Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akitoa maelekezo kwa Mhandisi wa Kampuni ya SINOHYDRO Corporation Limited, An Zhi Hui (kushoto) inayojenga Kiwanja cha Ndege cha Nduli mkoani Iringa, alipokagua maendeleo ya mradi huo,mkoani humo.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akimsikiliza Mhandisi kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Wenceslaus Bavuma, akimweleza maendeleo ya mradi wa Upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Nduli mkoani Iringa, wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea mradi huo, hivi karibuni.
Fundi wa Kampuni ya SINOHYDRO Corporation Limited, akiendelea na zoezi la kupima udongo katika Kiwanja cha Ndege cha Nduli mkoani Iringa. Kiwanja cha ndege hicho kinapanuliwa kwa kuongeza urefu wa barabara ya kuruka na kutua ndege,jengo la abiria, jengo la zimamoto,maegesho ya ndege,kituo cha nishati na taa.
Muonekano wa moja ya tabaka la chini la barabara ya kuruka na kutua ndege katika kiwanja cha ndege Nduli-Iringa.
********************************
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, ameutaka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) kufanya utafiti wa kwanini Wahandisi Wazawa hawakuomba kazi licha ya Mkandarasi Kampuni ya SINOHYDRO Corporation Limited kutangaza kazi kwa mradi wa upanuzi wa kiwanja cha Ndege cha Nduli mkoani, Iringa.
Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanja hicho Naibu Waziri Waitara amesema kutoshiriki kwenye miradi mikubwa ya ujenzi kunawanyima uzoefu wahandisi wazawa nchini, hali itakayosababisha kushindwa hata kufanya ukarabati baada ya mradi kukamilika.
“Kama nafasi zinatangazwa kwenye miradi na wahandisi wetu hawaombi kazi hizi, ipo haja ya kufanya utafiti kujua sababu ni ni nini, hivyo nawaagiza TANROADS kufanya utafiti kuhusu suala hili’, amesema Naibu Waziri Waitara.
Aidha, Naibu Waziri Waitara amezitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) na TANROADS kukaa pamoja ili kukubaliana namna ya kutekeleza awamu zote mbili za ujenzi kwa mara moja.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesera amesisitiza utekelezaji wa awamu zote mbili za ujenzi kwani utapunguza muda wa utekelezaji na kufanya mradi kukamilika kwa muda mfupi.
Naye Msimamizi wa Mradi kutoka TANROADS Mhandisi, Wenceslaus Bavuma, amemuhakikishia Naibu Waziri Waitara kuwa Wakala unasimamia kwa karibu mradi huo na utahakikisha viwango vyote vinazingatiwa ili mradi ukamilike kwa wakati na viwango.
Mradi wa kiwanja cha Ndege cha Nduli mkoani Iringa utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 40 na utahusisha urefushaji wa barabara ya kuruka na kutua ndege, maegesho ya ndege, jengo la muda la abiria, jengo la zima moto, jengo la kuongozea ndege, taa za barabarani na kituo cha nishati.
(Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi)