Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akisisitiza jambo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Anastazia James Wambura, jijini Dodoma, kuhusu ubovu wa barabara ya Kibiti – Lindi na mpango wa Serikali unaochukuliwa kutatua tatizo hilo.
………………………………………………………………………….
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, amewataka wasafisrishaji kutumia Bandari ya Mtwara kwa ajili ya kusafirisha mizigo yao ndani na nje ya nchi ili kunusuru barabara barabara ya Lindi – Kibiti kuharibika mara kwa mara.
Ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Anastazia James Wambura, lililouliza ni nini sababu ya barabara ya Kibiti hadi Lindi kuharibika mara kwa mara licha ya kufanyiwa ukarabati, Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua tatiza hilo ili kuzuia ajali za mara kwa mara katika barabara hiyo?
Kasekenya amefafanua kuwa kwa sasa Barabara ya Lindi hadi Kibiti inapitisha magari mengi na yenye uzito mkubwa zaidi ya ilivyokusudiwa wakati wa usanifu uliotumika kujenga barabara hiyo na kwamba hali hiyo inatokana na uwekezaji mkubwa wa viwanda na migodi katika mikoa ya Kusini na nyanda za juu Kusini uliojitokeza miaka ya hivi karibuni baada ya ujenzi wa barabara hii kukamilika.
“Ujenzi wa viwanda vikubwa kama cha Dangote mkoani Mtwara na uwepo wa migodi mikubwa ya Makaa ya Mawe mkoani Ruvuma kumechangia ongezeko la magari yanayobeba uzito mkubwa kuliko ilivyotarajiwa wakati barabara hii inafanyiwa usanifu”, amesema Kasekenya.
Naibu Waziri huyo ameliambia Bunge kuwa ili kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa barabara hiyo kwa sasa, Serikali inaendelea na mpango wa ukarabati mkubwa utakaowezesha barabara hiyo kustahimili wingi na uzito wa magari.
Katika mwaka wa fedha 2021/22 zaidi ya shilingi Bilioni Saba zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa barabara ya Lindi hadi kibiti.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.