……………………………………………………………..
KITUO michezo cha AAA Kivule Gym & Sports Promotion, kimejipanga kuinua vipaji vya michezo kwa wakazi wa Kata ya Kivule.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kivule, Dar es Salaam, jana, Mkurugenzi wa kituo hicho, Mohamed Mgonza, alisema lengo la kuanzisha kituo hicho ni kutoa fursa kwa vijana wa Kivule, kushiriki katika suala la michezo yote.
“Mji wa Kivule wengi wetu ni tumehamia kutoka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, ndiyo maana mimi na wadau wa michezo tumeamua kushirikiana kufungua kituo hichi ili kila mdau wa michezo aweze kuja kushiriki nasi na kuendeleza michezo kama ilivyo kwa maeneo mengine”, alisema.
Mgonza alisema maeneo mengi yanashiriki katika michezo lakini Kivule bado wako nyuma, ingawa kuna vipaji vingi ambavyo vinahitaji kuendelezwa.
Alisema kingine kilichotusukuma kufungua kituo hicho ni kwa sasa michezo inatoa fursa ya ajira kwa vijana, kwahiyo wanataka kuwasaidia vijana wengi wa Kivule na maeneo ya jirani kama vile Magole, Mbondole, Msongola, Majoe na Kitunda.
Mgonza alisema kituo hicho kinapokea mawazo na ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali na wa michezo, ikiwemo mpira wa miguu, masumbwi, riadha, sarakasi, karate, kick boxing, na michezo mingine wawasilishe mawazo yao na yatapokelewa na kufaniwa kazi.
Pia alisema kituo hicho tayari kimepata usajili wa kuandaa mashindano ya michezo mbalimbali kwahiyo wanatarajia kuandaa tamasha la wazi kwaajili ya ufunguzi kituo hicho.
Mgonza amewaomba wananchi wa Kivule na wadau wote kutoka maeneo mbalimbali waje washiriki katika kuinua vipaji vya vijana kwani michezo ni ajira pia michezo ni afya.