************************
Na Mwandishi wetu, Longido
Zaidi ya Wanariadha 350 walioshiriki Katika Mashindano ya Riadha ya OLARD RUN LONGIDO 2021 yaliyofanyika 31/05/2021 wamepatiwa Elimu ya Uchangiaji Damu pamoja na zoezi la Uchangiaji Damu katika Viwanja vya Shule ya sekondari Longido,Elimu ambayo Ilitolewa na DKT JUMA MUNA ambaye Ni Mganga Mfawidhi Hospitali ya ELI SPECIALIZED POLYCLINIC iliyopo Ngaramtoni Mkoani Arusha.
Katika Mashindano hayo ya riadha mbali na kutangaza utalii wa ndani lengo lingine ilikuwa ni kuhamasisha upimaji wa afya kwa wana riadha hao pamoja na wananchi wote lengo likiwa Ni kupambana na magonjwa yasiyoambukiza hasa shinikizo la juu la damu, kisukari na saratani mbalimbali.
Katika elimu hiyo ya uchangiaji damu Dkt Muna amesema Ni wakati sasa wa wana michezo kote nchini kutumia majukwaa ya kimichezo Kupambana na magonjwa mbalimbali hasa ya kisukari na shinikizo la juu la damu pamoja na kushiriki katika zoezi la uchangiaji damu ili kuokoa maisha ya mama na mtoto.
Dkt Muna alisema zoezi la Uchangiaji Damu Ni salama na lina faida nyingi kiafya ikiwepo kuokoa maisha ya wapendwa wetu, kuongeza kinga ya mwili (Body immunity) kwa kutengenezwa kwa seli mpya nyeupe bila kusahau kupunguza uwezekano wa mtu kupata magonjwa ya mishipa ya damu hasa ya moyo, kiharusi na kupunguza uwezekano wa kupata Saratani mbalimbali pale mtu anapochangia damu.
Kupitia mashindano hayo Dkt Muna ametoa wito pia kwa waandaji wa mashindano mbalimbali ya Kimichezo hasa Riadha na michezo mingine kutoa fursa kwa washiriki wa michezo hiyo kupima Afya zao hasa magonjwa ya moyo ili kuepusha athari mbalimbali za magonjwa hayo kwa wana michezo hasa kifo cha ghafla kutokana na maradhi mbalimbali hasa maradhi ya moyo (Sudden Cardiac death)
Mashindano hayo yalihidhuriwa na wanariadha zaidi ya 350, ambapo yalihudhuriwa na mgeni rasmi Mkuu wa wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe ambaye pia alishiriki mashindano hayo.