*****************************
Na Mwandishi wetu, Babati
MBUNGE wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia vyuo vikuu, Dkt Paulina Nahato amefanya uzinduzi wa safisha kitaa Mjini Babati kwa lengo la utunzaji wa mazingira yanayozunguka eneo hilo.
Uzinduzi huo umetayarishwa na kampuni ya The Show Case na kushirikisha wananchi mbalimbali wa Mjini Babati.
Dkt Nahato amewaasa vijana kujali mazingira yanawayozunguka na kujali afya zao katika kufanya shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo.
“Ukifanya shughuli zozote za kujiletea maendeleo na ili zifanikiwe unapaswa kuwa na afya ya kimwili, kiakili, kiroho, na kimahusiano,” amesema Dkt Nahato.
Ameahidi kununua mapipa madogo ya kuhifadhi taka kwenye baadhi ya maeneo ya mji wa Babati ili kuunga mkono kampeni hiyo ya safisha kitaa.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa mji wa Babati, Faustine Masunga amesema wanatarajia kujenga dampo jipya la kisasa ili kufanikisha usafi wa mazingira katika eneo hilo.
Mratibu wa The Show Case, Robin Mtasiwa amesema pamoja na kuandaa shughuli hiyo ya uzinduzi wa safisha kitaa, bila kujali faida, kuna changamoto ya vijana kutopewa nafasi japokuwa shughuli hiyo ina lenga kunufaisha jamii nzima na siyo mtu mmoja.
Katibu wa CCM Wilaya ya Babati Mjini, Fauswali Dauda amewaasa wamachinga kuwa na utaratibu wa kusafisha mazingira ili wasibughuziwe na viongozi na kuwapongeza vijana kwa shughuli hiyo na kuwaasa iwe endelevu.
Katibu wa Jumuiya ya UVCCM Wilaya ya Babati Mjini, Baraka Sultan Mipiko amesema wiki ijayo wataendeleza usafi wa mazingira kwenye eneo jingine kwa kusafisha makaburi karibu na Mahakama ya zamani.