………………………………………………………………
- Sasa kutumika katika mikutano ya Umoja wa Afrika
Georgina Misama- MAELEZO
Kiswahili ni kati ya lugha zinazokua kwa kasi siku hadi siku, inakadiriwa kwamba zaidi ya watu milioni 100 barani Afrika wanatumia lugha ya Kiswahili ama kama lugha mama au lugha rasmi.
Tanzania imekuwa nchi ya kwanza katika eneo la jangwa la Sahara kutumia Kiswahili kama lugha rasmi na lugha mama ambapo kinatumika pia katika mtaala wa elimu kwa shule za msingi kinatumika kama somo kwa shule za sekondari badala ya Kiingereza.
Uamuzi wa Tanzania kutumia lugha ya Kiswahili kama lugha rasmi ya mawasiliano katika shughuli za Serikali ulikuja baada tu ya kupata uhuru wake 1961, ambapo wakati huo lugha iliyokuwa ikitumika zaidi ilikuwa Kiingereza. Watoto wa shule walitarajiwa kujifunza Kiingereza katika shule za msingi na Kiswahili katika shule za sekondari. Hata hivyo, Serikali ilibaini kwamba uelewa wa watoto kwenye lugha ya Kiingereza ni mdogo hivyo kupelekea ufaulu wao katika masomo yanayofundishwa kwa lugha hiyo kufifia. Ni kwa msingi huo Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere iliamua kubadilisha matumizi ya Kiswahili na kukifanya kuwa lugha rasmi katika mtaala wa elimu.
Umuhimu wa lugha ya Kiswahili, uliifanya Serikali kuamua kuanzisha Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) mnamo mwaka 1967, ili Baraza hilo liweze kuendeleza, kustawisha na kuimarisha lugha hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa Tanzania inatumia Kiswahili sanifu.
Kutokana na lugha hii kufahamika na kupokelewa vizuri, Tanzania iliamua kuitumia kama lugha rasmi ya mawasiliano ambapo shughuli zote za kikazi zilianza kutumia Kiswahili ikitumika kama lugha ya kufundishia katika shule za msingi na kama mojawapo ya somo katika shule za sekondari. Aidha, lugha hii ya kibantu iliendelea kusambaa na kuenea katika nchi za Afrika Mashariki, Afrika ya Kati na baadhi ya nchi za Falme za Kiarabu. Nchi za Afrika Mashariki zinazotumia lugha hii kwa wingi ni pamoja na Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi. Nchi nyingine zinazotumia lugha hii ni Msumbiji, Oman, Somalia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Afrika ya Kusini kikizungumzwa na watu takribani milioni 98.
Unapozungumzia kupanuka kwa wigo wa Kiswahili kuanzia Tanzania, Afrika Mashariki, Afrika mpaka duniani kwa upana wake, huwezi kuacha kumzungumzia Hayati Rais John Magufuli, ambaye alikuwa ni Rais wa Awamu ya Tano wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Hayati Magufuli aliweka wazi mtazamo na utashi wake kwenye matumizi lugha hii.
Alikipenda na alikipa kipaumbele Kiswahili wakati wote wa uongozi wake, ambapo ukiachilia mbali kwa yeye mwenyewe kuonyesha mfano kwa kutumia lugha hiyo wakati wote, lakini pia aliwahamasisha watu wote pamoja na wadau wa elimu kuhakikisha wanatoa kipaumbele kwa matumizi ya lugha hiyo ambapo hakuweza kutofautisha matumizi ya Kiswahili na uzalendo halisi.
Aidha, Rais Magufuli aliwatambua na kuwapokeza wasaidizi wake pindi wanapofanya vizuri kwenye matumizi ya lugha hiyo. Mfano halisi ni siku aliyohudhuria maadhimisho ya siku ya sheria nchini yaliyofanyika kitaifa jijini Dodoma Februari 2021. Alianza kwa kumpongeza kumpandisha cheo Mhe. Jaji Zepharine Nyalugenda Galeba aliyekuwa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma. Sababu kubwa ya kumpandisha cheo Jaji huyu cheo ni kutokana na kutumia Kiswahili katika kazi yake ya Ujaji.
“Nitumie fursa hii, kumpongeza sana Mheshimiwa Jaji Galeba wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma kwa kutumia Kiswahili katika kutoa hukumu kwenye Kesi ya North Mara Gold Mine dhidi ya Gerald Nzumbi katika kesi ya Mapitio Na. 23 ya Mwaka 2020. Huyu ni Mzalendo wa kweli wa lugha ya Kiswahili kwenye Mahakama. Na kwa sababu ya uzalendo wake, kuanzia leo, namteua kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa”, alisema Rais Magufuli.
Sambamba na pongezi hizo, Rais Magufuli alitoa wito kwa Watanzania wote na hasa watumishi wanaotoa huduma kwenye sekta za sheria kujitathimini na kuona umuhimu wa kutoa huduma hiyo kwa lugha ya Kiswahili kwani Watanzania wengi wanapoteza haki zao kwa kushindwa kuelewa lugha inayotumiwa na wataalam hao.
“Kushindwa kuitumia lugha ya Kiswahili kwenye masuala ya Kimahakama na Kisheria sio tu kunawanyima haki wananchi wanyonge, bali pia kunawaongezea gharama kupitia ukalimani wa kutafsiri hukumu na mienendo ya kesi zao”, alisisitiza Hayati Dkt. Magufuli.
