WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais,Muungano na Mazingira Selemani Jafo,akizungumza wakati akifungua Kikao kazi cha maafisa Mazingira kilichofanyika leo June 3,2021 jijini Dodoma.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Dkt Festo Dugange,akielezea umuhimu wa kutunza mazingira wakati wa kikao kazi cha maafisa Mazingira kilichofanyika leo June 3,2021 jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais,Muungano na Mazingira Marry Maganga, akizungumza katika Kikao kazi cha maafisa Mazingira kilichofanyika leo June 3,2021 jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki wakifatilia Hotuba ya Waziri wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais,Muungano na Mazingira Selemani Jafo, wakati akifungua Kikao kazi cha maafisa Mazingira kilichofanyika leo June 3,2021 jijini Dodoma.
……………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais,Muungano na Mazingira Selemani Jafo amewataka maafisa Mazingira katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 inasimamiwa katika maeneo yao ili kutekeleza Kampeni Kabambe ya kudumu ya Usafi na Utunzaji wa Mazingira.
Kauli hiyo ameitoa leo June 3,2021 Jijini Dodoma wakati wa akifungua Kikao kazi cha maafisa Mazingira amesema kuwa utunzaji wa Mazingira ni ajenda muhimu ambayo maafisa hao wanapaswa kuisimamia ili iweze kutekelezeka.
Amesema kuwa mazingira ni muhimu na dunia inataabika na uharibifu wa mazingira ikiwemo uharibifu wa misitu ya asili na ya kupanda ambayo inachomwa moto na hivyo kusababisha hali ya mazingira kuwa mbaya katika maeneo mbalimbali.
Jafo amesema kuwa chanzo kikubwa cha mifereji ya kupitishia maji kuziba ni kutokana na kutokuwa na njia sahihi za usafi wa majumbani katika familia kutokana na baadhi ya watu kutupa taka kwenye miferi hiyo.
“Tinajifariji kuwa tunapanda miti milioni moja na laki tano lakini ukienda mwaka mwingine hata miti laki tano hauikuti katika utunzaji wa mazingira tunamambo mengi ya kufanya ndio maana katika ofisi yangu ninajukumu la kuwateuwa watu wanaoweza kutunza mazingira na nimefanya ili kufanya jambo hili kwa usahihi lazima upate watu sahihi”amesema Jafo
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Dkt Festo Dugange amezitaka Mamlaka za mitaa na sekretarieti za Mikoa kuifanya ajenda ya utunzaji wa mazingira inakuwa ya kila siku.
“Mamlaka za mitaa zishirikiane katika kampeni hii,zitumie Sheria ndogo kuwachukulia hatua wote watakaoshindwa kutimiza wajibu wao,wenyeviti,mameya na viongozi wengine wahakikishe suala la Usafi,usimamizi na Utunzaji wa Mazingira linapewa nafasi ya kwanza na linatekelezwa kwa vitendo,”ameeleza
Pia amezielekeza mamlaka zote zielekeze Shule pamoja na Vyuo kama bado wanatumia mkaa na kuni waache na waanze kutumia nishati mbadala pamoja na kuandaa mkakati wa kuelimisha kupitia njia mbalimbali kama vyombo vya habari ,ngoma na matangazo ya mabango.
Awali Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais,Muungano na Mazingira Marry Maganga amesema kuwa semina hiyo ina lengo la kujadili na kutoa mapendekezo katika changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo katika maeneo yao na kuzipatia ufumbuzi.