Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Kilimo cha parachichi kinaendelea kukua hasa katika nchi za Afrika Mashariki, Pia kilimo hichi hakihitaji fedha nyingi na subira ya ukuaji wa matunda haya mara nyingi huambatanishwa na faida kubwa wakati wa mavuno.
Kwa Tanzania, kilimo hichi kimeanza kushika kasi zaidi mwaka 2015 ambapo baadhi ya watu walijitokeza na kuelezea mafanikio waliyopata kutokana na kilimo cha parachichi.
Nchi za Ulaya kama Denmark, Ufaransa, Uingereza, Norway na Uholanzi zimeonyesha kufurahishwa na maparachichi yanayotoka nchi za Afrika Mashariki hususani Tanzania. Mikoa iliyojikita zaidi na uzalishaji wa zao hili ni Kilimanjaro, Mbeya, Njombe na Iringa, hii ni kutokana na hali ya hewa ya baridi iliyopo katika mikoa hiyo.
Kufuatia umuhimu huo wa zao la parachichi Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda leo tarehe 3 Juni 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe Queen Sendika Ofisini kwake Jijini Dodoma.
Katika mazungumzo yao Waziri Mkenda amemuhakikishia Rc Sendika kuwa Wizara ya Kilimo imejipanga kuimarisha sekta hiyo katika zao la Parachichi ambapo miongoni mwa mikoa ya kimkakati katika zao hilo ni pamoja na mkoa wa Iringa.
Kadhalika Waziri Mkenda amesema kuwa atafanya mashauriano na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) ili kujua nini kinahitajika kwa ajili ya kuanzisha vitalu vya uzalishaji mbegu mkoani Iringa vitakavyorahisisha upatikanaji wa miche ya parachichi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe Queen Sendiga ambaye katika mazungumzo hayo aliambatana na Katibu Tawala wa Mkoa huo Bi Happiness Seneda amesema kuwa Mkoa wa Iringa hutegemea miche ya Parachichi kutoka mikoa ya Njombe na Iringa hivyo jambo hilo huchelewesha kasi ya uzalishaji wa Parachichi.
Kufuatia changamoto hiyo Rc Sendika amemueleza Waziri Mkenda kuhusu uhitaji wa miche mingi ya Parachichi ikwiemo uwezekano wa kuanzisha vitalu vya kuzalisha miche hiyo kwa wingi mkoani Iringa.
Wapewe jicho la pekee kupatiwa miche na ikiwezekana kuwe na uzalishaji wa miche ya Parachichi Mkoani Iringa
Amesema kuwa wakulima wengi wanaojihusisha na kilimo hicho huuza katika soko la nje hivyo kuna umuhimu kwa serikali kuwezesha vijana nchini hasa wasio na kazi za kuajiriwa kujihusisha na kilimo hiki kwa kuwa hakina gharama.