Mkuu wa usalama barabarani Mkoa wa Arusha Mrakibu wa Polisi (SP) Solomon Mwangamilo akisisitiza jambo wakati akizungumza na waendesha bodaboda wanaofanya safari zao katikati ya Jiji katika kikao kilichofanyika mapema leo katika bwalo la Maafisa wa Polisi Arusha.
Mmoja ya waendesha bodaboda wanaotoa huduma ya kusafirisha abiria katikati ya Jiji akichangia mada katika kikao kilichohusisha waendesha bodaboda na Mkuu wa usalama barabarani Mkoa wa Arusha ambacho kimefanyika mapema leo katika bwalo la Maafisa wa Polisi Arusha.
Waendesha bodaboda wa katikati ya Jiji la Arusha wakifuatilia mada iliyokuwa inawasilishwa katika kikao kilichohusisha waendesha bodaboda na Mkuu wa usalama barabarani Mkoa wa Arusha ambacho kimefanyika mapema leo katika bwalo la Maafisa wa Polisi Arusha.
……………………………………………………………………………………….
Na Gasto Kwirine wa Polisi Arusha.
Mkuu wa usalama barabarani Mkoa wa Arusha Mrakibu wa Polisi (SP) Solomon Mwangamilo leo amekutana na kufanya kikao na waendesha bodaboda wanaofanya shughuli zao katikati ya Jiji la Arusha ambao wanajumuisha kata tatu ambazo ni Mjini kati, Levolosi na Kaloleni.
Kikao hicho ambacho kimefanyika katika bwalo la maafisa wa Polisi Arusha, mkuu huyo wa usalama barabarani amesema lengo la kikao hicho ilikua ni kuwajengea uwezo waendesha bodaboda hao kuhusiana na suala zima la utii wa sheria za usalama barabarani, kuongeza ushirikiano baina ya bodaboda na Jeshi la Polisi hasa katika mapambano dhidi ya uhalifu sambamba na kupunguza matukio ya ajali za barabarani.
Amesema vitendo vya uhalifu wa barabarani kwa baadhi ya vijana hutokana na mihemko ya ujana akitolea mfano kupasua mfumo wa upumuaji maarufu kwa jina la exosti na kulipua milipuko mikubwa mithili ya baruti, ambapo vitendo hivyo huleta usumbufu na taharuki kubwa kwa watu wengine hususani maeneo ya mahospitali.
Sambamba na hilo pia amewataka waendesha bodaboda hao kuwa na nidhamu ya kazi, kuithamini na kuikubali biashara hiyo ya kubeba abiria kuwa ni kazi na ajira rasmi hivyo wasiwafumbie macho wale wachache ambao wanaharibu biashara hiyo kwa kutenda uhalifu.
Aidha ametoa wito kwa vijana kutambua kuwa wao ni sehemu ya jamii, hivyo wanawajibu mkubwa wa kufichua wahalifu na matukio ya uhalifu katika maeneo yao ili Jiji la Arusha liendelee kuwa shwari hasa kwa kuzingatia ni kitovu cha utalii nchini.
“Hawa vijana ambao wanafanya mihemko na kufanya uhalifu wa barabarani ama wa kijinai wanatoka katika jamii, kwaiyo muwe wa kwanza katika kuchukia vitendo hivyo, tufikishieni taarifa sisi jeshi la Polisi kwa mficho ili tuweze kuwafikia wale watu wachache ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.” Alisisitiza SP Mwangamilo.
Kwa upande wake Bwana Hemed Mbaraka ambaye ni Katibu wa bodaboda kata ya Levolosi amesema kutokana kikao hicho jiji la Arusha linaenda kubadilika kwani wao kama bodaboda wataenda kuhimizana katika suala la utii wa sheria sambamba na kukemea matendo mengi ya kiuhalifu ambayo yalikuwa yanaonekana yanatendwa na bodaboda.
“Sasa tunakwenda kama bodaboda kuhimizana wenyewe kwa mujibu wa maelekezo ya kuhakikisha tunakwenda kumaliza matatizo yote”. Alisisitiza Bwana Hemed.
Naye bwana Johnson Lema dereva bodaboda toka kituo cha Namanga amesema watahakikisha wanaenda kushirikiana na Jeshi la Polisi kukamata pikipiki zote zinazotenda uhalifu hususani zile ambazo zinatoa milio mikubwa na kuzifikisha katika vituo vya Polisi.
Pia ameliomba Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua baadhi ya bodaboda ambao wanatabia ya kuvamia vituo ambavyo hawajasajiliwa baada ya kutenda uhalifu katika maeneo yao.
Bwana Fred Mollel ambaye ni mkazi wa Arusha amelipongeza Jeshi la Polisi kwa elimu ambayo wameitoa kwa bodaboda hao na kufafanua kuwa wengi hawafuati sheria za usalama barabarani hali ambayo inapelekea ajali nyingi kutokea, hivyo ametoa rai kuwa elimu hiyo iwe endelevu kwa bodaboda wote.
Kikao hicho ambacho kimehudhuriwa na madereva bodaboda zaidi ya 100 ni muendelezo wa vikao vya Mkuu wa usalama barabarani Mkoa wa Arusha na wadau wa usalama barabarani hususani makundi ya bodaboda ambavyo vinafanyika kila wiki.