TUME ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza Ratiba
ya uchaguzi mdogo wa Ubunge wa Jimbo la Konde, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa
Kaskazini Pemba na Kata 6 za Tanzania bara.
Tayari Tume imekwisha kupokea Barua kutoka
kwa Spika wa Bunge kuwa kiti hicho kiko wazi.
Taarifa iliyotolewa kwa Vyombo vya habari
Jijini Dodoma leo, 3 Juni, 2021, na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi, Dkt. Willson Mahera imesema uchaguzi huo umeapangwa
kufanyika tarehe 18 Julai,2021.
“Tume
ilipokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
ambaye kwa kuzingatia kifungu cha 37 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura
ya 343, ameitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi ya kiti cha Ubunge katika Jimbo
la Konde, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba,” alisema Dkt Mahera.
Kiti cha Mbunge wa Jimbo la Konde, Wilaya ya
Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba kiko wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge
wa Jimbo hilo, Khatib Said Haji na hivyo kukoma kuwa Mbunge kwa mujibu wa Ibara
ya 71(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Aidha, Tume imepokea barua kutoka kwa Waziri
mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa akiitaarifu juu ya
kuwepo kwa nafasi wazi za Madiwani kwenye kata sita (06) za Tanzania Bara.
“Kwa kuzingatia masharti ya Kifungu cha
37(1)(b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Kifungu cha 13 (2) cha
Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, Tume imeandaa chaguzi
ndogo ili kujaza nafasi ya Mbunge iliyo wazi katika Jimbo la Konde na nafasi za
udiwani kwenye Kata sita (06) za Tanzania Bara,” alisema taarifa hiyo ya Dkt.
Mahera.
Kata zitakazohusika katika uchaguzi huo ni
Kata ya Mbagala Kuu Jimbo la Mbagala Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam, Kata
ya Diringish iliyopo jimbo la Kiteto, Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, Kata ya
Mitesa, Jimbo la Lulindi, Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.
Kata nyingine ni Kata ya Gare, jimbo la
Lushoto Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, Kata ya Mchemo,Jimbo la Newala
Vijijini, Wilaya ya Newala mkoani Mtwara na Kata ya Chona, Jimbo la Ushetu,
Wilaya ya Ushetu mkoani Shinyanga.
Maandalizi kwaajili ya uchaguzi huo yameshafanyika na kazi ya utoaji fomu za uchaguzi kwa
wagombea inaanza Juni 21 hadi 27,2021huku uteuzi wa wagombea watakao wania
nafasi hizo ukifanyika Juni 27 mwaka
huu.
Aidha Dkt Mahera amesema kampeni za uchaguzi
katika jimbo la Konde na Kata utaanza Juni 28, 2021 na zitafikia ukomo wake Julai
17 mwaka huu na uchaguzi kufanyika 18 Julai,2021.
Mahera
alisema yayari Tume imekwisha vitaarifu Vyama vya Siasa kwa njia ya barua juu
ya kuwepo kwa uchaguzi huo mdogo na inavikumbusha kuzingatia sheria, kanuni,
Maadili ya Uchaguzi, Miongozo na Maelekezo ya Tume wakati wote wa kipindi cha
Uchaguzi.