 2020/2021 ambayo ni dhidi ya Dodoma Jiji, Mtibwa Sugar, JKT Tanzania Simba pamoja na Ihefu.