Ukienda kwenye anga za kimataifa, ni Hayati Dkt. Magufuli ambaye aliweza kuwashawishi viongozi wa mkutano wa 39 wa Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kukubali Kiswahili kitumike katika mawasiliano ya Jumuiya hiyo ambapo Wakuu hao walilipitisha wazo hilo bila kupingwa na sasa lugha ya Kiswahili inatumika katika mawasiliano ya SADC.
Aidha mapenzi yake kwa lugha ya Kiswahili hakuweza kuyaficha hasa pale alipofanya ziara katika nchi mbalimbali hasa za Kusini mwa Afrika ambapo alidiriki kuwapatia vitabu vya Kiswahili baadhi ya marais. Alitoa vitabu kwa Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ili aweze kujifunza Kiswahili ambapo naye kwa kuonesha kulikubali wazo la Hayati Magufuli alisema nchi yake itaanza kutumia lugha ya Kiswahili kufundisha katika shule za msingi na sekondari ambapo hivi karibuni katika msiba wa hayati Magufuli alisema kwamba hilo limekwisha tekelezwa na somo la Kiswahili sasa linafundishwa kama somo shuleni nchini Afrika Kusini.
Lugha ya Kiswahili imeendelea kupiga hatua nyingine ambapo imechaguliwa kuwa lugha rasmi kutumika katika mikutano yote itakayoendeshwa na Umoja wa Nchi za Afrika (AU).
Akiongea na waandishi wa habari katika maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Afrika, yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula alisema kuwa nchi wanachama wa umoja huo zimekubaliana kutumia lugha ya Kiswahili kuendeshea mikutano yake yote.
“Kwa mara ya kwanza katika historia ya Afrika Kiswahili kama lugha halisi mojawapo ya kiafrika kimechaguliwa kuwa lugha rasmi itakayotumika katika mikutano yote ya Umoja wa Afrika ambapo siku za nyuma Kiswahili kilikuwa kinatumika kama lugha ya kazi na katika ngazi ya Mikutano ya Maraisi tu. Jambo hili ni la kujivunia kwa sisi Watanzania na Afrika kwa ujumla”, alisema Mulamula.
Uamuzi wa kukichagua Kiswahili umeenda sambamba na utekelezaji wa kauli mbiu ya maadhimisho ya siku hiyo kwa mwaka huu inayosema ‘Sanaa, Utamaduni na Urithi njia za Kuijenga Afrika tunayoitaka’.
Ukiachilia mbali, mchango mkubwa wa Hayati Dkt Magufuli ambao umeonyeshwa kwa uchache tu katika makala hii, kitu kikubwa kilichobakia ni jinsi sasa Kiswahili kinavyopaa kwenye Nyanja za Kimataifa. Watanzania hawawezi kuacha kujivunia mafanikio hayo kwani ndio waasisi wa lugha hiyo Afrika na duniani kwa ujumla.
Tanzania kama nchi mama ya lugha ya Kiswahili bado inaendelea kujiimarisha, sambamba na kuyasaidia mataifa mengine kujifuza lugha hiyo. Serikali kupita Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) imefungua kituo cha kufundisha, kutaini na kupima ujuzi kwa wageni kutoka katika mataifa mbalimbali wanaofika hapa nchini na kuonyesha nia ya kujifunza lugha hii.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti hivi karibuni Bungeni Dodoma, Waziri wa Habari, Utamaduni ,Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amesema kwamba Serikali imetoa mwongozo wa Kitaifa wa kufundisha Kiswahili kwa wageni na tayari umeshaanza kutumika na vituo vinavyofundisha Kiswahili nchini ili kuleta ufananivu wa ufundishaji wa lugha hiyo.
“Mwongozo huu tayari umeanza kutumiwa na vituo vinavyofundisha Kiswahili kwa wageni ndani na nje ya nchi. Pia, umesambazwa kwenye balozi za Tanzania katika nchi za Namibia, Burundi na Korea Kusini. Balozi hizi ni zile ambazo tayari zimeanzisha vituo vya kufundisha Kiswahili au zipo katika maandalizi ya kufungua vituo hivyo,” anasema Mhe. Bashungwa.
Amebaisha kwamba mafunzo ya kuimarisha stadi za kufundisha Kiswahili kwa wageni yalitolewa kwa wataalamu 48 wa mkoani Dar es Salaam na Tanga. Mikoa mingine iliyokwishapatiwa mafunzo hayo tangu mwaka 2018/2019 ni Dar es Salaam,Mwanza, Mbeya, Arusha na Iringa ambapo hadi sasa idadi ya wataalamu waliosajiliwa ni 1,318. BAKITA inaendelea kutoa mafunzo haya katika Mikoa mingine katika mwaka 2021/22.
Ukiangalia ukuaji wa lugha ya Kiswahili katika jicho la kijasiriamali, unaioa fursa ya wazi katika maeneo mbalimbali yanayoambatana na kukua kwa lugha hii. Watanzania huu ndio wakati wa kijipambanua na kujikita katika katika maeneo mbalimbali kama kufundisha, kutafsiri na kuandika vitabu au nyaraka mbalimbali muhimu katika kujifunzia. Fursa nyingine zinazoweza kupatikana katika kupanua lugha hiyo ni pamoja na kukalimani, kutengeneza mifumo ya kufundishia ya kidigitali na kuuza nyaraka na vifaa.
MWISHO