Mkutano wa 31 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (SCMEACP) unafanyika jijini Arusha kuanzia
tarehe 7 hadi 11 Juni 2021.
Mkutano huo ambao umeanza kwa Ngazi ya Wataalam leo tarehe 7 hadi 9 Juni 2021 utafuatiwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu utakaofanyika tarehe 10 Juni 2021 na kuhitimishwa na Mkutano wa
Mawaziri utakaofanyika tarehe 11 Juni 2021.
Akifungua Mkutano wa Ngazi ya Wataalam, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughilikia Sekta za Uzalishaji na Jamii, Mhe. Christophe Bazivamo amezipongeza Nchi Wanachama
kwa kufufua viwanda vidogo na kutumia bidhaa za ndani hususan katika kipindi hiki cha janga la ugonjwa wa Corona ambalo limeathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za uzalishaji na ufanyaji biashara katika nchi nyingi duniani zikiwemo zile za EAC.
Ameongeza kusema kuwa, ugonjwa wa Corona umetoa funzo kubwa kwa Nchi Wanachama wa EAC kwamba zinaweza kufanya
biashara miongoni mwao na kujitosheleza kwa mahitaji mbalimbali ya msingi kwa maendeleo ya wananchi wa nchi hizo ikiwa ni utekelezaji wa Itifaki mojawapo muhimu ya Jumuiya ya Soko la Pamoja.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mkutano huo wa Ngazi ya Wataalam, Bi. Alice Yalla kutoka Jamhuri ya Kenya amesisitiza wajumbe kujadili kwa umakini agenda mbalimbali zilizopo mbele yao na kutoa mapendekezo yenye tija, ikizingatiwa kuwa Sekta ya Mipango ni moja ya Sekta muhimu katika Jumuiya ambayo pamoja na mambo mengine pia hushughulika na tathmini ya mipango na masuala yote yanayotekelezwa na Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Mkutano wa Wataalam pia utapitia agenda mbalimbali muhimu ambazo zitawasilishwa kwenye Mkutano ngazi ya Makatibu Wakuu utakaofanyika tarehe 9 na 10 Juni 2021 kwa majadiliano na hatimaye agenda hizo zitawasilishwa kwenye Mkutano ngazi ya
Mawaziri unaotarajiwa kufanyika jijini hapa tarehe 11 Juni 2021.
Miongoni mwa agenda hizo ni pamoja na Taarifa ya Utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa kwenye vikao vilivyopita; Taarifa kuhusu hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki; Kupitia maelekezo ya Baraza la Mawaziri kuhusu Rasimu ya Maboresho ya Utaratibu wa Mafao katika Jumuiya ya Afrika Mashariki; Taarifa kuhusu ombi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo la kujiunga na EAC; Taarifa kuhusu hatua
iliyofikiwa ya utatu wa Jumuiya za EAC-COMESA-SADC katika Eneo Huru la Biashara
Barani Afrika; Taarifa ya Uchangiaji wa Bajeti ya EAC kutoka Nchi Wanachama; na
Taarifa ya majadiliano kuhusu Eneo Huru la Biashara Barani Afrika.
Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano
wa Ngazi ya Wataalam unaongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na
Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Balozi Stephen Mbundi. Kadhalika Mkutano huo umehudhuriwa na Wajumbe kutoka
nchi zote wanachama ambazo ni Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini.
Mkurugenzi katika Wizara ya Afrika Mashariki na Maendeleo ya Kikanda ya Kenya na Mwenyekiti wa Mkutano wa Ngazi ya Wataalam, Bi. Alice Yalla akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo uliofanyika jijini Arusha ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa 31 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta linaloshughulikia masuala ya Afrika Masahriki na Mipango katika Jumuiya ya Afrika Mashariki unaotarajiwa kufanyika tarehe 11 Juni 2021. |
Ujumbe wa Kenya ukiwa kwenye mkutano wa ngazi ya wataalam |
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania ukishiriki Mkutano wa ngazi ya wataalam |
Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bibi Agnela Nyoni akifuatilia ufunguzi wa mkutano wa wataalam uliofanyika Arusha kwa ajili ya kuandaa Mkutano wa 31 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta linaloshughulikia masuala ya Afrika Masahriki na Mipango katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unaotarajiwa kufanyika tarehe 11 Juni 2021. |
Ujumbe wa Uganda ukiwa kwenye mkutano wa ngazi ya wataalam |
Balozi Mteule na Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bibi Caroline Chipeta akifuatilia mkutano wa ngazi ya wataalam uliofanyika Arusha ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa 31 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta linaloshughulikia masuala ya Afrika Masahriki na Mipango katika Jumuiya ya Afrika Mashariki unaotarajiwa kufanyika tarehe 11 Juni 2021. |
Ujumbe kutoka Taasisi mbalimbali za Jumuiya ya Afrika Mashariki nao ukishiriki mkutano wa ngazi ya wataalam |
Mkutano ukiendelea |
Mjumbe kutoka Rwanda akiwa kwenye mkutano wa wataalam |
Mjumbe wa Burundi naye akifuatilia mkutano |
Sehemu ya ujumbe wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ukishiriki mkutano wa wataalam |
Mkutano ukiendelea |
Mjumbe kutoka Tanzania akishiriki mkutano wa ngazi ya wataalam |
Mkutano ukiendelea |