*******************************
Na Damian Kunambi, Njombe.
Wakazi wa kata ya Milo wilayani Ludewa mkoani Njombe wamelalamikia uhaba wa magari ya kusafirishia abiria kutoka Njombe mpaka Milo kutokana na ubovu wa baraba hiyo na kupelekea kutumia gharama kubwa ili kuweza kusafiri na kukwamisha usafirishaji wa mazao.
Wakitoa malalamiko hayo katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na diwani wa kata hiyo Robert Njavike na kuhusisha viongozi wa vijiji na serikali wa kata hiyo uliolenga kusikiliza kero mbalimbali walizonazo wananchi wa kata hiyo.
Jackson Mgimba ni mmoja wa wananchi hao amesema kuwa awali magari yalikuwa mengi na walikuwa wakisafiri kwa gharama ya shilingi elfu tano hadi sita lakini kwa sasa wanasafiri kwa elfu 12 hadi 15 hivyo wanashindwa kusafiri na kusafirisha mazao yao ya biashara.
“Huku magari ni shida sana kutokana na ubovu huu wa barabara ambapo kwa sasa kuna gari moja tu! ambalo halikidhi mahitaji ya wananchi kutokana na wingi wetu, hivyo tunaomba serikali itutengenezee barabara ili tuweze kusafiri kwa gharama nafuu kama wenzetu wa maeneo mengine”. Alisema Mgimba.
Naye Edward Mwinuka ambaye mdau wa usafirishaji abiria amesema kuwa kuna baadhi ya wasafirishaji wamekuwa wakiwawekea vikwazo wenzao ili kuwakwamisha kufanya shughuli hizo na wabakie wao tu.
Akizungumzia suala hilo diwani wa kata hiyo Robert Njavike amesema tatizo hilo la ubovu wa barabara alishalifikisha TARURA ambapo wapo mbioni kuja kufanya matengenezo hayo.
Aliongeza kuwa kata hiyo inazalisha mazao mengi ya kibiashara kama njegele, mahindi, ngano pamoja na viazi hivyo uwepo wa usafiri ni muhimu sana kwa wananchi hao.
“Najua wananchi wangu changamoto hii inawapa shida sana hivyo mimi nitahakikisha barabara inatengezwa kwa muda muafaka lakini pia nitazungumza na wadau mbalimbali wa usafiri ili walete magari na mpate ahueni ya gharama”, Alimsema Njavike.
Sanjali na suala hilo la barabara pia diwani huyo alizielezea changamoto nyingine zilizotolewa na wananchi hao za umeme, maji na nyinginezo kuwa mbunge wa jimbo hilo Joseph Kamonga amekuwa akizipokea na kuziwasilisha ngazi za juu ikiwemo kuwakutanisha na mawaziri wa wizara mbalimbali.
Amesema mbunge huyo aliwapeleka madiwani wote bungeni Dodoma na wamekutana na waziri wa nishati benard kalemani na alipomueleza tatizo la umeme katika kata hiyo amesema mwaka huu milo lazima iongezwe kwenye grid ya taifa na hawatatumia tena umeme mbadala.
Pamoja na majibu hayo ya waziri lakini mbunge huyo aliongozana naye mpaka kwa mkurugenzi wa tanesco Dr. Mwinuka ambapo alikili kulifahamu tatizo la umeme Milo na kuahidi kulishughulikia.
Aidha juu ya changamoto ya maji diwani kasema mbunge huyo pia aliwakutanisha na waziri wa maji Juma Aweso na alipomueleza juu ya tatizo hilo la wananchi wa Milo hasa kwenye vijiji vya mapogoro na mavala waziri huyo amekubali kutatua changamoto hiyo.
” Kwakweli mbunge wetu anafanya kazi kubwa sana! Na nimekuwa nikimjulisha changamoto mbalimbali za wanamilo amekuwa akizishughulikia kwa kufikisha katika ngazi mbalimbali zinazohusika”, Alisema Njavike.