***********************************
Mnamo mwezi Desemba 2019, Benki Kuu ya Tanzania ilitoa Taarifa kwa Umma kuhusu Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018 iliyoanza kutumika rasmi tarehe 1 Novemba 2019. Pamoja na mambo mengine, taarifa hiyo ilirejea Kifungu cha 57 cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ambacho kinawataka watoa huduma ndogo za fedha wote kuwasilisha maombi ya leseni au usajili Benki Kuu ya Tanzania au kwenye Mamlaka Kasimishwa katika kipindi cha miezi 12 baada ya Sheria kuanza kutumika, yaani tarehe 31 Oktoba 2020. Muda huu uliongezwa kwa miezi sita hadi 30 Aprili 2021 ili kuwapa watoa huduma ndogo za fedha katika madaraja yote muda wa ziada wa kuandaa na kuwasilisha maombi ya usajili na leseni kwa Mamlaka za Usajili na Usimamizi.
Kutokana na changamoto zilizojitokeza katika usajili wa vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha, Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango ameridhia kuongeza muda wa miezi sita zaidi kwa ajili ya usajili wa vikundi hivi. Hivyo, muda wa mwisho wa usajili wa vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha ni tarehe 30 Novemba 2021. Muda huu wa ziada hauhusu watoa huduma ndogo za fedha wa daraja la pili wala la tatu.
Ni matarajio ya Benki Kuu ya Tanzania kuwa vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha vitatumia vizuri muda huu wa ziada kukamilisha na kuwasilisha maombi ya usajili kwa njia ya kielektroniki kupitia https://cmg.bot.go.tz/cmg-portal/login. Aidha, vikundi vitakavyopata changamoto yoyote katika kuwasilisha maombi ya usajili kwa njia ya kielektroniki vinashauriwa kuwasiliana na Maafisa Maendeleo ya Jamii au Maafisa TEHAMA katika Halmashauri iliyoko karibu ili kupata msaada.
Benki Kuu inaendelea kuutahadharisha umma kuhusu matangazo na maelekezo yenye kupotosha na kuleta taharuki yanayotolewa na watu wasiokuwa na nia njema kuhusu dhana na madhumuni ya usajili wa watoa huduma ndogo za fedha. Badala yake, wananchi wanashauriwa kuwasiliana na Mamlaka husika pale wanapohitaji maelezo au wanapokutana na changamoto mbalimbali katika mchakato wa maombi ya leseni au usajili wa huduma ndogo za fedha.
Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:
- Mkurugenzi wa Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania, S.L.P. 2939, Dar es Salaam au wasilisha barua pepe kwa [email protected]; [email protected]; [email protected]; na [email protected]
- Mkurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, S.L.P 1923, 41185 Dodoma au wasilisha barua pepe kwa [email protected] au [email protected]
- Mrajis, Tume ya Maendeleo ya Ushirika, S.L.P 201 Dodoma au wasilisha barua pepe kwa [email protected] au [email protected]