Wafanyabiashara wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wameifurahia kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea kutolewa wilayani humo ambapo wamesema kwamba, wamejua mambo mengi ya kodi tofauti na hapo awali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wafanyabiashara hao wameomba elimu hiyo ifanyike mara kwa mara ili kuongeza uelewa zaidi wa masuala ya kodi kwa sababu wafanyabiashara wengi huanza biashara bila kuwa na elimu ya masuala ya kodi.
“Mimi binafsi, elimu hii ya kodi imenipa kujiamini hususani katika suala zima la makadirio kwasababu nilikuwa nakwenda kukadiriwa kodi bila kuwa na uelewa wa namna TRA inavyokokoa makadirio yangu,” alisema Santos Yona ambaye ni mfanyabiashara wa vifaa vya umeme wa Kasulu mjini.
Yona ameongeza kuwa, kupitia elimu ya kodi aliyoipata, amefahamu kwamba lengo la TRA ni kutaka yeye akue kibiashara ili aendelee kuchangia zaidi kwenye maendeleo ya nchi yake.
“Kitu kingine ni kwamba, elimu ya kodi niliyoipata imenifumbua macho na kujua kumbe TRA ina lengo zuri na sisi wafanyabiashara maana wanataka tuongezeke kibiashara ili tuchangie kwenye ujenzi wa nchi yetu,” alieleza Santos.
Emakulatha Cosmas ni mfanyabiashara wa duka la vitenge mjini Kasulu ambaye ameishukuru Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kuwapatia elimu ya kodi hususani katika utunzaji wa kumbukumbu ambao ulikuwa ukimtatiza hapo awali.
“Kusema ukweli mimi nilikuwa sina elimu ya utunzaji wa kumbukumbu, ninashukuru leo nimetembelewa dukani kwangu na kupewa elimu hii ambapo sasa nimejua kwamba natakiwa kuandika manunuzi, mauzo, faida na matumizi yangu ya biashara kama nilivyoelekezwa,” alisema Emakulatha.
Naye, Kaimu Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka TRA Makao Makuu Rose Mahendeka ambaye pia ni kiongozi wa timu inayoelimisha walipakodi wilayani humo, amesema kwamba, zoezi hilo linakwenda vizuri na mwitikio wa wafanyabiashara ni mkubwa.
“Kwa kweli mwitikio wa walipakodi ni mkubwa hapa Kasulu na mpaka sasa wafanyabiashara wengi wamefika hapa ofisini kwa ajili ya kupata huduma na elimu ya kodi na wengine tumewatembelea na bado tunaendelea kuwatembelea katika maduka yao,” alisema Mahendeka.
Rose Mahendeka alieleza kuwa, katika zoezi hilo, wafanyabiashara wanaelimishwa kuhusu utunzaji wa kumbukumbu, matumizi sahihi ya mashine za EFD, kuhamasishwa kulipa kodi kwa hiari na wakati ikiwa ni pamoja na kupokea maoni na kushughulikia malalamiko yao.
Timu ya maofisa wa TRA Makao Makuu kutoka katika Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi ipo katika Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma ikiendelea na kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango.